The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mtazamo Kwamba Tunaweza Kutumia Ngono Kuwaadhibu Watu Waliotukosea ni Jini Tuliloliumba Wenyewe na Ambalo Limeendelea Kututafuna

Kama jamii tunapaswa kufikiri juu ya namna tunaandaa watoto wetu, hasa wakiume, kuelewa na kuwa na mahusiano chanya na ngono, na wanaamini katika usawa wa kijinsia.

subscribe to our newsletter!

Hivi karibuni, vichwa vya habari vilitawaliwa na habari ya ‘Binti wa Yombo’ anayedaiwa kufanyiwa ukatili wa kingono na vijana wa nne, kwa kile kinachoaminika kuwa ni kisasi cha kuibwa kwa mume kilichofanywa na “afande” aliyewatuma vijana hao kutekeleza uhalifu huo.

Tukio hili limegusa hisia za watu wengi sana kwenye jamii, kila mmoja akitaka hatua stahiki zichukuliwe ili kuhakikisha haki ya binti inapatikana, na wahusika wote wanafikishwa mbele ya sheria, ikiwemo wale vijana, afande aliyewatuma, na wengine kwenda mbali zaidi kutaka mume anaedaiwa kuchepuka naye kuwajibishwa.

Binafsi, ninafarijika sana kuona jamii ikipaza sauti juu ya jambo hili. Inatia moyo kuona nguvu ya umma ikitumika kuhakikisha si tu haki inatendeka, bali pia matukio haya yanakomeshwa. Hata hivyo, bado nina wasiwasi kwamba hatujatoa muda wa kutosha kuzungumzia suluhu ya muda mrefu ya masuala ya ukatili wa kingono unaofanywa na vijana wa kiume kwenye jamii yetu.

Mimi nimezaliwa na kulelewa katika familia ya kidini. Wazazi wangu walihakikisha kwamba makuzi yangu, kwa kiasi kikubwa, yanafuata imani na mafunzo ya dini ya kikristo. Sina kumbukumbu halisi za lini, na ni kwa namna gani nilijifunza ngono ni nini, inafanywaje na ina maana gani. 

Ninachojua ni kwamba niliyokuwa nikiyaona na kuyasikia yalikuwa yanaleta maana kadri siku zilivyokuwa zikienda. Kanisani nilijifunza amri kumi za Mungu, mojawapo ikiwa ni usizini au usifanye uasherati. Ingawa haikuwa na maelezo ya kutosha mwanzoni, baadae nilielewa maana yake. 

Nyumbani hakukuwahi kuwa na maongezi ya aina yoyote kuhusu ngono. Ninafikiri kwamba wazazi wangu waliamini sisi ni watoto hivyo hatuwezi kuelewa ngono, hivyo hakukuwa na haja ya kuizungumzia. Hata hivyo, nilikua nikiskia wakiliongelea kama tendo la ndoa. 

Nilikua na bahati kwamba mama yangu alikua ni nesi aliyefanya kazi kwenye kliniki ya mama na mtoto kama mkunga. Na kwa sababu tulikua tunakaa karibu na hospitali, kuna mengi kuhusu afya ya uzazi nilijifunza nikiwa mdogo sana kwa kumsikiliza mama akiwa anaongelea kuhusu kazi yake na watu wengine, mimi nikiwepo, asijue ninaelewa kila kitu.

SOMA ZAIDI: Je, Watanzania Tuko Huru Kuongelea Ngono Kwa Uwazi?

Shuleni, hali ilikua tofauti kidogo. Kulikua na kitu kinaitwa “mchezo mbaya.” Ilikua ni kawaida sana kusikia fulani na fulani wamekamatwa wakifanya mchezo mbaya. Ukiwa na bahati, mtoto aliyekuzidi umri anaweza kukueleza nini maana ya mchezo mbaya, la sivyo ilibakia kuwa msemo mgeni kwa wengine. 

Nilipofika darasa la sita, mwaka 2001, mmoja wa rafiki zangu wa karibu aliniambia kuna mwanafunzi mwenzetu darasani ana picha za watu wanafanya “matusi.” Ilikua ni kitu cha siri sana kama magendo, lakini kila mtu alikuwa anatamani kuona. 

Nakumbuka siku moja wakati wa mapumziko tulienda kwenye uwanja wa mpira na yule mwanafunzi, akatoa kurasa iliyochanwa kwenye jarida la ngono aliloiba kutoka kwa kaka yake mkubwa nyumbani, akatuonesha. Ilikua ni mara yangu ya kwanza kuangalia picha ya ngono. Mwaka huohuo ndipo tulianza kujifunza ukuaji, au balehe, na mifumo ya uzazi katika somo la sayansi. 

Mwalimu wangu alikua mcheshi, binafsi nilikua ninafurahia sana somo lake, pengine kwa sababu baadhi ya masuala ya kisayansi aliyokuwa akifundisha, kama vile namna mimba inapatikana, inakua na mtoto kuzaliwa, nilikua tayari nina uelewa kidogo kutoka kwa mama yangu na kazi zake.

Mifumo rasmi

Haya yote ni kusema kwamba, wakati ninakuwa, hakukuwa na mfumo rasmi ambao ungeweza kunisaidia kuelewa ngono ni nini, inafanywaje, na ina maana gani kwenye maisha yangu kama binadamu. Kazi hiyo kwa kiasi kikubwa ilifanywa na watoto wenzangu walionizidi umri ambao nilikua ninakutana nao shuleni, mtaani au kwenye mikusanyiko ya kifamilia – niwaite wote tu kaka zangu. 

Kaka zangu walinifundisha namna ngono inafanywa; walinifundisha sababu za kufanya ngono, ikiwemo kuthibitisha uanaume wangu; na muhimu zaidi walinifundisha “mbinu” za kupata ngono kutoka kwa wasichana. Kaka zangu hao walinicheka pale nilipoonesha kushindwa kupata ngono, na walinifurahia na kunisheherekea pale nilipofanikiwa, bila kujali nimetumia mbinu gani. 

Japo hii ilikua kinyume na imani yangu ya dini, sikuwa na uwezo wa kuepukana na ushawishi huo. Ningeweza vipi wakati hata mwili wangu wenyewe ulikuwa unanidai ngono?

SOMA ZAIDI: Utajuaje Kama Mwanao Anafanyiwa Ukatili wa Kingono?

Kadri umri ulivyokuwa ukisogea, kuelekea u-teenager, matarajio ya kuwa na mbinu bora na idadi kubwa ya wasichana uliofanya nao ngono yalikuwa yakiongezeka. Nilijihisi mnyonge mara kadhaa rafiki zangu walipokuwa wakisimulia hadithi za wasichana wengi waliofanya nao ngono na aina ya vitendo walivyowafanyia, kwetu wote ilikua ni kitu cha kujivunia. 

Hadithi za wadada wa kazi majumbani, mabinamu, watoto wa jirani vichakani, kulala na wasichana tunaokutana nao kisimani kuchota maji, na hata wasichana “kupigwa mtungo” zilikua ni za kawaida sana. Hakuna kati yetu aliyewahi kufikiri, au hata kuzungumza, ni namna gani hawa wasichana wanajiskia juu ya hilo. 

Kitu pekee tulichokuwa tunaongea ni kwamba, hata wao ndivyo wanavyopenda na ndivyo wanavyotaka. Ukweli ni kwamba, hadi nafika kidato cha sita au chuoni miaka ya mwanzo, niliamini kwamba msichana anaweza kusema hapana akimaanisha ndiyo, na njia pekee ya kuthibitisha hilo ni kulazimisha iingie, kisha ataanza kufurahia.

Ngono

Ngono ni kitu kikubwa sana kwenye maisha ya binadamu. Nafasi ya ngono kwa binadamu siitofautishi sana na vitu kama chakula, malazi, mavazi, usalama, na kadhalika. Hii ni kwa sababu sisi kama binadamu hatuwezi kuendelea kuwepo bila kufanya ngono na kuzaliana. 

Hata hivyo, jamii zetu zimetengeneza mila, desturi na tamaduni ambazo zimefanya ngono – na athari zake zote chanya na hasi –kuwa mwiko kuzungumzwa kwa upana wake. Ni kweli kwamba mifumo hii imetokana na haja ya kujenga jamii yenye ustaarabu na yenye kuwa na familia imara, zenye kulinda watoto ambao ni kizazi kijacho. 

Lakini kama ilivyo kwa mila, desturi na tamaduni zingine potofu zilizowekwa kwa nia njema, ongezeko la maarifa kwenye jamii husukuma mabadiliko ya fikra na kutoa fursa ya kubadili mila, desturi na tamaduni hizo kadri inavyofaa. 

Ngono ni tendo la starehe na la uzazi linalofanywa na watu kwa sababu kadha wa kadha na ni imani yangu kwamba kila mtu anatamani jamii ambayo ngono inakuwa ni kitendo chanya, kinachofanywa kwa malengo chanya, yenye afya na pengine tija. Hata hivyo, mara nyingi sana ngono imekuwa ikifanywa, au kutumika, kwa namna ambayo husababisha athari kubwa kwa wahusika na jamii nzima.

SOMA ZAIDI: Aliyehukumiwa Kifungo cha Maisha Jela kwa Kosa la Ulawiti Aachiwa Huru, Mahakama Yatoa Ufafanuzi

Vijana waliofanya ule ukatili wa kingono hawakufika hapo walipofika kwa bahati mbaya. Kuna njia waliyopita kwenye maisha yao ambayo iliyowafikisha kwenye kile chumba, siku ile, muda ule, wakifanya ukatili ule. 

Njia hiyo, pamoja na mengine mengi, ilihusisha kujengwa kwa uelewa kwamba ngono inaweza pia kutumika kama silaha dhidi ya mwanamke pale inapobidi. Mtazamo huu, ambao upo kati ya vijana, na hata wazee, wengi katika jamii yetu ni jini tulilolilea wenyewe, na sasa linatutafuna. Kwa mtazamo wangu, tunawafelisha vijana wetu sisi wenyewe.

Maswali

Swali la kujiuliza ni je, ni nani alitakiwa awepo mara ya kwanza vijana wale walikuwa wakijifunza kuhusu ngono? Ni nani alipaswa kujibu baadhi ya maswali waliyokuwa nayo? Ni nani alipaswa kuhakikisha kwamba fikra za kutumia ngono kama silaha hazipati nafasi ya kuwa sehemu ya uelewa wao kuhusu ngono? 

Ni nani alipaswa kuhakikisha kwamba vijana hawa wanaelewa mahusiano na tofauti za kijinsia kati yao na wenzao wa kike, na kwamba jamii yetu ina mifumo dume ambayo ni kandamizi kwa watoto wa kike, na hivyo wanapaswa kuwa bora zaidi ya wengine? Ni nani alipaswa kuhakikisha vijana hawa wana uwezo wa kukataa vishawishi vyovyote vya kujihusisha na vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya wanawake? 

Jibu rahisi la maswali yote haya ni wazazi, walezi, walimu na viongozi wa dini. Lakini swali linaloibuka tena ni je, wazazi, walezi, walimu na viongozi wa dini wana uelewa, maarifa, utayari, na nyenzo zinazohitajika kwa wao kutekeleza hayo majukumu yao? 

Kama wewe ni mzazi, ulishawahi kufikiria kwamba una jukumu la muhimu la kuhakikisha mtoto wako anapata muongozo sahihi kuhusu ngono? Walimu, viongozi wa dini na yeyote ambaye watoto wanapita mikononi mwake, ni kwa namna gani kama jamii tumewatayarisha kuwa daraja sahihi kwa watoto wetu katika safari yao kutoka utotoni kuja ukubwani, hususani uhusiano wao na ngono?

Kuna ushahidi wa kutosha kwamba elimu kamilifu na sahihi ya afya ya uzazi husaidia watoto na vijana kuchelewa kujihusisha na masuala ya ngono, lakini pia kujiepusha na matokeo hasi ya ngono kama vile mimba zisizotarajiwa na maradhi. 

SOMA ZAIDI: Mambo Muhimu Wazazi Tunapaswa Kuwafundisha Vijana Wetu

Kuna ushahidi mwingi pia kwamba utoaji wa elimu hiyo unaozingatia si tu mabaya, bali pia mazuri yatokanayo na ngono – kama vile starehe, mapenzi, familia na afya – si tu husaidia uwasilishwaji wa mada kwa vijana wadogo, lakini pia huboresha uelewa wa uhusiano ambao mtu anakua nao na ngono kwenye maisha yake. 

Lakini pia kuna ushahidi wa kutosha kwamba elimu ya usawa wa kijinsia ni njia sahihi ya kupunguza, kama siyo kumaliza, ukatili wa kijinsia na kingono.

Inawezekana uchambuzi huu ukakuacha na maswali mengi zaidi ya majibu, hilo ni moja ya lengo la andiko hili. Kama jamii tunapaswa kufikiri juu ya namna tunaandaa watoto wetu, hasa wakiume, kuelewa na kuwa na mahusiano chanya na ngono, na wanaamini katika usawa wa kijinsia. 

Hii ndiyo namna pekee tunayoweza kuhakikisha kwamba baada ya miaka 20, 30 au 50 ijayo tutakua na jamii ambayo haitokuwa na vichwa vya habari kama ya ‘Binti wa Yombo’ kwa sababu wanajamii wote, au walio wengi, watakuwa na heshima kwa wanawake, na hakutokuwa na mtazamo kwamba ngono inaweza tumika kama silaha, pale inapobidi. 

Ili tuweze kufika huko, tunapaswa kuanza kuhoji mila, desturi na tamaduni zinazochochea usiri usio na tija juu ya masuala ya ngono, kujenga mifumo madhubuti ya utoaji elimu, huduma na msaada kwa watoto na vijana wetu.
Otuck William ni mwanamuziki wa kizazi kipya na mtetezi wa haki za kijamii, hususan kwenye eneo la afya ya uzazi na ujinsia. Kwa maoni, anapatikana kupitia otuckwilliam@gmail.com au X kama @Otuck_William. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. William nimelipenda sana chapisho lako. Nashauli ungetengeneza kitabu cha kujumuisha maoni na maono haya ili yakafundishwe mashuleni hasa msingi na sekondari ikiwa ni sehemu ya mtahala.
    All the best William 👍

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *