Mbeya. Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imefutilia mbali shauri namba 41 la mwaka 2023 la wakazi wa Isela kijiji Cha Ndolezi mkoani Songwe dhidi ya serikali na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutaka kupisha hifadhi ya Kimondo.
Hayo yamebainishwa Ijumaa, Agosti 23, 2024, jijini Mbeya chini ya Jaji mkuu Mussa Pomo wakati akisikiliza shauri hilo amesema upande wa wadai hauelezi ukubwa wa eneo linalobishaniwa lakini pia kesi hiyo imefunguliwa na mtu zaidi ya mmoja na kila mtu anamiliki eneo lake ambapo haijaainishwa kwenye hati iliyopo mahakamani hapo kuwa kila mtu anamiliki eneo la ukubwa gani na namba ngapi.
Itakumbukwa kuwa mwaka 2022 wakazi hawa wapatao 120 walitakiwa kuhama katika maeneo yao ili kupisha hifadhi ya Kimondo chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, hali iliyopelekea wakazi hawa kufungua shauri katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.
Kwa upande wake wakili Philip Mwakilima ambaye hakuwepo mahakamani hapo akizungumza kwa njia ya simu amesema atakutana na mawakili wenzake upande wa wadai na wananchi ambao wamefungua shauri hilo ili kufahamu hatua zitakazochukuliwa zaidi ikiwemo kukata rufaa.