The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mahakama Yaipiga ‘Stop’ Serikali Kuhamisha Wanavijiji Mbarali

Ni kwenye zoezi la Serikali kuwahamisha wanavijiji vya Ukwavila na Iyala kupisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, imetoa uamuzi wa kufuta na kutengua amri na maelekezo ya Serikali ya kuwafukuza wananchi wilayani Mbarali, mkoani Mbeya.

Uamuzi huo uliotolewa Agosti 7, 2023, umekuja baada ya wanavijiji watatu wa vijiji vya Ukwavila na Iyala – Heneri Mwadupa, Charles Mwanyimbwa na Josephat Edson – kufungua shauri la madai mchanganyiko namba 02 la mwaka 2023, dhidi ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Katibu wa Wizara hiyo pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wananchi hao waliiomba Mahakama kuuita kwa ajili ya kuutathmini uamuzi uliotolewa na Waziri wa Ardhi Oktoba 25, 2022, ambapo waziri aliamuru wanakijiji, katika vijiji vya Luhanga, Madundasi, Msanga, Iyala, Kalambo na katika vitongoji vingine 47 ndani ya mkoa wa Mbeya, kuondoka mara moja na vivyo hivyo maeneo hayo kufutiwa usajili, ili kuruhusu upanuzi wa mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Wanavijiji hao walipinga uamuzi huo wa Serikali, wakidai kuwa hawakuwa wamepatiwa taarifa za awali na pia hawakuwa wamepatiwa haki ya kusikilizwa. Pia, walihoji uhalali wa amri hiyo ya kufukuzwa kwao kwani hawakuwa wamelipwa fidia, huku Serikali ikishindwa kueleza ni wapi wataenda na kupelekwa baada ya kuondolewa katika maeneo yao.

Katika uendeshaji wa kesi hiyo, wananchi hao waliwakilishwa na Mawakili wa Kujitegemea, Faraji Mangula na Neema Siwingwa, huku upande wa Serikali ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Joseph Tibaijuka.

SOMA ZAIDI: Wakulima Wadogo 852 Mbarali Waiburuza Serikali Mahakamani Wakitetea Ardhi Yao

Wanavijiji waliieleza Mahakama kuwa wamekuwa wakazi wa maeneo hayo kwa zaidi ya miaka ishirini ambapo walisema kwamba wamepatiwa maeneo hayo na Serikali kwa ajili ya makazi na kilimo.

Wanavijiji pia walieleza kuchanganywa na kauli za Serikali, kwani wakati wa Hayati Rais John Magufuli, Serikali, mnamo Januari 15, 2019, iliamuru kutokufutwa kwa vijiji hivyo na badala yake maelekezo yalitolewa kuwa, kutokana na ongezeko la watu, Serikali inapaswa kuwagawia wananchi maeneo yenye rutuba na kuhifadhi maeneo yenye miti na misitu kwa ajili kuwa sehemu ya hifadhi, kitu ambacho hakikufanyika.

Serikali ilijitetea kwamba mipaka inayoelezwa na wananchi imewekwa kupitia sheria ndogo namba 28 ya mwaka 2008 (G.N No. 28/2008), ikifafanua kwamba sheria ya hifadhi ya kitaifa inakataza na kuzuia shughuli zozote za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi.

Serikali ilikiri kwamba Rais Magufuli alitaka zoezi la uwekaji mipaka litathminiwe upya na busara itumike ili kutokuwaondoa watu katika maeneo ambayo hamna sababu ya kufanya hivyo.

SOMA ZAIDI: Wakulima Mbarali Walalamikia Mashamba Yao Kuuzwa Kinyemela

Hii ilimaanisha ya kwamba mipaka ya eneo la hifadhi inapaswa kuwekwa kwanza na kisha tathmini ndiyo ifanyike ili kubaini ama kuliacha eneo hilo kuwa sehemu ya hifadhi au kuruhusu kuwepo kwa makazi ya watu na shughuli za kibinadamu, Serikali ilieleza.

Serikali ilisisitiza kwamba maeneo hayo ni maeneo oevu na hivyo ni muhimu katika utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji; hivyo kwa misingi hiyo, ni lazima maeneo hayo yalindwe dhidi ya wavamizi, walio ndani ya mipaka, ikiwemo wanavijiji walioleta shauri hilo mahakamani.

Wakili wa Serikali alieleza kuwa watu wilayani humo hawafukuzwi, bali Serikali inaendelea kubaini mipaka kama ilivyoelezwa na sheria ndogo namba 28 ya mwaka 2008, ikiitaka Mahakama kupuuza hoja za waleta maombi kwamba walipatiwa maeneo hayo.

Baada ya kusikiliza hoja za upande zote mbili, Mahakama ilieleza kwamba, ni dhahiri kuwa Serikali ilitoa tamko Oktoba 25, 2022, ikihoji endapo kama tamko hilo, lililoambatana na amri, lilitolewa kwa usahihi na kwa kuzingatia taratibu.

Jaji Lilian Mongella, aliyekuwa akisimamia shauri hilo, alirejea kifungu cha nne cha Sheria ya Ardhi ya Kijiji, ambapo, pamoja na mambo mengine, kinaeleza kwamba, pale ambapo ardhi ya kijiji imepatiwa kwa wanakijiji, wanakijiji hao wanapaswa kupewa taarifa, au notisi, na Halmashauri ya Kijiji, kuhusiana na kusudio la kuhamishwa.

SOMA ZAIDI: Ucheleweshaji Kesi Mahakamani Unavyokwamisha Upatikanaji wa Haki

Dk Mongella aliendelea kueleza kuwa, sheria inahitaji wanakijiji kupatiwa fursa ya kuwasilisha maoni yao kuhusiana na uhamisho huo unaokusudiwa; na vivyo hivyo, kifungu hicho kinaeleza kuwa hamna uhamisho unapaswa kufanyika mpaka zoezi la ulipwaji fidia utakapofanyika.

Jaji Mongella aliendelea kusema kwamba hamna yeyote kati ya waleta maombi ambaye alipatiwa nafasi ya kumhoji waziri wala kuhoji tamko husika la Serikali, akihitimisha kwamba wanavijiji walinyimwa haki yao ya msingi ya kusikilizwa.

Mongella, hata hivyo, alisema ukiukwaji huo umefanyika katika kijiji cha Iyala na si kijiji cha Ukwavila, kwani tamko la Serikali la Oktoba 25, 2022, haujakitaja kijiji cha Ukwavila na badala yake ulikitaja dhahiri kijiji cha Iyala.

Mahakama Kuu ilikubaliana na maombi ya mleta maombi namba tatu – Josephat Edson– na ikafuta na kutupa amri na maelekezo yaliyotolewa na waziri wa ardhi Oktoba 25, 2022, yanayohusiana na kijiji cha Iyala.

Mahakama Kuu imeiamuru Serikali kuzingatia taratibu za kisheria katika kutekeleza mpango wake kwa kutoa fursa kwa Edson kuwasilisha maoni yake kabla ya maamuzi yeyote yale kuchukuliwa dhidi yake.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *