The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kulihitaji Utafiti Ligi Kuu Kutumia Uwanja wa Amaan

Ni muhimu sana kushirikisha umma katika mambo muhimu kabla ya kukimbilia kuyaamua na kuyatangaza.

subscribe to our newsletter!

Wiki tunayoimaliza, Bodi ya Ligi Kuu ya Bara (TPLB) ilitangaza marekebisho na maboresho ya kanuni za uendeshaji wa mashindano hayo, ikipanua wigo wa maeneo ya kuchezea, kuongeza ada za wachezaji wa kigeni na mambo mengine.

Ni uamuzi ambao umekuja siku chache kabla ya msimu mpya kuanza na tayari Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka (TFF) imeshabariki, huku jamii ikiona kila kitu kuwa ni kipya.

Jamii haikupata muda wa kujadili marekebisho hayo na ndiyo maana nimesema ni jambo jipya kwao. Hata kama jamii haihusiki moja kwa moja na masuala ya uwanjani na nje ya uwanja kulinganisha na timu, bado TPLB ilikuwa na wajibu wa kuushirikisha umma, ambao umejaa watu wa fani tofauti, katika jambo hilo.

Niliandika hapo awali kuwa mabadiliko, au maboresho, ya kanuni hayafanywi na watu wanaojifungia chumbani pekee, au TFF na timu za Ligi Kuu, Championship na Ligi Daraja la kwanza, bali na umma wote kwa ujumla.

Ndiyo maana leo hii tunaweza kuzungumzia jambo ambalo linaenda kufanyiwa marekebisho na Ligi Kuu ya England kwa kuwa linakuwa limeshawekwa hadharani kwa ajili ya umma kulijadili. 

SOMA ZAIDI: Hongera TFF kwa Tuzo, Lakini Bado Maboresho Yanahitajika

Na umma unajumuisha wachezaji wa zamani, makocha, waamuzi, viongozi wa zamani, wasomi wa elimu ya viungo katika vyuo vikuu, wachumi, wanasheria, watu wa masoko, wataalamu wa utamaduni na wenye fani nyingine nyingi zinazoendana na michezo au masuala yanayoshirikisha watu wengi.

Dharau

Kitendo cha kutangaza mabadiliko bila ya kushirikisha umma ni kuudharau kuwa hauna mchango wowote katika maendeleo ya soka, kitu ambacho si sahihi.

Hata leo tunapojadili kilichotangazwa, tunafanya hivyo kama wajibu kwa taifa letu lakini hatutarajii watu waliotupuuza wakaona hoja na kufikiria kuzuia mabadiliko au maboresho hayo kwanza ili utafiti na utafutaji maoni ufanyike kwanza.

Tumetangaziwa kuwa Uwanja wa Amaan wa Zanzibar sasa unaweza kutumiwa na timu za Bara kwa mechi za Ligi Kuu. Sijui walizingatia nini katika kufanya uamuzi huo. Lakini hapo wanasheria wangeweza kutoa maoni yao kisheria kuhusu masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano na hilo linaweza kutafsiriwa vipi.

Ndiyo, kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), visiwa hivyo vimepewa upendeleo wa pekee wa kuwa mwanachama na ndiyo maana klabu zake zinashiriki mashindano ya Afrika.

SOMA ZAIDI: Kutumia Takwimu Pekee Tuzo za TFF ni Usumbufu

Kwa hiyo, uamuzi huo unaibua mkanganyiko na unaweza kurudisha mjadala usioisha wa Zanzibar ni nchi au si nchi, kitu ambacho si busara kuibuliwa kila mara.

Gharama

Kwangu naona uamuzi huo unaweka mwanya wa kuongeza gharama kwa timu zetu. Kama Simba, Yanga, KMC au hata Coastal Union itaamua kuutumia uwanja huo kwa mechi na Kagera Sugar, Pamba au Prisons?

Utamaanisha gharama zaidi ya zile ambazo ingeingia kwa mechi kuchezwa Uwanja wa Mkapa, KMC Mwenge au Azam Complex. Fedha inayopatikana kutoka haki za matangazo na udhamini italazimika kutumika kwenye gharama za safari kuliko timu kufanya mipango ya maendeleo.

Bado klabu zinashindwa kugharimia timu zao za vijana kwa ajili ya kucheza msimu mzima kama timu za kwanza. Bado klabu zinashindwa kuwa na shule za soka za watoto. Bado ni ngumu kwa hizi klabu kumudu gharama za kulea timu za wanawake.

Juu yake tunaweka mwanya wa kuongeza gharama za safari. Sidhani kama ni busara. Ni rahisi kwa Simba na Yanga kuamua kwenda Amaan, lakini ni ngumu kwa timu nyingine kuzifuata. Hiyo haiihitaji akili kubwa.

SOMA ZAIDI: Bodi ya Ligi Kuu Iongoze Uboreshaji Kanuni za Ligi

Zaidi ya yote, fedha ambazo timu hizo zingepata kutokana na viinbgilio vya mlangoni angalau kugharimia safari, ni ndogo kulingana na uchumi wa Zanzibar. Kiingilio cha juu cha mechi ya Azam na Coastal Union kilikuwa Sh5,000 na bado uwanja haujai.

Na kwa sababu timu zinazoweza kuhamishia mechi zake Amaan ni Simba, Yanga au KMC za Dar es salaam, maana yake tunazidi kuzitangaza timu hizo mbili huku tukidumaza mapenzi ya mashabiki kwa klabu nyingine. 

Simba na Yanga zikijiimarisha zaidi Zanzibar, kuna uwezekano ule ushabiki kwa timu kama KMKM, Mlandege na zile za majeshi ukapungua na mashabiki wakawa hawajitokezi kwa wingi kuangalia timu za asili ya huko, wakisubiri mechi kubwa.

Tumefikiria nini?

Kibiashara sijui TPLB ilifikiria nini? Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) lilifikia makubaliano na kampuni ya Relevant Sports ya Marekani kufanyia marekebisho sheria zake zinazozuia mechi rasmi za mashindano za nchi moja kufanyikia nchi nyingine.

FIFA ilifikia uamuzi huo kama kutafuta amani baada ya Relevant Sports kufungua kesi dhidi ya Shirikisho la Soka la Marekani (USSF) kuamua kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa kuzuiwa kuandaa mechi za ligi ya Hispania nchini Marekani.

SOMA ZAIDI: Yusuf Manji Alimuachia Somo Zuri Mohammed Dewji

FIFA imeunda jopo la wataalamu wake kukusanya maoni na kufanyia utafiti suala hilo kabla ya kuliwasilisha kwenye mkutano mkuu kwa ajili ya kulipitisha.

Katika suala hilo, utashi wa kibiashara wa Relevant Sports ndiyo unaotaka kulazimisha mechi za ligi kuchezewa nje ya nchi. Uamuzi wa TPLB umechochewa na nini? Na umeangalia maslahi mapana ya taifa? 

Kwamba kuchezea mechi za Ligi Kuu ya Bara visiwani Zanzibar kutapoozesha na pengine kuua soka la ushindani katika visiwa hivyo? Ndiyo maana nasema ni muhimu sana kushirikisha umma katika mambo muhimu kabla ya kukimbilia kuyaamua na kuyatangaza. 

Kanuni ni kitu muhimu na ndiyo maana tangu Februari, FIFA bado inaangalia uwezekano wa kuruhusu mechi za ligi kuchezwa nje na wakati huo wote jopo lake linaangalia ni namna gani uamuzi huo unaweza kuwa na manufaa kwa mchezo wa mpira wa miguu kote duniani.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Uchambuzi mzuri sana,
    Ni kweli kabisa usiopingika hakunaga mabadiliko ya kanuni ama Sheria yanayopitishwa bila kushirikisha wadau wa sekta husika
    Kwa hili TFF wametukosea

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *