The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Vijana Wenzangu, Tusiruhusu Kisingizio Chochote Kituzuie Kushiriki Kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Mkuu

Wanasiasa hupenda kujiita watumishi wa wananchi, uchaguzi ni fursa adhimu ya kuwathibitishia kwamba hilo ni kweli na siyo maskhara.

subscribe to our newsletter!

Kuna namna ambayo sisi wananchi tunasahau nguvu tuliyonayo kutokana na vikwazo vinavyoendelea kuwepo kwenye jamii, na hii inatuondoa kwenye malengo yetu makuu ambayo tunapaswa kuyatimiza kutokana na mamlaka tuliyonayo. 

Kuelekea chaguzi kuu mbili ambazo zipo hapa mbele yetu – chaguzi za Serikali za Mitaa na chaguzi ya Serikali Kuu – na kama wananchi ‘tunaosadikika’ kuwa waamuzi wa mwisho kwenye mustakabali huu wa kuleta maendeleo na mabadiliko kwenye jamii zetu kupitia kura zetu, kuna haja kubwa ya kutumia nguvu na mamlaka tuliyonayo ya kufanya maamuzi ya kuamua hatma za maisha yetu.

Ni kipindi kifupi sana ambacho, kwa mara nyingine, tunakutana na wale wanaotuongoza ili kutupatia mrejesho wa wapi wamefikia na jinsi gani wanaweza kutupeleka mbele zaidi. Katika kipindi hiki, wananchi mara nyingi tunapotoshwa na sera nyingi na ahadi ambazo utekelezaji wake ni mgumu hata kufikirika, na ambazo siyo jawabu la matatizo yaliyopo kwenye jamii zetu. 

Hatuhitaji kukumbushwa kile kinachokosekana kwenye jamii zetu; badala yake, inatupasa tupaze sauti na kuzungumzia kwa mapana namna gani tunahitaji mabadiliko zaidi. 

Tusiwe wepesi wa kusahau masuala ambayo hayapo sawa kwenye jamii zetu na kupotoshwa na kauli lainishi za muda mfupi, hali inayopelekea kulalamika mara baada ya kipindi hiki muhimu kupita na kujikuta hatujabadili chochote, tukiwa bado mahala pale pale au hata kurudishwa nyuma zaidi. Sasa ni wakati wa kufanya mabadiliko, siyo baadaye, ambayo hatujui itakuwa lini, wapi, na pengine itatukuta tukiwa katika hali gani.

SOMA ZAIDI: Je, Uchaguzi Serikali za Mitaa 2024 Utaongeza Wanawake Wenyeviti wa Vijiji?

‘Wananchi ndiyo waajiri wetu, na hivyo inatupasa kuwatumikia vyema.’ Hii kauli kwa sasa ndiyo wakati wake sahihi katika utekelezaji na udhihirishaji, na pia kuwakumbusha wale waliopo madarakani kuhusu mpango mkakati wa msingi wa kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwenye jamii zetu.

Changamoto

Changamoto katika mchakato wa kuleta mabadiliko kwenye jamii zetu hazikosekani; zipo, tena ni nyingi. Tukizitazama kwa mapana, changamoto hizi ni kikwazo kikubwa sana kwa wananchi kushiriki kwenye chaguzi muhimu katika jamii zao. 

Suala kama ugumu wa maisha, hasa ukosefu wa kipato kinachojitosheleza, ni moja ya changamoto kubwa inayochangia wananchi kukubali kurubuniwa, au kubadilisha maamuzi yao, ili kutimiza haja zao za muda mfupi pasipo kuzingatia matokeo ya muda mrefu. 

Maslahi haya ya muda mfupi yameendelea kuathiri na kuangamiza jamii zetu kwa kiwango kikubwa sana. Na kama jamii, tunahitaji muamko wa kuweka mbele vipaumbele vyetu ili kubadilisha hali ya maisha yetu na kuleta maendeleo bora. Huu ni wito wetu wa pamoja, ili tuweze kutokomeza changamoto zinazotukabili na kufanikisha mabadiliko yenye tija.

Pia, kumekuwepo na tungo nyingi tata zikiwa zinatamkwa hadharani, zenye lengo la kukatisha tamaa baadhi ya wananchi katika ushiriki wao kwenye zoezi la upigaji kura, kama vile zinazoashiria uwepo wa wizi wa kura kwenye michakato hiyo. Kauli hizi hazipaswi kutukatisha tamaa, bali kutuzidisha ari ya kusiriki kwenye michakato hiyo ili hata kama kunakuwepo na wizi wa kura, basi iwe ni ngumu kufanya hivyo.

SOMA ZAIDI: Wadau Waingiwa Hofu Kuelekea Uchaguzi 2024, 2025

Kundi kubwa la wananchi bado linaonekana halina uelewa mpana na wa mashiko kuhusu elimu ya mpiga kura, ikiwemo umuhimu wa kushiriki kwenye masuala mazima ya kijamii na kuweza kujiletea mabadiliko na badala yake kuaminika kuwa ni zoezi la watu fulani ambao wapo ngazi fulani na ambao ndiyo wanaaminika kufanya hayo mabadiliko kwa mbadala wao. 

Asasi thibitishwa na kutambulika kutoa elimu hii zinatosheleza matakwa ya jamii? Wana rasilimali za kutosha za kuweza kuhakikisha kwamba elimu hii inawanufaisha Watanzania wengi wa kule chini ili kuweza kuitumia haki yao vizuri? Kwa maana hizi ni chachu kubwa katika utoaji msaada serikalini katika usambazaji wa elimu hii muhimu.

Changamoto na vikwazo tunavyokumbana navyo kama wananchi kuhusu upigaji kura na ushiriki katika maendeleo ya jamii vinahusiana kwa karibu na suala la muda. Ni vipi tunaweza kutumia muda tulionao kwa njia bora ili kufanikisha mabadiliko endelevu kwa manufaa yetu na kwa vizazi vijavyo? 

Kwa kuhitimisha, nitoe wito kwetu sote kwamba tunapopata nafasi ya kuzungumza, ni wajibu wetu sisi wananchi kuupazia sauti kubwa wajibu wetu tulionao wa kuamua hatma ya maisha yetu na yale ya taifa letu. Hata baada ya muda kupita, tunahitaji kuangalia nyuma kwa fahari na kujivunia kwamba tulifanya maamuzi sahihi kwa mustakabali wa taifa letu kwa ujumla.

Kelvin Expellah ni mshauri wa masuala ya utetezi na uchechemuzi kutoka Twaweza East Africa. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia consultantke@twaweza.org. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts