Ijumaa iliyopita, Rais wa Sudan Kusini aliwaandalia chakula wanamichezo walioshiriki Michezo ya Olimpiki iliyomalizika jijini Paris kwa ajili ya kuwapongeza kwa kushiriki mashindano hayo kwa mafanikio, licha ya kutotwaa medali yoyote.
Sudan Kusini, taifa jipya barani Afrika na ulimwenguni, iliwakilishwa na wanamichezo 14, riadha wawili wa mbio fupi na 12 wa timu ya wanaume ya mpira wa kikapu. Mwanariadha wa mbio za mita 100 kwa wanawake alishindwa kumaliza baada ya kupata jeraha mara baada ya kuchomoka sehemu ya kuanzia na baadaye kuanguka, wakati yule wa mbio za mita 400 hakuweza kuvuka raundi za awali.
Timu ya taifa ya mpira wa kikapu ndiyo iliyotingisha michezo hiyo mikubwa duniani. Ilishiriki kwa mara ya kwanza na ikafanikiwa kupata ushindi mmoja dhidi ya Puerto Rico na kupoteza mechi nyingine dhidi ya Marekani na Serbia. Iliustua ulimwengu wakati ilipoipa wakati mgumu Marekani, maarufu kwa jina la Dream Team, katika mechi ya kirafiki kabla ya Olimpiki kuanza michezo hiyo jijini Paris.
Haikuweza kuvuka hatua ya makundi, lakini ilikuwa imetuma salamu duniani kuwa kuna mwamba amejitambua na anakuja kwa nguvu katika mpira wa kikapu.
Pamoja na kutofika hatua za juu katika riadha na kikapu, bado Rais wa Sudan Kusini aliona kuna kitu cha kukaa nao ili kuwapongeza na kuwapa moyo. Pia, katika chakula hicho alitangaza kuwa atatenga eneo kwa ajili ya kujenga kijiji cha michezo.
SOMA ZAIDI: Kulihitaji Utafiti Ligi Kuu Kutumia Uwanja wa Amaan
Unaweza kushangaa kwamba taifa dogo na jipya kama Sudan Kusini limeweza kuambulia ushindi wa kwanza wa Olimpiki kwenye mpira wa kikapu, huku ikituma wanariadha wake katika mbio za mita 100 na 400, ambazo kwa kawaida hutawaliwa na nchi kama Marekani, Jamaica, Uingereza na Canada.
Huwezi kushangaa
Lakini ukiijua Sudan Kusini huwezi kushangaa. Mungu amewajalia wananchi wa huko miili mikubwa na urefu ambao ni talanta muhimu katika mpira wa kikapu na mbio fupi. Kwa maana nyingine, Sudan Kusini wamejitambua kuwa nguvu yao kubwa iko wapi na wameitumia ipasavyo.
Nchini Botswana, rais alitangaza Ijumaa iliyopita kuwa ya mapumziko kitaifa baada ya mwanariadha wake, Letsile Tebogo, kuwa Mwafrika wa kwanza kutwaa medali ya dhahabu katika mbio za mita 200, akiwa mbele ya Wamarekani wawili, Kenny Bednarek, aliyetwaa medali ya shaba na Noah Lyles, aliyekuwa wa tatu.
Kwa ujumla, Afrika haijawahi kutwaa medali ya dhahabu katika mbio fupi (mita 100, mita 200 na mita 400 kupokezana vijiti.
Pamoja na udogo wake, Botswana ilipeleka wanamichezo 11: wanariadha tisa na waogeleaji wawili. Tebogo amepita mafanikio ya mwanariadha wa Namibia, Frankie Fredericks ambaye alitwaa medali nne za shaba katika Olimpiki ya 1992 na 1996, Mary Onyali (mita 200 1996), huku Mnigeria mwingine Glory Alozie akitwaa shaba katika mbio za mita 100 jijini Sydney.
SOMA ZAIDI: Hongera TFF kwa Tuzo, Lakini Bado Maboresho Yanahitajika
Kwa kawaida, ushindi wowote kwenye Olimpiki ni shangwe kwa taifa na ndio maana Rais wa Botswana hakuchelewa kuitangaza Ijumaa iliyopita kuwa siku ya mapumziko kwa wananchi wote.
Mikono mitupu
Kwetu, wanamichezo saba wanarejea mikono mitupu baada ya miaka minne ya kujiandaa na kutafuta nafasi ya kufuzu. Idadi ya wanamichezo wanaoenda kuiwakilisha nchi inazidi kupungua kadri siku zinavyokwenda, huku msisimko wa Olimpiki ukizidi kupungua. Inapewa nafasi ndogo na vyombo vya habari, huku vijiweni kukiwa hakuna mazungumzo ya Olimpiki labda kutokee jambo kubwa.
Si riadha, ambayo huko nyuma tuliwahi kufanya vizuri duniani, si soka, si mpira wa kikapu, si mpira wa wavu, si ngumi ambayo pia tulikuwa wazuri, na wala si michezo mingine ya ndani ambayo tunaweza hata kukaribia kufuzu kucheza Olimpiki.
Tumebakia kwenye mbio za marathoni tu, ambako inaonekana ni jitihada binafsi na vipaji walivyo navyo watu wa kutoka mikoa ya kaskazini na kati kutokana na mazingira ya mikoa yao. Tanzania ina kila hali ya hewa inayoweza kuzalisha wanamichezo wazuri wa michezo tofauti na kuwa taifa tishio, si tu Afrika bali duniani kwa ujumla.
SOMA ZAIDI: Kutumia Takwimu Pekee Tuzo za TFF ni Usumbufu
Lakini ni kama michezo mingine inapotea huku mchezo wa mpira wa miguu ukiendelea kupata umaarufu kwa kasi. Hakuna anayezungumzia netiboli, ambao ni mchezo wa kwanza kwa msichana wa Tanzania; wala si ngumi ambao unarejeshwa kwa nguvu na wadhamini ambao hawaangalii ngumi za ridhaa ambazo ndizo zilizokuwa zinazalisha mabondia wazuri, bali ngumi za kulipwa; wala si mpira wa wavu na mikono, iliyokuwa ikichezwa sana kwenye majeshi; na wala si mpira wa meza uliokuwa ukichezwa sana shule za sekondari; na wala si mpira wa kikapu.
Sisi wa zamani tuliishuhudia michezo hiyo kwa karibu wakati Serikali ikishiriki kuikuza na kuiendeleza. Karibu kila mchezo ulikuwa na mtendaji aliyekuwa ameajiriwa na Serikali, huku wizarani kukiwa na dawati la kila mchezo.
Pia, mashirika na taasisi za Serikali zilishiriki kwa kiwango kikubwa kukuza michezo, zikiwa na timu za michezo tofauti na wachezaji kuwa waajiriwa wa hizo taasisi au mashirika.
Lakini tulipolegeza masharti ya kiuchumi, mashirika na taasisi za Serikali zikaanza kubana matumizi na eneo la kwanza likawa michezo kwa kuwa wanamichezo hawakuwa wanazalisha bali kutumia kinachozalishwa na wengine. Kwa hiyo, watia hasara wakaondolewa.
Usingeweza kuilaumu Serikali kwa kulegeza masharti ya kiuchumi kwa sababu dunia ndio ilichukua mkondo huo, lakini hatukuwa na mtazamo mpana wa nini kifanyike kwa sekta ambazo zingeathirika na mageuzi hayo ya kiuchumi, na hasa michezo.
SOMA ZAIDI: Bodi ya Ligi Kuu Iongoze Uboreshaji Kanuni za Ligi
Ndio, mpira wa miguu unavutia mamilioni ya Watanzania na hivyo ni rahisi kwa mashirika na kampuni binafsi kuingiza fedha zao kwa ajili ya kutangaza huduma na bidhaa zao.
Mvuto huo unaweza kuwepo katika netiboli kama zitakuwepo jitihada za makusudi za kuukuza kwa kuwa ndio mchezo maarufu kwa wanawake, lakini haukuwa na nguvu ya kuusukuma kupita katika mageuzi ya kiuchumi. Uliyumbishwa na mageuzi hayo na haujaweza kusimama sawasawa.
Labda kuna uhai kidogo katika mpira wa kikapu ambao kutokana na kufuatiliwa na vijana wengi, angalau taasisi zinawekeza fedha na televisheni zinaona thamani kununua haki za matangazo. Pia, marathoni zimekuwa zikipata msukumo kutoka kampuni kwa kuwa kibiashara zinalipa.
Si hivyo kwa mpira wa mikono, wavu, meza, kuogelea, michezo ya ndani ya riadha na mingine mingi.
Tutafakari
Wakati tukiwakaribisha nyumbani wanariadha wetu waliokuwa Paris, Ufaransa kushiriki – si kushindana—Olimpiki, ni muhimu kutafakari jinsi ya kunyanyua michezo mingine na kuipa mvuto utakaowezesha kusimama imara kiuchumi ili mwaka 2028 tutakapokuwa tunatuma timu Olimpiki, tuwe na wigo mpana zaidi wa kushindana na hivyo nafasi ya kushinda.
SOMA ZAIDI: Yusuf Manji Alimuachia Somo Zuri Mohammed Dewji
Na kikubwa zaidi ni kwa jinsi gani Serikali inaweza ikabeba jukumu hili la kusaidia michezo mingine kusimama imara. Tunaweza kuwa na mfumo wetu tofauti na ya nchi nyingine kama kweli tunataka kuinua sekta hii yenye uwezo mkubwa wa kuajiri vijana bnila ya kuwa na elimu kubwa ya darasani?
Hawa vijana wenye uwezo wa kutembea kilomita hadi 20 kwa siku wakiuza lesso, karanga, kalamu, vibanio vya nguo au mafuta ya kupaka mwilini, hawawezi kuchukuliwa na michezo kama kurushe tufe, kisahani, kuruka juu au mbio fupi, maana wengine ni wa miraba minne?
Kama Serikali haiwezi kutoa fedha za kusaidia vyama vya michezo, au klabu za michezo, kutokana na majukumu yake makubwa, inawezaje ku kutengeneza mazingira kwa kampuni na taasisi zitakazowekeza fedha michezoni?
Kunaweza kuwa na unafuu wowote na unaoratibiwa kwa makini wa nafuu ya kodi kwa kampuni zitakazodhamini michezo hii inayopotea na kuiwezesha kuajiri? Kama hizo kodi ndizo zinazotakiwa zisaidie huduma za kijamii, kwa nini zisichukuliwe moja kwa moja na michezo kwa njia hiyo?
Haya ni mawazo yangu tu, lakini ni muhimu kuanza kufikiria ni kwa vipi Serikali inaweza kutengeneza mazingira ya kuwezesha michezo kuwa sehemu ajira imara na hivyo kusaidia kuongeza ufanisi katika ushiriki wetu wa mashindano makubwa ili siku moja tuwe na mapumziko kwa kuwa tumeshinda.
Ni vizuri kuboronga katika michezo ya Paris kukatupa fikra mpya na mtazamo mpya kwa michezo, kwamba ikikuzwa, kuwekewa mazingira mazuri na kuendelezwa inaweza kufikia malengo ya kimichezo na yale ya kiuchumi badala ya kuiona kuwa ni burudani pekee.
Kama Wizara ya Utamaduni inaweza kuanzisha mfuko kwa ajili ya kukopesha wasanii, nini kifanyike kwa wanamichezo, hasa hii ambayo kwa sasa haina kipato chochote wala vyama vyao havipati ruzuku kutoka mashirikisho yao ya kimataifa?
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.