The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Askari wa Uhifadhi Kilwa Wadaiwa Kukiuka Haki za Binadamu Wakihamisha Wananchi Kwenye Ardhi Yenye Mgogoro

Wananchi wamelalamika kupigwa na kubolewa nyumba zao na askari wa hifadhi ikiwa ni sehemu ya kuwalazimisha wahame kwenye ardhi yao.

subscribe to our newsletter!

Lindi. Watu kuvunjiwa nyumba zao, wengine kupigwa mpaka hawawezi tena kutembea, huku baadhi wakipokonywa mali zao kama vile pikipiki, ni baadhi tu ya shutuma nzito ambazo wananchi wa Mtepera, wilayani Kilwa, mkoani hapa wamezielekeza kwa askari wa uhifadhi wanaodaiwa kutekeleza vitendo hivyo kulazimisha wananchi waondoke kwenye ardhi yenye mgogoro.

Kikiwa na wakazi wanaokadiriwa kufika 2,000, kijiji cha Mtepera kinapatikana Kaskazini-Magharibi mwa mkoa wa Lindi, umbali wa takriban kilomita 200 kutoka Manispaa ya Lindi, ambako ndiko yaliko Makao Makuu wa mkoa huo ulioanzishwa Julai 1, 1971. Kijiji hicho pia kinapakana na Hifadhi ya Wanyamapori Selous ambayo askari wake wamelalamikiwa kutekeleza vitendo hivyo vya kikatili.

Wakazi wa kijiji hiki, ambao wanadai kuishi hapa kabla hata ya uhuru, wapo kwenye mvutano mkubwa na hifadhi hiyo ambayo inadaiwa kumega eneo lenye ukubwa wa takriban ekari 18,000, ikisema ni eneo la hifadhi, hali iliyopelekea kaya zipatazo 150 kukosa makazi baada ya kulazimishwa kuhama kutoka kwenye eneo hilo.

Mnamo Agosti 2, 2023, The Chanzo ilifika kwenye eneo hilo linalozua mgogoro na ambalo Hifadhi ya Wanyamapori Selous imepiga marufuku watu kuwepo hapo ambapo ilikuta mabaki ya nyumba zilizobomolewa, huku kukionekana mabaki kama vile mabati na kuta za nyumba zikiwa zimelala chini.

Saidi Mbyoko, mmoja kati ya wananchi wa kijiji cha Mtepera, akiwa anakagua moja ya nyumba zake zinazodaiwa kubomolewa na askari wa uhifadhi. PICHA | OMARI MIKOMA

SOMA ZAIDI: Serikali, Wananchi Wavutana Kuhusu Uhalali wa Kukalia Eneo la Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo – RAZABA

The Chanzo iliweza kufika kwenye eneo hilo baada ya wananchi kusema kwamba muda huo kunakuwa hakuna askari wa uhifadhi. Wananchi walidai kwamba endapo kama askari hao watawakuta kwenye eneo hilo basi huwatoza faini wananchi hao na kuwafanyia vitendo vingine vya kikatili.

Wananchi waliokuwa wakiishi kwenye eneo hili, ambalo lilikuwa na vitongoji viwili vya Namalonji na Mnanda, kwa sasa wengi wao wanaishi kwa ndugu na jamaa zao wilayani Kilwa, huku wengine wakijenga vibanda vya kujistiri kwenye eneo la kijiji hicho cha Mtepera ambalo halina mgogoro. Eneo hilo linatenganishwa na lile lenye mgogoro na Mto Matandu.

Hatuna pa kwenda

Mmoja kati ya wananchi waliolazimishwa kuhama kwenye eneo hilo, Holo Gwesu, amelilalamikia zoezi hilo kutokuwa shirikishi, akidai kwamba askari wa uhifadhi waliwapa notisi ya siku moja tu kuhama kwenye eneo hilo, hali anayosema imemuathiri sana kimaisha.

“Kule ambako tulikuwa tunakaa, tulikuwa tunalima; tulikuwa wafugaji, tuna ng’ombe,” alisema mama huyo wa watoto watatu. “Lakini tulishitukia siku moja, tukakuta magari na mapolisi, tukaambiwa tuhame. Tukaomba mashamba tuvune, wakatukatalia.”

“Ikabidi tukaondoka tu, chakula tukaacha, tembo wakala, kulikuwa na shamba la mtama na shamba la viazi, tembo wameshakula,” Gwesu, 52, alilalamika. 

“Sasa hivi hatuna hata sehemu ya kwenda,” aliendelea kulalamika mama huyo. “Hapa tulipo, mnapotuona hapa, hizi nyumba tumepewa tu [na wasamaria wema], tukaambiwa tujisimamie kwa mwezi mmoja ili tuangalie tunaenda wapi.”

Mabaki ya makazi yanayotajwa kuharibiwa na Askari wa Uhifadhi

SOMA ZAIDI: Wananchi, Wawekezaji Wavutana Ulipaji Fidia Mradi wa Uchimbaji Mchanga Kigamboni

Hatua ya askari wa uhifadhi kuhamisha wananchi kutoka eneo hilo ilitokana na ziara ya mawaziri nane wa kisekta iliyotembelea kijijini hapo mnamo Disemba 30, 2022, ambapo aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Angeline Mabula, alipiga marufuku wananchi kuishi karibu na maeneo ya vyanzo vya maji na hifadhi.

“Kwa sababu kijiji kina eneo kubwa, ambalo watu bado wanaweza wakapangwa [na] wakakaa vizuri, hakuna sababu ya kujibana kwenye mto, matokeo yake tunaharibu mazingira,” alisema Mabula ambaye nafasi yake kwa sasa inashikiliwa na Mbunge wa Ukonga (Chama cha Mapinduzi – CCM), Jerry Silaa.

Uonevu mkubwa

Hata hivyo, wanakijiji wameieleza The Chanzo kwamba zoezi la kuwahamisha kwenye eneo hilo limegubikwa na uonevu mkubwa, huku askari wa uhifadhi wakilalamikiwa kuwakamata wananchi kiholela, kuwaweka ndani pasi na sababu za msingi, kuwapiga na hata kuwanyang’anya mali zao.

Mmoja kati ya wanakijiji hao, Abdallah Mpacha, aliiambia The Chanzo kwamba askari wa uhifadhi walimkamata yeye akiwa na wenzake na kuwapeleka kwenye kambi zao ambapo anadai waliwatesa kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa nane mchana.

Abdallah Mpacha, ambaye anadai kupigwa na kunyang’anywa pikipiki yake na askari wa uhifadhi, akielezea mkasa huo kwenye mahojiano na The Chanzo. PICHA | OMARI MIKOMA

“Tulipigwa sana hata kutembea mimi nilikuwa nashindwa,” Mpacha, ambaye anafanya kazi kama dereva wa bodaboda, alisema. “Karibu miezi mitatu nilikuwa siwezi kutembea mimi, nilikuwa nakaa tu.”

SOMA ZAIDI: Kuwaondoa Wananchi Ngorongoro ni Shambulio Dhidi ya Ufugaji wa Asili

Baba huyo wa watoto nane aliongeza kwamba baada ya kuteswa huko, yeye na wenzake walipelekwa Kituo cha Polisi cha Kilwa Masoko na kuswekwa mahabusu, akitakiwa kutoa Shilingi 1,400,000 kwa ajili ya kupata dhamana kwa kosa la kutembea kwenye eneo la hifadhi.

Mpacha na wenzake waliweza kuachiwa na polisi baada ya kulipa fedha hizo lakini alishindwa kurejeshewa pikipiki yake baada ya askari kusema kwamba pikipiki hiyo itaendelea kubaki kuwa mali ya Serikali kwani Mpacha alikiuka sheria kwa kuiendesha kwenye eneo la hifadhi.

“Ikabidi nirudi nyumbani na madonda yangu,” Mpacha, 41, alinung’unika. “Ile pikipiki ilikuwa inanisaidia sana mimi na familia yangu. Sasa napata shida sana. Kwa hiyo, nilikuwa naiomba Serikali nisaidiwe niweze kurudishiwa pikipiki yangu.”

Mwanakijiji mwingine, Fitina Nguku, alihadithia namna askari wa uhifadhi walivyomkamata yeye na mwenzake hapo Julai 7, 2022, ambapo waliwapiga sana na kuwapokonya vitu walivyokuwa navyo, ikiwemo viatu vyenye thamani ya Shilingi 50,000 ambavyo Nguku alikuwa amebeba.

Nguku, 53, anadai aliwekwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Kilwa Masoko kwa siku 12 na jela kwa siku 16 kabla ya Mahakama ya Wilaya haijamfutia kesi. Lakini baada tu ya Mahakama kumfutia kesi, askari walimkamata muda huo huo na kumpeleka Lindi ambapo aliunganishwa kwenye kesi nyingine akiwa na wenzake 16.

SOMA ZAIDI: Serikali Wilayani Mbozi Yadaiwa Kuhamisha Wananchi kwa Nguvu Kupanua Hifadhi ya Kimondo

“Novemba 14, [2023], ile kesi ikawa imeisha,” alisema baba huyo wa watoto watano. “Tukapigwa faini ya Shilingi milioni moja na kitu, kwa wote. Tukalipa pale, tukarudi nyumbani. Kipindi chote wakati kesi inaendelea nilikuwa mahabusu, kwani sikuweza kupata dhamana.” 

“Kimwili, kiukweli nimeathirika sana kwa namna nilivyopigwa,” alisikitika mwanakijiji huyo. “Kiuchumi pia nimeathirika.”

Naye Pendo Masai, mkulima kutoka kwenye kijiji hicho cha Mtepera, alisimulia namna askari wa uhifadhi walivyomvamia nyumbani kwake, wakatoa vyombo kutoka kwenye nyumba hiyo kabla ya kuibomoa, wakisema notisi ya kuhama eneo hilo ilikuwa imepita.

“Kule [nilikohamishwa] mimi nilikuwa tu mkulima,” alisema mama huyo wa watoto wanne mwenye umri wa miaka 35. “Kuna mashamba yangu huko. Nimeacha ekari 70. Sasa sina nyumba, nimepewa tu hapa kwa muda. Sielewi lolote hapa nilipo.”

Uzushi

Hata hivyo, uongozi wa Hifadhi ya Wanyamapori Selous umekanusha vikali madai haya ya uvunjifu wa haki za binadamu, huku Jackson Msaki, Afisa Mhifadhi wa Selous Kanda ya Kilwa, akisema madai hayo hayana ukweli wowote.

“Tumefanya [zoezi hili la uhamishaji] kwa amani sana,” alisema Msaki kwenye mahojiano yake na The Chanzo yaliyofanyika kwa njia ya simu hapo Agosti 28, 2023. “Tulikuwa tunakubaliana, tunatoa muda na mwananchi ambaye bado hajavuna, tukampa muda akavuna mazao yake, ndiyo anaondoka.”

Kuhusu madai ya watu kupigwa na kunyang’anywa mali zao, Msaki alikanusha kwamba vitendo hivyo vimefanyika, akisema kwamba hakuna mtu alikamatwa wala kuchukuliwa mali zake.

SOMA ZAIDI: Mahakama Yaipiga ‘Stop’ Serikali Kuhamisha Wanavijiji Mbarali

The Chanzo ilimuuliza Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai, kama anafahamu malalamiko haya ya wananchi wa Mtepera ambapo alijibu kwamba taarifa hizo za ukiukwaji wa haki za binadamu ni za uongo zilizojaa upotoshaji.

“Hajapigwa mtu,” alikanusha Ngubiagai. “Hawajachomewa nyumba. Hajahamishwa mtu kwa nguvu, ila wameambiwa wasiingie kwenye hifadhi na kufanya shughuli yoyote hifadhini. Hiyo ndiyo hali halisi ya Mtepera.”

Lakini kwa mujibu wa Pili Mkemi, ambaye ni Mratibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), wilaya ya Kilwa, utaratibu huo wa uhamishaji wa wananchi kwenye kijiji hicho siyo tu haufati sheria bali pia una harufu ya ukiukwaji wa haki za msingi za binadamu.

“Namna wanavyofanyiwa wanakijiji, kiukweli, haizingatii misingi ya haki za binadamu,” Mkemi, ambaye amekuwa akilifuatilia sakata hilo kwa ukaribu, aliiambia The Chanzo. “Wanahamishwa bila kujua wataenda kukaa wapi. Wengine wameacha mazao shambani.”

“Ni wito wetu kama shirika kwamba ni muhimu kwa Serikali kufuata misingi ya haki za binadamu na utawala bora wakati wa kutekeleza zoezi hili,” aliongeza Mkemi. 

“[Wanakijiji] hawa ni walipa kodi wetu,” aliongeza afisa huyo. “Sasa tukiwafanyia mambo ambayo si mazuri, na wakawa kwenye njia panda ya kutojua hatima yao, kwa kweli tutakuwa hatuwatendei haki.”

Tatizo kubwa

Hii, hata hivyo, si mara ya kwanza kwa askari wa uhifadhi nchini Tanzania kudaiwa kukiuka haki za binadamu wakati wa kutekeleza majukumu yao, na wala Mtepera siyo sehemu pekee ya nchi ambapo wanakijiji wake wana migogoro na mamlaka za uhifadhi.

Mnamo Mei 30, 2023, kwa mfano, LHRC ilitoa tamko la kulaani ukiukwaji wa haki za binadamu uliokuwa ukifanywa na mamlaka za uhifadhi nchini kwa jamii za watu wanaoishi karibu na hifadhi za taifa na mapori tengefu. 

SOMA ZAIDI: Wakulima Wadogo 852 Mbarali Waiburuza Serikali Mahakamani Wakitetea Ardhi Yao

Kwenye taarifa yao hiyo, LHRC walisema kwamba matukio hayo mara nyingi huhusisha matukio ya watu kupigwa, kuuwawa, kudhalilishwa, kufukuzwa kwenye maeneo yao na kunyang’anywa mifugo kinyume cha sheria, ikiitaka Serikali kukomesha vitendo hivyo.

“Serikali iunde tume maalum, au kikosi kazi, kitakachofanya kazi ya uhakiki wa mipaka katika maeneno yote ya hifadhi na mapori tengefu ambayo kwa muda mrefu, na kwa nyakati tofauti tofauti, yamekuwa yakisababisha migogoro kati ya wananchi na askari wa mamlaka za wanayamapori,” LHRC ilishauri kwenye tamko lao hilo.

Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *