The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Uchunguzi wa Polisi Wabaini Tukio la Msichana Aliyebakwa na Kulawitiwa Lilifanyika Dodoma, Wanne Mbaroni

Jeshi la Polisi limeeleza pia limefanikiwa kumpata msichana aliyefanyiwa ukatili na amehifadhiwa eneo salama na anaendelea kupata huduma zinazostahili kupewa mtu aliyefanyiwa ukatili wa aina hiyo

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Jeshi la Polisi nchini limesema kuwa uchunguzi wao umebaini kuwa video iliyosambaa mitandaoni ikionesha mwanamke mmoja akibakwa na kulawitiwa na kikundi cha wanaume lilifanyika jijini Dodoma.

Katika taarifa iliyotolewa leo na Msemaji wa Jeshi la Polisi, SACP David Misime imesema, tukio hilo limefanyika mwezi Mei mwaka 2024 katika eneo la Swaswa jijini hapa.

“Hadi sasa uchunguzi umefanikiwa kukamata watuhumiwa wanne kati ya sita ambao walipanga kutekeleza tukio hilo,” amesema Misime.

Tayari Polisi imewakamata wanaume wanne kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti mwanamke huyo.

 “ Watuhumiwa hao wamekamatwa mkoani Dodoma na mkoa wa Pwani,” amsema Misime,  “ambao ni Clinton Honest Damas maarufu kama Nyundo, Praygod Edwin Mushi, Amini Lord Lema na Nickson Idala Jackson.”

Tangu Agosti 2, 2024 ilisambaa video mtandaoni ikimuonesha mwanamke mmoja akibakwa na kulawitiwa na wanaume watano, ambapo katika moja ya video ikionesha wanaume hao wakimtaka mwanamke huyo kuomba msamaha kwa afande wao kwa kitendo chake cha kutembea na mume wake.

Kufuatia kusambaa kwa video hizo wananchi na wadau mbalimbali wa haki za binadamu walipaza sauti kutaka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wanaume hao ambao walidaiwa kuwa ni askari wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Hata hivyo, katika hatua za awali pamoja na Jeshi la Polisi kutoa taarifa ya kuchunguza tukio hilo, pia iliwataka watu waache kusambaza video hizo mitandaoni kwa ajili ya kulinda utu na heshima ya mwathirika wa tukio. 

Katika taarifa ya Polisi pia imeeleza imefanikiwa kukamata watuhumiwa wanne huko jijini Dar es salaam ambao walikiuka sheria kwa kusambaza picha mjongeo wa tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii.

“Watuhumiwa hao ni Flora Mlombora, Agatha Mchome, Madatha Jeremiah Budodi na James Nyanda Paulo,” ameeleza Misime.

Sambamba na hilo, taarifa imesema watuhumiwa wanne wamekamatwa kwa kutuhuma za kutengeneza na kusambaza taarifa za uongo mitandaoni zinazosema binti aliyebakwa amekutwa amefariki. Watuhumiwa hao ni  ni Amos Lwiza, Adam Dongo, Venance Mallya na Asack Elias kutoka mikoa ya Arusha na Dar es Salaam.

“Uchunguzi unaendelea kukamilishwa sambaba na kuwasaka watuhumiwa wawili ambao bado wamejificha ili wafikishwe Mahakamani.”

Jeshi la Polisi limeeleza pia limefanikiwa kumpata msichana aliyefanyiwa ukatili na amehifadhiwa eneo salama na anaendelea kupata huduma zinazostahili kupewa mtu aliyefanyiwa ukatili wa aina hiyo.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *