The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mwenye Kiwanda Rungwe Adaiwa Kuchelewesha Malipo ya Wakulima 13,000 wa Chai

Wasema hali hiyo inaathiri maisha yao, mwenye kiwanda adai kumaliza deni ndani ya mwezi Machi 2024.

subscribe to our newsletter!

Mbeya. Mvutano unaendelea kati ya wakulima 13,000 wa chai kutoka Rungwe mkoani hapa na mmiliki wa kiwanda cha chai cha Katumba juu ya ucheleweshwaji wa malipo ambao wakulima hao wameiambia The Chanzo unaathiri maisha yao na shughuli zao za kilimo.

Wakulima hao, wengi wao wakiwa ni kutoka Bonde la Mwakaleli, waliuza zao hilo la biashara mwezi Disemba mwaka 2023 wakitegemea kulipwa fedha zao ndani ya wiki mbili kama kanuni za Bodi ya Chai Tanzania zinavyoelekeza lakini mpaka sasa hawajapokea fedha.

Wakulima hao, ambao walishindwa kusema ni kiasi gani haswa wanakidai kiwanda hicho, waliiambia The Chanzo kwamba kucheleweshwa kwa malipo yao kunaathiri uwezo wao wa kuhudumia familia zao pamoja na kuendelea kujishughulisha na kazi yao hiyo ya kilimo.

Telezia Mahenge, mmoja wa wakulima hao, alisema kwamba mpaka sasa ameshindwa kupeleka watoto wake shule baada ya kushindwa kuwapatia mahitaji yao ya msingi kama vile sare na mahitaji mengine baada ya kuchelewa kupata malipo yake.

“Watoto mpaka sasa hivi hawajaenda shule, chai ndio zao tunalotegemea litusaidie,” Mahenge, mama wa watoto sita, alisema kwenye mahojiano na The Chanzo. “Tunashindwa hata tule nini na watoto.”

SOMA ZAIDI: Bei Duni, Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Vilio Vikubwa vya Wakulima wa Mwani Z’bar

Mahenge, 58, kutoka kijiji cha Mwela, anasema kwamba ameumizwa sana na hali hiyo, akiongeza: “Tumeumia sana. [Sisi] tunachuma chai hakuna faida yeyote, huyu muwekezaji wetu ametuumiza parefu.”

Noah Mwakasege ni mzee mwenye umri wa miaka 71 na mmoja wa walalamikaji aliyesema kwamba hali inayoendelea imemfanya yeye na wakulima wenzake washindwe kuhudumia zao la chai vizuri na hata kushindwa kuchuma chai kutokana na kukosa fedha za kuwalipa vibarua.

“Mpaka sasa hatujapata hela zetu,” Mwakasege alilalama. “Wachumaji wamegoma, hatuna hela ya kuwalipa.”

Ambilikile Mwasameta, msimamizi wa malalamiko haya ya wakulima wa muda mfupi, alisema kwamba wakulima hao wamechukua jitihada mbalimbali kuhakikisha wanapata malipo yao, lakini jitihada hizo zimeshindwa kuzaa matunda.

“Tuliandika barua kwa Mkuu wa Kiwanda, Mkuu wa Wilaya, pamoja na wabunge lakini barua hizi hazikujibiwa,” Ambilikile anaeleza.

SOMA ZAIDI: ‘Tunaona Ina Tija’: Alizeti Kuwaondolea Adha ya Korosho Wakulima Liwale?

Malalamiko haya yaliwasilishwa pia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, alipofika Mbeya kuzungumza na wananchi kama sehemu ya ziara yake ya nchi nzima ya kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho tawala nchini.

“Akaulizwa Mtendaji Mkuu Rebi Gabrieli kutoka katika kiwanda cha Katumba na Tukuyu kuhusu haya madai,” Ambilikile alisema. “[Rebi] alijibu kuwa ifikapo Februari 20, 2024, fedha za miezi miwili zitakuwa zimelipwa. Sijui kama ahadi hii ni ya kweli.”

Kwenye mahojiano yake na The Chanzo, Rebi alikiri kutowalipa wakulima fedha zao ndani ya mwezi mmoja, huku akibainisha sababu ya kucheleweshewa fedha zao.

“Biashara ya chai inasuasua, spidi ya kuuza chai ni ndogo sana, mamlaka husika ilisharipoti hili,” alisema Rebi. “Na ndiyo maana unaona Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe, amelazimika kuanzisha soko la chai la ndani hapa nchini. Kila kampuni ukienda imejaza chai. Soko la chai limeyumba.”

“Mpaka sasa tumeshawalipa wakulima hawa fedha zao za Disemba zaidi ya milioni 779, wanazo mifukoni mwao,” aliongeza Rebi. “Kwa hiyo, hapa wanatudai tu fedha za Januari ambazo tunatarajia kuwalipa Machi 20, [2024].”

SOMA ZAIDI: Wakulima Mbozi Wagoma Kuuza Kahawa Yao Wakidai Bei Hairidhishi

The Chanzo ilimuuliza Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jafari Haniu, kama anayafahamu malalamiko haya ambapo alimsihi mwandishi awatafute wenye kiwanda pamoja na wakulima, akisema yeye hawezi kulitolea maelezo suala hilo.

Zao la chai hulimwa katika wilaya 12 zilizopo kwenye mikoa sita nchini Tanzania, ikiwemo Mbeya, Njombe, Iringa, Kagera, Kilimanjaro na Tanga.

Mkoani Mbeya, ambako zao hili hulimwa zaidi wilayani Rungwe kukiwa na vyama vya ushirika tisa, wakulima waliweza kuuza kilo milioni 6.2 kwa bei ya Shilingi 366 kwa kilo moja kwa msimu wa 2023.

Modesta Mwambene ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Mbeya. Anapatikana kupitia mwambemo@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *