The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wadau Waingiwa Hofu Kuelekea Uchaguzi 2024, 2025

Sababu ni ufinyu wa mapendekezo ya wadau yaliyoanishwa kwenye sheria za uchaguzi, CCM yasema mabadiliko hayajafika kikomo.

subscribe to our newsletter!

Mwanza. Wadau mbalimbali wa masuala ya kisiasa hapa nchini wameoneshwa kutoridhishwa na mabadiliko yaliyofanyika kwenye sheria za uchaguzi, kwa kile walichodai kuwa bado hazitoi mwanga kamili wa kuwa na chaguzi huru na za haki. 

Sheria hizo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba moja ya mwaka 2024, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi namba mbili ya mwaka 2024, Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa namba tatu ya  mwaka 2024 na Sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali namba nne ya mwaka 2024.

Madai hayo yametokana na kile kilichoelezwa kuwa Serikali imetupilia mbali baadhi ya mambo ambayo wadau hao waliyapendekeza yawepo kwenye sheria hizo, lakini pia kitendo cha maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kushikiliwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee pasipo kuwashirikisha wadau wengine. 

Haya yote yamebainishwa jana Mei 8, 2024, wakati wa mkutano wa kitaifa wa kutafakari na kujenga uelewa wa pamoja juu ya sheria za uchaguzi zilizopitishwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu wa hapo mwakani. 

Mkutano huo wa siku mbili ambao umeendelea pia leo hii umeandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ukiwakutanishwa wadau mbalimbali kutoka kwenye vyama vya siasa, asasi za kiraia, mabalozi pamoja na waandishi wa habari. 

Baadhi ya mambo ambayo wadau hao wameyataja kuwa yametupiliwa mbali ni pamoja na pendekezo la kufanyika kwa marekebisho madogo kwenye katiba ya mwaka 1997, kuruhusiwa kwa mgombea binafsi, matokeo ya Urais kupingwa mahakamani pamoja na viongozi wa umma wanaoteuliwa na Rais kutokuwa sehemu ya tume ya uchaguzi.

Wadau wanakosoa uchaguzi Serikali za mitaa kuendelea kusimamiwa na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), licha ya Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iliyopitishwa kueleza kuwa kuwa tume hiy ndiyo ambayo itakuwa na wajibu kusimamia uchaguzi. 

“Serikali haikuona umuhimu wa kufanya mabadiliko madogo [ya katiba] kwa hivi sasa,” anasema Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa TCD. “Ilipeleka miswada mitatu bungeni ambayo baada ya mijadala na marekebisho ilipitishwa na kuwa sheria.”

“Sheria ambayo imepitishwa inasema kwamba jukumu la Tume Huru ya Uchaguzi ni kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa, sasa hili likoje kwamba sheria tayari imepitishiwa lakini uchaguzi wa Serikali za Mitaa utasimamiwa na TAMISEMI? Labda pana maelezo ya namna gani katika kipindi hiki cha mpito?” Alihoji Profesa Lipumba.

Anna Henga ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu na Demokrasia (LHRC). Akitoa mada kwenye mjadala huo ameeleza kwamba kwa mujibu wa uchambuzi wao walioufanya sheria za uchaguzi zilizopitishwa zimebeba asilimia 30 tu ya walichukuwa wakikitaka. 

“Kwa hiyo kama [sheria za uchaguzi] zingeweza kuleta mabadiliko ya 15 ya katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kubadilisha kidogo na kubadilisha baadhi ya vitu kwenye Katiba tungeweza kupata matokeo makubwa zaidi.”

“Sisi kule ofisini kwetu tulikuwa tunasema hapa tumepata kama asilimia 30 tu ya tulichokuwa tunakitaka asilimia 70 bado. Kwa hiyo kama tungeweza kutaka kufikia hiyo [asilimia] 70 angalau tungeweza kuibadilisha katiba ingeweza kutusaidia sana.”

Madai haya ya Henga yametokana na kile alichoeleza kuwa Serikali haijapeleka bungeni muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kitu ambacho walikuwa wamekipendekeza lakini pia Serikali haijatekeleza baadhi ya maamuzi ya mahakama kwenye kesi mbalimbali za kimkakati. 

Baadhi ya maamuzi hayo ni pamoja na wafungwa kupiga kura, kuwepo kwa mgombea binafsi na kutokutumia wakurugenzi wa halmashauri kwenye uchaguzi. 

Mifumo haiakisi

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, yeye ameeleza kuwa mabadiliko kwenye sheria hizo yaliyofanyika kwenye sheria za uchaguzi hayaakisi mifumo ya uchaguzi iliyopo kutokana na madai yake ya kuwa kila kitu bado kipo chini ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. 

Mbowe anadai kuwa ikiwa imesalia miezi minne hivi sasa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, bado wao kama vyama vya upinzani hawajui kanuni zitakazotumika kwenye uchaguzi huo, kwani licha ya kuwa wao ni washiriki lakini wamekuwa hawashirikishwi kwenye hatua zozote.

“Tunakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa miezi minne ijayo hatujui kanuni, sisi ni washiriki, wanaojua ni Serikali na CCM, wanahodhi kila hatua,” anasema Mbowe. 

“Sasa tukija kuangalia haya mabadiliko yanayotolewa hapa ni mapambo tu, hayajaweza kutibu majeraha yaliyokuwepo. Na Rais anatoka na kauli nzuri nzuri, kwamba tutakuwa na tume huru, tutakuwa na chaguzi huru ni vizuri, hata Magufuli alisema hivyo.” 

“Mheshimiwa [Abdulrahman] Kinana naye amesema tutakuwa na uchaguzi huru viongozi wengi wa Chama Cha Mapinduzi wanasema tutakuwa na chaguzi huru. Tunashukuru kwa hayo matamko ya matumaini lakini je, kweli mifumo yetu ina akisi hivyo? 

 Hatujafika kikomo

Akijibu malalamiko haya ya wadau ambao moja kwa moja walielekeza shutuma zao kwa Serikali inayoongozwa na CCM kada wa chama hicho Profesa Palamagamba Kabudi ameeleza kuwa wao walisikiliza maoni ya wadau na mabadiliko yataendelea kufanyika kwani bado hayajafika kikomo. 

Kabudi ameyataja baadhi ya mambo ambayo yalipendekezwa na yakaainishwa kwenye sheria hizo kuwa ni pamoja na suala la wagombea kupita bila kupingwa pamoja na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kufanyiwa usaili. 

“Mawazo yote yaliyotolewa ni mawazo mazuri kwa sababu unapotaka kufanya maboresho ni lazima uwe tayari kusikiliza,” anasema Kabudi ambaye pia ni Mbunge wa Kilosa. 

“Na kwa Chama cha Mapinduzi kimeamua kwa kuyakubali mengi yaliyokuja kutoka kwa wadau. Na yale ambayo yalionekana kabisa kwamba mwaka 2020 na 2019 yameleta shida hapakuwa na tashishwi katika kuyakubali.”

“Kwa hiyo kwa ujumla Chama cha Mapinduzi mabadiliko mengi yaliyofanyika [ni] mabadiliko ambayo hajafika ukomo na ni vizuri kabisa kama nilivyosema huo ni mchakato, ni mwendo, ni safari unamwagilia maji ili mmea ukue. Kwa hiyo yapo mengi yamefanyiwa kazi lakini hatua iliyochukuliwa ni hatua sahihi na mwendo sahihi.”

Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *