The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wakulima wa Mwani Mtwara Walia na Ukosefu wa Soko la Uhakika: ‘Tunafanya Kazi ya Kulima Tu, Hakuna Tunachokipata’  

Wafanyabiashara nao wana kilio hichohicho, huku Serikali ikisema inaelekeza jitihada zake kwenye ujenzi wa viwanda vya uchakataji, ikiamini hiyo ndiyo suluhu ya kudumu ya changamoto tajwa.

subscribe to our newsletter!

Mtwara. Wakulima wa zao la mwani kutoka halmashauri ya wilaya ya Mtwara wamelalakimia kushuka kwa bei ya zao hilo la biashara, wakiitaka Serikali kuichukulia kwa uzito changamoto hiyo inayoathiri maendeleo na ustawi wao kama wananchi.

Kwa mujibu wa utafiti wa The Chanzo, bei ya mwani mnene mkoani hapa imeporomoka kutoka Shilingi 2,500 kwa kilogramu moja, mwaka 2022 na 2023, hadi shilingi 1,000 kwa mwaka 2024. Kwa mwani mwembamba, imeshuka kutoka Shilingi 1,200 kwa kilogramu, mwaka 2022 na 2023, mpaka Shilingi 700 hadi 500, mwaka 2024.

Mbali na kushuka kwa bei, wakulima hao pia wamelalamikia kukosekana kwa soko la zao hilo, hali inayowafanya watembee umbali mrefu kwenda kutafuta wanunuzi, ambapo wakati mwingine hutakiwa kurudi na mzigo nyumbani kwani hukosa kabisa watu waliotayari kununua hata kwa bei hiyo ndogo. 

Mwajuma Mbango (katikati), mwenyekiti wa kikundi cha wanawake wanaolima mwani Mtwara, akionesha mwani mwembamba, aina ambayo wanaizalisha kwa wingi. PICHA I OMARI MIKOMA

Fatuma Nauli ni mmoja wa wanakikundi cha wanawake kinachoitwa Azimio, kikundi chenye wanawake nane ambao wanajishughulisha na kilimo cha mwani katika kijiji cha Msakala, kata ya Ziwani, halmashauri wilaya Mtwara. 

Nauli ameiambia The Chanzo kuwa maslahi madogo wanayoyapata hivi sawa kwenye kilimo cha mwani yanamfanya ashindwe kupata mahitaji ya msingi, ikiwemo kushindwa kuwasomesha watoto wake.  

‘Hakuna tunachopata’

“Ninapitia changamoto sana za kulima, lakini hakuna ninachokipata,” Nauli, 49, anasema. “Mwani tunaupata kwa wingi, lakini hatuna wateja wa kuwauzia, tukapata maslahi. Tunafanya kazi ya kulima tu, hakuna tunachokipata.” 

“Yaani [mwani] hauna bei maalum, Shilingi 400, Shilingi 500, Shilingi 600 mwisho Shilingi 700,” anaongeza mkulima huyo. “Leo kuna mtu ananunua kwa Shilingi 700, sasa unalima mwani lakini hela huipati, unafanya kazi ya kutumia hela yako. 

SOMA ZAIDI: Bei Duni, Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Vilio Vikubwa vya Wakulima wa Mwani Z’bar

“Sisi walimaji wa mwani tunaomba tufanyieni kila jambo linalowezekana mtusukumie wateja ili tuwapate na sisi tupate kunafsika, tukiuza mwani tuwasomeshe watoto wetu.”

Hali ya kukosekana kwa masoko wanayokutana nayo wakulima hawa hivi sasa inawakumbusha miaka iliyopita ambapo wanunuzi wa mwani walikuwa wakiweka kituo cha manunuzi kwenye kila kijiji ambacho kilikuwa na wakulima wa mwani, suala ambalo kwa sasa halipo tena.

Mmoja wa watu ambao wanaukumbuka wakati huo ni Hadija Mbaruku ambaye ni mkulima wa mwani kutoka katika kijiji cha Ziwani. 

Hadija anasema kuwa humlazimu kusafiri umbali wa kilomita takribani tano kutoka kijijini kwao kwenda katika kijji cha Mnete, kata ya Msanga Mkuu kwa ajili ya kwenda kuuza mwani ambapo hulipia nauli ya usafiri wa pikipiki Shilingi 4,000 ili kufika huko.

‘Hakuna wanunuzi maalumu’

“Changamoto kubwa ni soko, hatuna wanunuzi maalumu,” Hadija anasema. “Kama sisi tunaotoka katika kijiji cha Ziwani ndiyo tunapata sana changamoto, afadhali wale wenzetu wanaoishi Mnete au Pwani kabisa, wakisema leo wanunuzi wamekuja basi wanakuwa rahisi sana kukimbilia soko.”

“Leo mteja akipatikana unaubeba mwani na bodaboda, unaupeleka huko Mnete, unalipa Shilingi 4,000, akiubeba kutoka kule kuuleta hapa [kama umekosa mnunuzi] unalipa Shilingi 4,000 tena,” aliongeza Hadija. 

“Kwa hiyo, wewe unafanya kazi ya kulipa nauli tu, hiyo pia kwetu changamoto. Kama ingekuwa mteja anakuja hapa hapa basi ingekuwa rahisi.” 

SOMA ZAIDI: Serikali, Wadau Waeleza Mikakati ya Kuboresha Kilimo cha Mwani Zanzibar

Subira Muhibu ni mwenyekiti wa kikundi cha Jivunie chenye wanawake wanaolima mwani katika kijiji cha Mkungu, kata ya Naumbu, halmashuri ya wilaya ya Mtwara. 

Subira ameiambia The Chanzo kuwa changamoto ya soko imeendelea kuwaumiza kwa kuwa wamekuwa wakitumia gharama kubwa kununua zana za uzalishaji wa mwani, zikiwemo kamba ambazo kwa sasa kama moja huuzwa Shilingi 5,000.

“Ikiwa bei inashuka, ina maana sisi tunaathirika sana maana yake, ukiachana na kamba, kuna viatu vya baharini, bila ya kuwa na viatu hivyo huwezi kwenda baharini kulima mwani,” alisema Subira. “Pia, kuna miti ambayo tunapandia mwani nayo ile tunanunua, muda mwingine tunaenda kukata maporini huko, inamaana nguvu kazi inatumika na pesa inatumika.”

“Kwa hiyo, kwetu inakuwa ni changamoto sana kwa sababu unaweza kuzalisha mwani mwingi sana lakini bei inakuwa ndogo ambayo nayo inabidi uigawe kama mafungu matatu,” aliongeza mkulima huyo. “Ununue vifaa vya kwendea baharini, ununue kamba, na uangalie masuala ya maisha nyumbani, kwa hiyo pesa inakuwa ndogo sana.”

Ulimaji wa mwani

Mkoa wa Mtwara una zaidi ya kilomita 100 za bahari zinazozalisha zao la mwani. Kwa kiasi kikubwa, zao hili linazalishwa katika wilaya Mtwara na kwa uchache katika manispaa ya Mtwara Mikindani. 

Kilimo cha mwani, kwa kiasi kikubwa, hufanywa na wanawake waliounda vikundi. Katika halmshauri ya wilaya Mtwara kuna vikundi 67 ambavyo vina wakulima 1,763 ambao huzalisha mwani kwa wastani wa tani 650 kwa mwaka.

Mbali na Mtwara, mikoa ya Lindi, Pwani pamoja na visiwa vya Zanzibar pia kuna wakulima wa zao hilo la biashara la mwani. Kwa mfano, Zanzibar, kwa mwaka 2023, ilizalisha tani 16,653 za zao hilo linalotumika pia kama malighafi ya kuzalishia bidhaa mbalimbali za urembo, kwa mujibu wa taarifa za Serikali visiwani humo. 

SOMA ZAIDI: Konokono Wanavyowaliza Wakulima Mbeya, Serikali Yatafuta Suluhu ya Kudumu

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Biashara (UNCTAD), kupitia ripoti yake iliyotolewa Machi 2024, ikilenga kuangalia fursa za bahari na mchango wa zao la mwani katika kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu, iliitaja Tanzania kuwa kwa mwaka 2023 ni taifa la nane kwa uzalishaji wa zao hilo duniani, huku kwa Afrika likiwa ni taifa la kwanza kwa kuzalisha zao hilo na kuliuza nje ya nchi. 

Ripoti hiyo ilionesha kwamba kwa mwaka 2015, uzalishaji wa zao la mwani nchini ulifikia kiwango cha juu cha tani 178,000 kabla ya kuporomoka mwaka 2021 hadi kufikia tani 81,000. 

Kushuka kwa kiwango hicho kulielezwa kuwa kunaweza kuwa kulisababishwa na milipuko ya magonjwa na wadudu, mabadiliko ya tabianchi, viwango vya chini vya usalama wa viumbe hai na  wakulima kulipwa bei ya chini.

Vita ya Urusi yatajwa

Bakari Rajabu ni meneja wa kampuni ya ununuzi wa mwani ya Mwani Mariculture, kampuni ambayo imekuwa ikinunua zao hilo tangu mwaka 1,980. 

Kwenye mahojiano yake na The Chanzo, Rajabu anasema kuwa kushuka kwa bei ya mwani kumechangiwa pia na vita vinavyoendelea kwenye baadhi ya nchi za magharibi, ikiwemo Urusi na Ukraine, nchi ambazo awali walikuwa wanunuaji wakubwa wa mwani. 

Mfanyabiashara huyo aliendelea kueleza kuwa hali hiyo imewathiri na wao kama wanunuzi kwani hivi sasa wamekuwa wakibaki na mzigo mwingi kwenye maghala kutokana na kukosa wateja kutoka nje ya nchi kama ilivyokuwa hapo awali.

“Kwa sasa mara nyingi oda za nje zinakuwa ni ndogo, na tunabakia na mzigo mkubwa kwenye maghala ambao haujasafirishwa,” Rajabu anaeleza. “Kwa hiyo, changamoto inakuwa hivyo kwamba mzigo tunakuwa nao mkubwa wakati uhitaji wake kule unakuwa mdogo.”

SOMA ZAIDI: Mwenye Kiwanda Rungwe Adaiwa Kuchelewesha Malipo ya Wakulima 13,000 wa Chai

“Hii inatuathiri kwa sababu inapopungua bei, wakulima wanavunjika moyo, na wakati mwingine athari inakuja sisi mzigo tunanunua kwa bei kubwa, inapokuja taarifa ya kushuka bei inatukuta wakati tuna mzigo mkubwa maghalani, kwa hiyo tunapata hasara zaidi,” aliongeza Rajabu.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya Mtwara, Abeid Kafunda, amekiri juu ya uwepo wa changamoto ya kushuka kwa bei na kukosekana kwa masoko ya uhakika ya zao la mwani wilayani humo, akiiambia The Chanzo kuwa hayo yote yanatokana na kushuka kwa bei ya zao hilo kwenye soko la dunia. 

Kafunda ametoa wito kwa wananchi, akiwataka wawe wavumilivu kwani Serikali inafanya jitihada za kuwatafutia masoko na kwa kuanza wameingia makubaliano na kampuni ya mwani kutoka Zanzibar (ZASCO) ambayo tayari imefanikiwa kulifikia soko la nje. 

Makubaliano waliyoingia na kampuni hiyo ni ya kuwasaidia wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara nao waweze kupata masoko ya nje, kwa mujibu wa maelezo ya Kafunda. 

Kuongeza thamani

Kwa upande wake, Dk Nazael Madalla, Mkurugenzi wa Utunzaji wa Viumbe Maji Kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ameiambia The Chanzo kuwa mipango ya Serikali katika kukabiliana na changamoto za masoko ni kuwafundisha wakulima kupitia vikundi vyao namna ya kuongeza thamani ya zao la mwani kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo wataziuza ndani na nje ya nchi. 

Dk Madalla akaongeza kuwa mpango mwingine ni ule wa ujenzi wa kiwanda kuchakata na kusanifu mwani huko Zanzibar unaofanywa na Serikali kwa lengo la kuchakata mwani unaozalishwa nchini ili kuwezesha wakulima kupata masoko ya ndani na kupunguza utegemezi wa masoko ya nje ya nchi kama ilivyo sasa.

“Kwa hiyo, wizara imekuwa ikifanya hizo juhudi za kuwafundisha hawa wakulima katika vikundi vyao jinsi ya kuongeza thamani na kutengeneza bidhaa mbalimbali,” alisema Madalla. 

“Na tunaona matumizi mengine, kwa mfano, pale Tanga kuna kiwanda cha kutengeneza mbolea zinazotokana na mwani. Kwa hiyo, hizo zote ni juhudi ambazo tunazifanya ili kuhakikisha kwamba wakulima wakilima wawe na sehemu ya kuuza.

“Vilevile, tumeanza kuwa na uhamasishaji mkubwa wa matumizi ya mwani nchini kama chakula, kwamba mwani ni chakula kizuri kwani una madini mengi,” Dk Madalla alimalizia kusema.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *