Wakulima Mbarali Walalamikia Mashamba Yao Kuuzwa Kinyemela

Eneo hilo lenye ukubwa wa hekari 28 liliuzwa na mmoja ya wakulima waliokuwa wakilima hapo kwa mtu mmoja ambaye mpaka sasa utambulisho wake haujajulikana hali iliyowaacha watendaji wa Serikali ya kijiji kurushiana lawama.

subscribe to our newsletter!

Mbeya. Wananchi wapatao 14 wa kijiji cha Iyala, kata ya Ruhanga, wilayani Mbarali, mkoani Mbeya wameiomba Serikali ya kijiji kuwarudishia eneo la mashamba lenye ukubwa wa hekari 28 ambazo wanadai kuporwa na mmoja wa wanakijiji hao aliyejulikana kwa jina la Patrick Boniface na kuyauza kwa mtu mwingine ambaye utambulisho wake haujajulikana mpaka sasa.

Wananchi hao wametoa maombi hayo wakati wakizungumza na The Chanzo ambapo wameeleza kuwa wamekuwa wakilalamika kwa muda sasa lakini bado suala lao halijapatiwa majawabu. 

Wameeleza kuwa walibaini kuwa mashamba hayo yamechukuliwa na kuendelezwa na mtu mwingine baada ya kwa nyakati tofauti kufika katika mashamba kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa kilimo ambapo walikuta tayari yameshaandaliwa na walipojaribu kuuliza kwa vibarua ambao walikuwa wanalima matuta katika mashamba hayo, wakaelezwa kuwa Patrick Boniface ameuza mashamba hayo kwa bosi wa vibarua hao, ambaye hata hivyo hakutajwa jina.

Mmoja ya wahanga wa kunyang`anywa shamba aliyefahamika kwa jina la Tumaini Mgode ameelezea kuwa wamekuwa wakiyamiliki mashamba hayo kwa muda wa zaidi ya miaka sita, tangu kipindi ambacho Serikali ya kijiji kupitia halmashauri ya kijiji hicho ilipoamua kugawa maeneo.

“Yaani tunaiomba Serikali, tunaomba itusaidie sisi tunanyang’anywa mashamba wakati 2016 tuligawiwa hadi leo tunalima tunashangaa leo hii mtu anaenda kuuza kwa tajiri,” amelalamika Mgode. “Sisi watu masikini twende wapi, tutapeleka wapi familia zetu?

Kwa mujibu wa Mgode, wakulima hao wamekuwa wakizungushwa kila mara wanapotafuta ufumbuzi wa malalamiko yao bila kupata majibu stahiki huku muda wa kuandaa mashamba yao kwa ajili ya kilimo ukiwa unaishia.

Iginas Sakumoyo Daniel, mkulima mwengine aliyepoteza shamba lake, ameieleza The Chanzo kuwa licha ya kuwa na viambata ambavyo vinaonyesha umiliki wa mashamba hayo, bado yamechukuliwa.

“Ndiyo sisi tulipewa mashamba na kamati mwaka 2016 na [viambata vya umiliki tunavyo na tumelima kwa miaka sita lakini tumeshangaa tunaenda kusafisha shamba tunakuta limepigwa matuta,” anasema. 

Akizungumza na The Chanzo kuhusiana na malalamiko hayo, Mwenyekiti mstaafu Williard Sabumoyo Mkatasa ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti mwaka 2016 wakati wanagawa maeneo hayo kwa wananchi, amesema kutokana na uhaba wa maeneo ya kilimo uliokuwepo kipindi hicho na idadi ya watu, hasa vijana kuongezeka katika kijiji cha Iyala, Halmashauri ya Kijiji ilikaa na kupitisha ajenda ya kuwagawia wananchi eneo la kilimo ambapo kila kichwa kilikuwa kinapatiwa hekari mbili.

“Najua mwaka 2016 tulikaa na halmashauri [ya kijiji] na kujadili eneo ambalo lilikuwa la wafugaji kulipunguza baada ya vijana kuomba mashamba maana hawakuwa na maeneo ya kulima,” anasema Mkatasa. “Sisi kama halmashauri tulikaa na kujadili na kusema lile eneo la wafugaji tulipunguze baada ya kuwa eneo la wafugaji pekee lingine liwe eneo la wakulima, na tulifanya hivyo na tulipojadili kwenye halmashauri tulienda kwenye mkutano mkuu [wa kijiji] na mkutano ukapitisha lile eneo liwe eneo la wakulima.”

Inadaiwa kwamba Patrick Boniface kabla ya kuuza mashamba hayo alikuwa anadai kuwa ni mashamba yao ya familia, kitu ambacho wakulima wanakipinga. The Chanzo ilishindwa kumpata Boniface kujibu shutuma zinazoelekezwa dhidi yake. Kijana huyo amekuwa haonekani tena kijijini hapo tangu alipotekeleza mpango wa kuuza eneo hilo.

Hata hivyo, mdogo wake anayejulikana kwa jina la Kurwa Boniface Yawanga anakana kuwa mashamba yaliyouzwa na kaka yake ni sehemu ya mashamba yao.

“Siyo kweli [kama mashamba yaliyouzwa ni sehemu ya familia yetu],” Yawanga aliiambia The Chanzo. “Amenyang’anya tu shamba la watu la kwake aliuza muda mrefu.”

Alipotafutwa kuelezea mgogoro unaoendelea kwenye kijiji chake, Mtendaji wa Kijiji cha Iyala Nyelu Mmasai alisema kwamba hawezi kuzungumzia mgogoro huo kwa sababu yuko nje ya kituo cha kazi kwa kazi maalum.

Akijibu swali la The Chanzo kama anafahamu mgogoro huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Reuben Mfune alisema malalamiko na mgogoro wa wakazi wa kijiji cha Iyala haujafika mezani kwake.

Asifiwe Mbembela ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mbeya; unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mbembelaasifiwe@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts