Search
Close this search box.

Je, Watanzania Tuko Huru Kuongelea Ngono Kwa Uwazi?

Faida za kuwa huru kuongelea ngono ni nyingi kuliko hasara.

subscribe to our newsletter!

Kwa siku kadhaa sasa, wimbo wa Pita Huku wa msanii wa Singeli Dulla Makabila umekua ukisumbua kwenye mitandao ya kijamii na hata kwenye vyombo mbalimbali vya habari, kama vile runinga na redio.

Hata hivyo, umaarufu wa wimbo huo uliongezeka mara dufu pale zilipoibuka taarifa za mwimbaji wake kuitwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kwa kile kinachoonekana ni kwa lengo la kuhojiana naye kuhusiana na maudhui ya rekodi hiyo.

SOMA ZAIDI: BASATA na Kupatwa kwa Sanaa na Wasanii Tanzania

Hatujui, kwa hakika, yote yaaliyojadiliwa kwenye kikao hicho lakini tuseme kwamba kililenga kuhakikisha kwamba jamii inaelewa kwamba lengo la kazi hiyo ya sanaa ilikua ni kuelimisha jamii na si kuchochea maadili yasiyo mema.

Mimi kama msanii na mwanaharakati, niseme tu ninamuheshimu Dulla kama mwanamuziki, mtunzi, msanii, na muhamisishaji.

Ninatamani kwamba wasanii tungekua na uhuru zaidi wa kuelezea na kuchambua mambo yetu ya kijamii kwa namna ambayo sanaa inaruhusu.

Kuikumbusha jamii

Kwa ambao hawajasikiliza huu wimbo, Dulla anajaribu kuikumbusha jamii kuhusu baadhi ya changamoto zinazotukabili kwa kutumia mfumo wa kidini ambao wengi katika jamii yetu wanauelewa.

Yaani, siku ukifa utahukumiwa kulingana na matendo yako duniani, na hivyo kwenda peponi au motoni.

Hiyo ndiyo dhana nzima ya Pita Huku. Kwa kutumia dhana hii, Dulla anaigiza kama mtoa hukumu kwa watu ambao wanakufa duniani, hivyo anaamua wapi unatakiwa kwenda kulingana na matendo yako duniani.

Hukumu za watu kwenye wimbo huo ni kama ifuatavyo:

Mhusika wa kwanza ni mwanamke wa makamo, umri kati ya 30 – 45, ambaye ameishi kwenye ndoa. Wakati wa ndoa yake amekua akitoka kimapenzi na vijana wadogo na wakati mwingine hayo yamekua yakijionesha kwenye mitandao yake ya kijamii.

Sababu yake kuu ni kwamba haridhishwi kimapenzi na mume wake ambaye, inasemekana, ana kitambi. Hivyo, hukumu yake ni motoni.

SOMA ZAIDI: Mpango wa Wasanii Kulipwa Mirabaha Umefikia Wapi?

Mhusika wa pili ni mchungaji ambaye kabla hajafa alitumia wadhfa wake kufanya ngono na waumini wa kike, na pia kutumia uchawi kudanganya watu kuhusu imani yake. Hukumu yake ni motoni.

Mhusika wa tatu ni kijana mlevi ambaye hufanya maovu akiwa amelewa lakini alikua mtoaji sadaka mzuri kwa wanaohitaji. Hukumu yake ilikua peponi.

Mhusika wa nne ni DJ. Baada ya kifo DJ anaelekea peponi kwa sababu wakati anafanya kazi yake, alikua akizima muziki wakati wa ibada.

Mhusika wa tano kwa ujumla alionekana ana ‘laana’ kwa sababu chumbani kwake kuna mafuta kila kona. Hukumu yake ya kwenda motoni iliamuriwa kwa sababu ya kupenda “kwa mpalange,” na pia aliitwa shoga.

Hii ni moja ya mifano iliyotolewa na BASATA wakiwa wanawasilisha maongezi yao na Dulla kwa waandishi wa habari.

Mhusika anayefuata tayari alionesha wasiwasi wa “kutoboa” kwenda peponi, kwa mujibu wa mhukumu. Yeye ni daktari ambaye pamoja na ufundi wake wa kutoa mimba ipasavyo, alihukumiwa kwenda motoni.

Hakimu ndiyo cheo ambacho Dulla aliamua kumpa mhusika wa saba. Lakini sifa za mtu anayepata hukumu hii zinafanana na watu wa kada mbalimbali, ikiwemo wanasiasa na wanasheria.

SOMA ZAIDI: Ras Inno: Hatutungi Nyimbo Tukaziimbe Rumande

Huyu anakwenda motoni kwa sababu ya kutotenda haki. Cha kushangaza ni kwamba mtu huyu hakutegemea kwamba anakwenda motoni.

Mhusika wa nane ni msichana ambaye huvaa kama mvulana, na tabia yake ya kufanya ngono na wasichana wenzie, anapelekwa motoni.

Mhusika wa tisa ana makosa mengi: kwanza ni kuuza ngono tena kwa kiwango cha kimataifa; pili ni kufanya wanaume wapoteze familia, mfano kwa kula ada ya watoto wake; tatu ni kuwashawishi kingono shemeji zake kwa kupita na khanga; na kikubwa ni kutumia uchawi kufanikisha hayo yote.

Mhusika wa mwisho ndiye ambaye hukumu yake ya kwenda motoni imechukua muda mrefu kuliko wote kwa sababu ana makosa mengi.

Kosa kubwa ni kuwa mchawi, na ametumia uchawi wake kufukuzisha watu kazi, kusababisha magonjwa, kutenganisha wapenzi, kubadilisha umbile lake, kuua watu na kuwashawishi kwamba siyo yeye aliyeua, kuwa chanzo cha umasikini, na kutumia nguvu za giza kufanikisha ndoto za watu.

Mimi siyo muumini wa imani kwamba kuna mbingu na moto baada ya haya maisha, na kwamba matendo yetu hapa duniani ndiyo yatatumika kuamua tutakapoishia.

Lakini ninaelewa hiyo dhana, na ninaelewa kwa nini jamii inaamini hivyo. Kwa hiyo, sitojadili namna “hukumu” hizi zimetolewa kwa sababu hilo ni suala la kiimani.

Hoja zangu zitajikitika kwenye masuala ya kijamii yaliyoibuliwa kwenye hizi “kesi” na mtazamo wangu juu yake. Lengo ni kuchambua mifumo iliyopo kwenye jamii zetu inayopelekea matukio haya kutokea.

“Kesi” nane kati ya kumi kwenye wimbo huu zinahusiana na masuala ya ngono, uzazi, jinsia na ujinsia. Hiyo peke yake inaonesha kuwa kwa kiasi kikubwa jamii za wanadamu zinaathirika sana na haya masuala.

SOMA ZAIDI: Tutapiga Marufuku Vitu Vingapi Kwa Kuwaletea ‘Ukakasi’ Watu Wengine?

Mara nyingi tunaposikia kuhusu changamoto kwenye masuala ya ngono, uzazi, jinsia na ujinsia tunawaza tu kuhusu magonjwa kama UKIMWI, ukatili wa kijinsia, na mimba za utotoni.

Lakini ni kwa namna gani tunaweza zitambua changamoto zote kama hatuna uelewa wa kutosha kuhusu masuala yenyewe?

Kuongelea masuala ya ngono kwenye jamii yetu bado ni mwiko kwa sababu ngono inachukuliwa na jamii kama tendo la ndoa hivyo kama hujiandai kuingia kwenye ndoa, au huko kwenye ndoa, huna sababu ya kuongelea kuhusu ngono.

Na pia kama watoto, tulikuzwa kuamini kwamba ngono ni tendo baya, linasababisha magonjwa na ni dhambi. Linakua zuri tu pale unapoingia kwenye ndoa.

Kama matokeo ya kutokuwepo uwazi kwenye kuzungumzia ngono, watu wengi tunaingia kwenye mahusiano tukiwa hatujui namna ya kuongea na wenza wetu kuhusu raha au karaha tunazozipata tunapofanya nao ngono.

Wazazi wanashindwa kuongea na watoto wao kuhusu ukuaji, mahusiano na ngono. Vijana wanapata taarifa ambazo siyo sahihi na kujikuta kwenye changamoto.

Kama tungekuwa huru …

Tungekuwa na jamii yenye utamaduni wa kuongea kwa uwazi na upana kuhusu ngono na mapenzi, ikiwemo raha zake, karaha zake, faida zake na changamoto zake kwa kila rika na watu kwa mahitaji yao, tungeongeza uwezekano wa wanawake (na wanaume) kufurahia ngono wakati wa kufanya ngono na wenzi wao.

Kwa sasa, inakisiwa kwamba ni asilimia 50 tu ya wanawake ndiyo “hufika kileleni.” Hivyo, pengine tungepunguza uwezekano wa ndoa nyingi kuingia kwenye matatizo.

Pia, tungekuwa tunaongea zaidi kuhusu sura halisi za ukatili wa kingono. Takwimu na ushahidi wa kutosha unaonesha kwamba ukatili wa kingono hufanywa na watu waliokaribu na ambao wanaaminiwa na muathirika pamoja na familia au jamii husika.

SOMA ZAIDI: Bila Uhuru wa Mwanafasihi, Fasihi Haiwezi Kuwa Chombo cha Ukombozi wa Umma

Watu hao ni kama ndugu wa karibu, viongozi wa kidini na kimila, watu wenye mamlaka, vyeo, pesa nakadhalika.

Tungekuwa na jamii yenye utamaduni wa kuongea kwa uwazi na upana kuhusu ngono na mapenzi pia, tungekua na jamii jumuishi na si tenganishi.

Tungekua na uelewa mzuri kuhusu upatikanaji wa mimba, hivyo kuwa na uwezo wa kuzuia mimba pale ambapo hatuzihitaji, na kuruhusu uhuru wa wanawake juu ya miili yao.

Ninaamini tungekua na uwezo wa kutambua uhusiano wa moja kwa moja kati ya vifo vya mama wajawazito (maternal mortality) na utoaji mimba usiyo salama (unsafe abortion).

Pengine tungepunguza unyanyapaa dhidi ya dhana ya utoaji mimba ili tujadili suluhu zenye kuokoa maisha ya watu.

Tungekuwa na jamii yenye utamaduni wa kuongea kwa uwazi na upana kuhusu ngono na mapenzi tungekua na jamii inayoelewa haki za uzazi na ujinsia, kama haki za binadamu, na hivyo tungekua na wanasheria na mahakimu ambao wangetetea upatikanaji wa haki hizi.

Tungeelewa pia kwamba asilimia kubwa ya vitendo vya ngono vinavyofanyika kwenye jamii zetu ni transactional, yaani natoa kitu ili nipate kitu.

Miamala hii ina sura tofauti, lakini yote ni miamala inayofanyika kwenye ndoa, kwenye mahusiano, kwenye maeneo ya kazi, biashara nakadhalika.

SOMA ZAIDI: Vitali Maembe: Sijawahi Kuogopa Kusema Ukweli

Pengine mtazamo huu ungesaidia kumaliza unyanyapaa dhidi ya wenzetu ambao kwao wao hii ni njia rasmi ya kujiingizia kipato.

Kwa kuhitimisha, tungekuwa na jamii yenye utamaduni wa kuongea kwa uwazi na upana kuhusu ngono na mapenzi, pengine tungeacha kuwalaumu wanawake kwa madhara yanayosababishwa na tamaa za wa wanaume.

Pia, na bila kusahau, pengine tungejua kwamba siyo kila tatizo letu ni matokeo ya uchawi!

Naomba nikomee hapa kwa leo, huku nikitoa kongole kwa Dulla Makabila kwa ngoma yake hiyo kali na nikitahadharisha, kwa kutumia maneno ya gwiji la muziki wa hip-hop Afande Sele, kwamba, niliyoyaeleza hapa Ni Mtazamo Tu Masela, Msijenge Chuki!

Otuck William ni mwanamuziki wa kizazi kipya na mtetezi wa haki za kijamii, hususan kwenye eneo la afya ya uzazi na ujinsia. Kwa maoni, anapatikana kupitia otuckwilliam@gmail.com au Twitter kama @Otuck_William. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *