The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wakulima Wadogo 852 Mbarali Waiburuza Serikali Mahakamani Wakitetea Ardhi Yao

Serikali inataka wakulima hao wadogo kuacha kulima kwenye mashamba yao ikidai mashamba hayo yapo kwenye eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

subscribe to our newsletter!

Mbarali, Mbeya. Jumla ya wakulima wadogo 852 kutoka Mbarali, Mbeya wamefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, ikiwa ni sehemu ya jitihada zao za kuuzuia mpango wa Serikali wa kuwaondoa katika ardhi yao.  

Ezekia Kimanga na wenzake 851 katika kesi hiyo wanawashtaki Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (mshtakiwa wa kwanza) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (mshtakiwa wa pili). 

Wawasilishaji wa maombi hayo ni wanakijiji wanaoishi na kujishugulisha na shughuli za kilimo ndani ya vijiji 23 vilivyopo wilayani Mbarali ambavyo ni Mahango, Mkunywa, Ikeha, Nyangadete, Magigiwe, Vikaye, Igunda, IvalanjiIkanutwa, Nyeregete, Mwanavala, Ibumila, Songwe, Warumba, Ukwavila, Kapunga, Iyala, Luhanga, Madundasi, Msanga, Simike, Kilambo na Udindilwa.

Hatua hiyo inafuatia kupitwa kwa wakati kwa notisi ya siku 90 iliyotolewa na wawasilisha maombi kwa Serikali wakiitarifu kuhusu nia yao ya kutaka Mahakama iingilie kati suala la tishio la kuondolewa katika ardhi yao.

Jebra Kambole ni wakili anayewawakilisha wanavijiji hao katika kesi yao hiyo ambaye ameiambia The Chanzo kwamba hatua ya kuishtaki Serikali imetokana na juhudi za kulitatua suala hilo nje ya Mahakama zimeshindwa kuzaa matunda. 

“Ombi hili ni la dharura sana kwani Serikali imewazuia wakulima kulima ardhi yao ambayo tayari imeshaandaliwa kwa ajili ya kilimo,” Kambole alibainisha wakati wa mahojiano. 

“Wakulima walikuwa wamepanga kwamba kufikia katikati ya Februari 2023 wamekuwa wamepanda mbegu na kama watashindwa kufanya hivyo katika msimu huu wa mvua, watakabiliwa na njaa na umaskini katika miezi ijayo,” aliongeza Kambole. 

“Pia, zoezi la uondoshwaji linakusudiwa kutekelezwa katika kipindi ambacho wanakijiji hawajatengewa maeneo yoyote mbadala na Serikali,” Kambole aliiambia The Chanzo. “Kitendo hiki kinawafanya raia hawa wa Tanzania kuwa wakimbizi kwenye nchi yao.” 

Alipoulizwa kama anafahamu chochote kuhusiana na mpango huo wa wananchi kuishitaki Serikali, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angelina Mabula aliiambia The Chanzo: “Sifahamu chochote.” 

Mvutano wa muda mrefu

Mvutano kati ya wakulima wadogo na mamlaka za Serikali huko Mbarali umekuwepo kwa muda mrefu sasa, hususan kati ya vijiji 23 vya wilaya hiyo na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo imekuwa ikidai kwamba vijiji hivyo vipo ndani ya ardhi yake.

Mnamo Februari 15, 2020, wizara nane zinazohusika na uhifadhi zilitembelea Mbarali kama sehemu ya juhudi za Serikali kutafuta suluhu ya mzozo huo uliodumu kwa miaka takriban 10 lakini hakuna suluhu iliyopatikana. 

SOMA ZAIDI: Apigania Haki Yake ya Ardhi Kwa Miaka 36 Bila Mafanikio

Serikali inasema vijiji hivyo vipo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa mujibu wa GN Na. 28 ya mwaka 2008. Hata hivyo, imeshindwa kufanyia kazi ushauri wa Rais wa awamu ya tano hayati John Magufuli aliyeshauri vijiji hivyo virasimishwe badala ya kuharibiwa.

Mnamo Januari 19, 2019, Magufuli, aliyefariki Machi 17, 2021, aliagiza kusitishwa mara moja kwa zoezi la Serikali kuharibu vijiji vinavyodaiwa kuwa katika maeneo ya hifadhi, vilivyokadiriwa kuwa karibu 366 nchini kote, na kutaka “busara” zitumike katika zoezi la kuweka mipaka. 

Lakini wakulima hao wadogo wa Mbarali walipata habari za kushtusha hapo Oktoba 25, 2022, kufuatia tangazo la Serikali kwamba vijiji vitano na vitongoji 47 kutoka vijiji 14 vinatakiwa viondolewe ili kuruhusu upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. 

Akitoa tangazo hilo, Dk Mabula alivitaja vijiji vitakavyoathirika kwa asilimia 100 na zoezi hilo kuwa ni Luhanga, Madundasi, Msanga, Iyala na Kalambo vyenye wakazi 21,252, akisema wananchi hawapaswi kuwa katika maeneo hayo na usajili wa vijiji hivyo unapaswa kubatilishwa.

Mnamo Januari 17, 2023, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea Mbarali ambapo alitangaza kuwa vijiji 34 kati ya 39 vilivyotangazwa kuwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha vitaepushwa kuondolewa, huku wakazi wa vijiji vitano vilivyobaki wataondolewa kwenye hifadhi baada ya kulipwa fidia ya ardhi yao. 

SOMA ZAIDI: Wadau wa Ardhi Waitaka Serikali Kuheshimu Maamuzi ya Mahakama

“Timu ya mawaziri kutoka wizara nane ambazo zimekuwa zikishughulikia suala hili imefanya kazi kubwa iliyopelekea marekebisho ya mipaka ya hifadhi, ambayo ilielezwa katika GN. Vijiji hivyo vitano lazima viondolewe kwa sababu vipo katika maeneo nyeti,” gazeti la Serikali la Daily News lilimnukuu Majaliwa akisema. 

Majaliwa alisema pia Serikali imeridhia maombi ya wakazi wa vijiji hivyo vitano waliopangwa kuhamishwa kuendelea kutunza mazao yao hadi yatakapovunwa kwa mujibu wa taarifa ya Daily News

Lakini kulingana na ripoti ambazo The Chanzo imezipata kutoka kwa wakulima hao wadogo wa huko Mbarali, vumbi bado halijatulia kutokana na mvutano uliopo kati yao na mamlaka za Serikali. 

Kati ya Januari 1 na Januari 2, 2023, mwandishi wa habari hii alitembelea Mnazi, moja kati ya vijiji vilivyopo wilayani Mbarali ambavyo watu wake wameamuriwa kuondoka na kusikia kero za wananchi zinazotakana na agizo hilo la Serikali. 

Hawana uhakika 

Watu wengi hapa wanaonekana kutokuwa na uhakika na mustakabali wa maisha yao na wapo makini sana linapokuja suala la kuongea na waandishi wa habari kwani wanahofia kwamba kufanya hivyo kunaweza kuwaweka kwenye mgongano na Serikali na kufanya maisha yao kuwa magumu. 

Huku akiwa hajui nini cha kufanya ili hali hiyo iwe nzuri, Paulinus Msigwa anashangaa inakuwaje Serikali iamuru yeye na wakulima wenzake kuondoka katika ardhi ambayo ana hati miliki yake. 

SOMA ZAIDI: Namna Ukosefu wa Ardhi ya Kutumia Unavyogeuka Kuwa Janga Kilosa

“Sisi siyo wakimbizi hapa,” Msigwa, 38, aliiambia The Chanzo wakati wa mahojiano. “Tumekuwa tukiishi hapa maisha yetu yote, kuishi na kulima ardhi yetu. Kijiji chetu kinatambulika kisheria. Ardhi tunayolima pia ina hati miliki za kimila zinazotolewa na Serikali.”

Wakati ikiwa Mbarali, The Chanzo ilipata hati miliki za kimila zilizotolewa kwa wanavijiji wengi wa Mnazi, baadhi zikianzia mwaka 1999. 

Wakulima hao wadogo wameweza hata kuanzisha chama chao cha ushirika, Nguvukazi Mwanavala AMCOS Limited ambacho kilisajiliwa kisheria na mamlaka za Serikali za mitaa. 

Abdulkarim Abasi ni mkazi wa Mnazi ambaye ni mkulima mdogo mwenye umri wa miaka 60 aliiambia The Chanzo kwamba “huhisi uchungu” anapofikiri jinsi atakavyoitunza familia yake kwa kuwa sasa wameamriwa kuondoka katika sehemu pekee ambayo amewahi kuijua katika maisha yake. 

“Nimepoteza kama Shilingi milioni 4.8 kwa kukodisha shamba na kununua mahitaji mengine muhimu ya kilimo hivi tunapozungumza,” Abasi akiwa amevaa kanzu huku akitembea kwa kutegemea fimbo yake anaiambia The Chanzo. “Siwezi tena kulima shamba. Nitarudishaje pesa zangu?”

Wanakijiji wanalalamika kuhusu kwenda kwenye mashamba yao kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha kukamatwa na kufanyiwa aina nyingine za unyanyasaji zisizojulikana kutoka kwa wenye mamlaka, wakichangua kukaa ndani ya nyumba zao na kungoja “miujiza itendeke,” kama mwanakijiji mmoja alivyosema. 

Mnamo Januari 19, 2023, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera aliagiza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) “kumshughulikia ipasavyo” mtu yeyote atakayepatikana Mnazi na maeneo mengine ambayo watu wameamriwa kuondoka. 

Ombi la dharura 

Hatua ya kuishitaki Serikali inafuata baada ya mikakati ya awali iliyochukuliwa na wakulima wadogo hao kujikwamua na usumbufu huo kuchukua muda mrefu kutoa matokeo yaliyotarajiwa. 

Hiyo ni pamoja na ile iliyohusisha kukishirikisha Chama cha Mapinduzi (CCM), chama tawala, na kukiomba kuingilia kati ambapo Paulinus Msigwa aliongoza ujumbe wa watu wanne kwenda kumuona Naibu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara) Abdulrahman Kinana hapo Disemba 2022.

SOMA ZAIDI: Ufafanuzi Mdogo wa Kile Kinachoendelea Ngorongoro

Jebra Kambole, wakili anayewawakilisha wananchi hao, alisema kesi hiyo itatajwa Februari 15, 2023, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Mbeya. 

Kambole alisema kesi hiyo ina umuhimu wa hali ya juu kwani ardhi yenye mgogoro ni ya wawasilisha maombi na familia zao, wakiwemo watoto wanaosoma shule katika eneo moja na hatua hiyo ya Serikali itawaathiri wananchi na familia zao. 

“Ndani ya ardhi yenye mgogoro, kuna ofisi za Serikali ya kijiji, makanisa, shule, maeneo ya mazishi, na maeneo ya kiutamaduni,” alibainisha wakili huyo wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Haya yote yataathiriwa kama hatua ya Serikali au mamlaka zake zitaendelea.”

“Baadhi ya wawasilisha maombi walichukua mikopo kutoka benki na kuweka hati miliki za ardhi zao kama dhamana, na wanatarajia kulipa mkopo huo kupitia kulima na kilimo,” aliongeza Kambole. “Hilo halitafanyika kama watu wataondolewa katika ardhi hiyo.”

Asifiwe Mbembela ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mbeya anayepatikana kupitia barua pepe mbembelaasifiwe@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Inahuzunisha sana, mamlaka zinajali kutanua hifadhi za wanyamapori kuliko maisha ya watu. Mimi ni mzaliwa wa Mbarali inaniuma sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *