The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

BASATA na Kupatwa kwa Sanaa na Wasanii Tanzania

Masharti na urasimu wanaowekewa wasanii wa Tanzania na BASATA si tu ni hatari na kizingiti katika biashara, bali ni adui mkubwa wa haki ya ubunifu na uhuru wa kazi.

subscribe to our newsletter!

Sina namna ya kusema zaidi ya kukopa maneno ya Nandy, ya kwamba hakika mkunaji limempata pele – nalo pele linamuwasha haswa. Si mwengine huyo mkunaji, ni msanii. Yaani kwa lugha ya sanaa ya michano tunaweza kusema, kama GWM na Sugu walivyoimba, ‘Yamewakuta… Yamewakuta… Yamewakuta Wasanii Mzee Mwenzangu! Nao wamebaki na machungu.’

Kwa takribani wiki sasa, wasanii wengi wa kizazi kipya wametema nyongo zao baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuamua kuanza rasmi kusimamia mamlaka yake ya ukaguzi wa kazi za sanaa. Uamuzi huu wa BASATA unakuja ikiwa ni sehemu ya usimamizi na utekelezaji wa mabadiliko ya sheria ya mwaka 2019 na utunzi wa sheria ndogo ya mwaka 2017/18.

Mabadiliko hayo ya sheria yanayoipa nguvu, na nidiriki kusema jeuri, BASATA yametokea katika kipindi cha miaka minne au mitatu nyuma; ambapo ni katika kipindi hicho hicho ambapo kumekuwepo na utunzi na mabadiliko ya sheria zenye kuleta ukakasi wa hali ya juu. Hata hivyo, wakati waitwao “wanaharakati wa haki za kibinadamu” wakiwa wanakaza mishipa ya shingo na kuzipinga sheria hizo, wasanii (wengi) wao walikuwa fungate. Pasi na shaka walikuwa wakitii maneno ya wahenga – Pilipili usiyoila, inakuwashia nini?

Hata hivyo, sasa wasanii wameipata pilipili yao na inawawasha haswa. Naam! Si nyingine, ni pilipili ya mamlaka ambayo imewaamsha kutoka kwenye usingizi wa kupuuza misingi ya haki na kuwazindua toka kwenye upofu na “uchawa” kwa Serikali. Sasa sina shaka, hata gwiji wao aliyeona na akaimba ‘akheri akae kimya’ atakuwa ameguswa na hali hii ambayo inaweza kuwa tishio hata kwake pia.

Zama tamu za BASATA

Miaka minne nyuma na kuendelea, BASATA kama chombo kilikuwa hakina makali – yaani hawakuwa na nguvu yenye tija wala mamlaka ya moja kwa moja kwa msanii na kazi zao. Sheria Namba 23 ya mwaka 1984 iliyoiunda BASATA ilitamka ya kwamba, Baraza hilo litakuwa na majukumu ya kufufua na kukuza uzalishaji na maendeleo wa kazi za sanaa kwa lengo la kueneza utamaduni wa Tanzania.

Zaidi, BASATA walikuwa pia na majukumu ya kufanya tafiti; kutoa huduma za kiushauri na misaada ya kitaaluma; kupanga na kuratibu shughuli za watu wanaojihusisha na uzalishaji wa kazi za sanaa; kutoa mafunzo; na kuishauri Serikali katika masuala ya maendeleo ya sanaa, miongoni mwa mambo mengine.

Katika majukumu hayo ya awali, BASATA walisalia kwa kiasi kikubwa kuwa “wadau wa heshima” katika tasnia ya sanaa, kwani hawakuwa na mamlaka madhubuti ya kufanya maamuzi yanayoweza kuwa na tija. Hali hii ilishuhudia wasanii na wadau wengine katika sanaa na jamii kukipuuza chombo hicho. Kwa lugha rahisi, BASATA walikuwa kana kwamba ni mbwa waliokosa meno au nyoka wasio na sumu.

Katika wakati huo, wadau wakuu wa masuala ya sanaa, kwa kiasi kikubwa, walikuwa ni wasanii, hususani wasanii wakubwa, wamiliki wa vyombo vya habari na Serikali – kupitia vyombo vingine tofauti ukiachana na BASATA, kama vile Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Jeshi la Polisi. Wakati huo, BASATA walibaki kukumbukwa katika shughuli za kiitifaki na za kitaifa.

Tamu yageuka shubiri

Baada ya zaidi ya miongo mitatu ya ubwete (udumavu), kwa hisani ya awamu ya tano, BASATA hatimaye ilianza kuota meno. Mabadiliko ya sheria katika kipindi hicho yalikibariki chombo hicho na majukumu madhubuti ya ufuatiliaji na udhibiti wa kazi za sanaa. Kubwa kuliko hata hivyo ni kwamba sheria ikakitunuku chombo hicho na fimbo ya ukaguzi, ambayo imeambatana na utoaji vibali.

Zaidi, BASATA imepewa mamlaka ya uangalizi wa masuala ya utamaduni na maadili. Lakini ni ipi maana ya utamaduni na maadili? Hapo sheria imekaa kimya; jambo ambalo ni hatari zaidi kiutendaji na katika utekelezaji wa sheria husika.

BASATA ikazidi kumea, toka kamchicha sasa chombo hicho kimestawi na kuwa bonge la limbuyu; limbuyu linalowashurutisha wasanii kujisajili katika chombo hicho ilimradi kupata uhalali kisheria. Hivyo, mtu anayefanya au anayejishughulisha na kazi za sanaa (kumaanisha msanii) anapaswa kujisajili na BASATA.

Mambo ya kustaajabisha kwa BASATA ni kwamba, ikiwa kazi za sanaa ni pamoja na ushairi, ambao binafsi huutumia kwa ajili ya kufanya chombeza za nafsi na moyo nikieleza hisia zangu, sasa mimi naye ni msanii sawa na Chibu na sote tutatakiwa kujisajili BASATA; na hili ni la lazima (sio muhimu) ilimradi kuendelea kuandika mashairi yangu ya huba – la sivyo sheria inaweza kuchukua mkondo wake kwangu (mkondo upi? Sijui!)

Janga kuu la ukaguzi

Kuhitajika kujisajili na kulazimishwa uanachama ni kesi, lakini sio kesi kubwa kama ya sheria kutuhitaji kusajili kazi zetu za sanaa katika Baraza hilo la Sanaa. Tuchukulie mfano mdogo tu, yani mimi Kido, ninaloshairi langu kama nilivyoeleza hapo juu, kabla ile sijalichapa na kuliwasilisha kwa manzi (yani mlaji au walaji – ikitegemeana na muda huo) basi ninatakiwa kufika kwanza kwa hawa wakaguzi (BASATA), waitathmini sanaa yangu, kisha wanipe ithibati ya kueleza hisia zangu kwa yule nimpendae (kisheria – mlaji).

Twende na mfano mwengine mmoja, mimi ni mbunifu mitindo (au pengine ni mshonaji tu  – hii nayo ni sehemu ya sanaa), amekuja kwangu mteja na kitenge chake anataka nimbunie mtindo wa kuwarusha roho wadeni wake. Mimi, kama msanii wa ubunifu mitindo, ninawajibika kisheria kubuni, kushona na ile kabla ya kukabidhi nguo (ambayo kwa jicho la sheria ni kazi ya sanaa) ninapaswa kuwasilisha kazi yangu ikapate baraka za wakubwa hawa wa ukaguzi kabla sijampatia mteja wangu – la sivyo sheria itachukua mkondo wake.

Mustakabali wa wasanii na sanaa

Hakika haya si ya Firauni, achilia mbali Musa… haya yastaajabishayo akili, nafsi, mwili, na roho ni ya BASATA tu. Kwani haya matakwa ya kisheria na urasimu huu “wa kishamba” si tu ni hatari na ni kizingiti katika biashara, bali ni adui mkubwa wa haki ya ubunifu na uhuru wa kazi.

Kwa anayejiuliza, ni vipi BASATA na sheria zake zinaathiri haki ya kazi, anapaswa kujiuliza namna gani wafanyao sanaa za papo kwa hapo watakavyo athirika na sheria hii. Ndugu zangu wa WATU BAKI, wanaofanya sanaa ya kuchekesha jukwaani (stand-up comedy) wataenda wapi? Je, sheria hii itatuzalishia kina Young Killa Msodoki wengine, watakaopata nafasi na ‘kuchana’ jukwaani papo kwa hapo? Jibu ni rahisi, hapana! Na hili lina maana kwamba Dulla (Mjukuu wa Ambua) na Blaza Jabir Saleh (miongoni mwa wengine), hawataweza tena kufanya sehemu ya vipindi vyao ambavyo hujikita katika sanaa ya mtindo huru (freestyle).

Itoshe tu kusema kwamba ni mengi sana yanawekwa rehani na sheria hii; hivyo ikiwa mamlaka zinaamua kuzirejea akili zao, japo kidogo, basi hawana budi kwanza, kabla ya yote, kuondokana na ajenda ya ukaguzi na vibali. Kisha baada ya hapo, hawana budi kujiuliza, kwani walaji wenyewe wanasemaje?

Jasper “Kido” Sabuni ni mshairi na muandishi wa masuala ya kijamii aliye mbioni kuchapisha kitabu chake cha mashairi ya mapenzi na hisia za moyo. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni kidojasper@gmail.com au unaweza kumfuatilia katika ukurasa wake wa Instagram kama kido_afrika. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Hatua ya BASATA kutaka wasanii wawasilishe kazi zao kwenye baraza hilo kabla ya kuzitoa kwa walaji wao imezua mjadala mpana na taharuki katika tasnia ya sanaa nchini. Kama wewe ni mdau wa sanaa na unadhani una maoni ungependa kuchapisha, The Chanzo iko tayari kuchapisha maoni hayo. Unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *