The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Tunaona Ina Tija’: Alizeti Kuwaondolea Adha ya Korosho Wakulima Liwale?

Wakulima wana matumaini kwamba zao hilo litawatoa kutoka kwenye dimbwi la umasikini.

subscribe to our newsletter!

Lindi. Mariamu Lingunje amekuwa akilima korosho miaka yake yote ya ukulima, akilazimika kukabiliana na changamoto lukuki zinazokuja na ulimaji wa zao hilo la biashara, kubwa ikiwa ni ukosefu wa soko la uhakika, hali inayoathiri bei ya zao hilo. 

Kwa sasa, hata hivyo, Lingunje na mamia ya wakulima wenzake mkoani hapa wamepania kuondokana na adha hizi kwa kujihusisha na kilimo kingine. Hiki ni kile kilimo cha zao la alizeti, zao muhimu kwenye utengenezaji wa mafuta ya kupikia.

The Chanzo ilimkuta Lingunje, 45, akiwa shambani kwake majira ya saa nne asubuhi akiendelea na shughuli za mavuno ya alizeti, ambayo mashudu yake hutumika kulisha mifugo, akiambatana na wenzake wanaounda kikundi kwa ajili ya ulimaji wa zao hilo linalochochea hisia za matumaini kwa wakulima walio wengi.

“Kilichotuvutia kwenye kilimo cha alizeti [ni kwamba] tunapanda, tunavuna, na tunauza,” Lingunje, mama wa watoto wa nne, aliiambia The Chanzo. Yeye ni katibu wa kikundi cha akina mama 22 kutoka kijiji cha Nganyaga wanaojihusisha na kilimo cha alizeti. 

“Tunapata mafuta ambayo tunauza na kupata fedha,” aliendelea kusema mama huyo huku akiwa ameshikilia zao hilo alilotoka kuvuna muda mfupi. “Ni faida na fursa ambazo kilimo cha korosho kimeshindwa kutupatia.”

Kwa ekari moja, Lingunje anasema yeye na kikundi chake wanaweza kuzalisha gunia kumi za alizeti kama kutakuwa na mvua ya kutosha. Lakini hakuna mvua ya kutosha, mkulima huyo alikiri. Kwa hiyo, wakulima hao huishia kupata kati ya gunia nne au tano ambazo anakiri siyo mbaya sana.

Alizeti juu, korosho chini

Lingunje na wenzake kwenye kikundi chao ni miongoni mwa wakulima kadhaa mkoani Lindi na mikoa ya jirani walioanza kukiendea kilimo cha alizeti kama sehemu ya kukimbia kero na usumbufu unaotokana na utegemezi wao wa zao la korosho na lile la ufuta, mazao mawili watu wa maeneo haya wamezoea kulima. 

Wakulima hawa siyo kwamba wameacha kulima mazao hayo, bali wameongeza tu zao la alizeti ili wanufaike na fursa inazotoa.

Mariamu Lingunje, katikati, akiwa na wanakikundi wenzake wanaochojishughulisha na kilimo cha alizeti wilayani Liwale, mkoani Lindi, wakivuna alizeti shambani. PICHA | OMARI MIKOMA

SOMA ZAIDI: Pembejeo za Ruzuku Zahusishwa na Kushuka kwa Uzalishaji wa Korosho Mtwara

Taarifa kutoka LSED, shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na shughuli za maendeleo wilayani Liwale, na ambalo limekuwa likiwahamasisha wananchi walime zao la alizeti, zinaonesha kwamba mpaka kufikia Juni 2023, kulikuwa na wakulima 372 wa zao hilo wilayani humo, wanaolima eneo lenye ukubwa wa ekari 1,250. 

Jumla ya tani 45 za alizeti zimezalishwa ambazo baada ya kukamuliwa zilizalisha jumla ya lita 150,000 za mafuta, taarifa hizo kutoka LSED zinaonesha.

Kushamiri huku kwa kilimo cha alizeti wilayani Liwale kunaenda sambamba na kuendelea kuporomoka kwa bei ya korosho, hali ambayo imekuwa ikiwasumbua wakulima kwa miaka mingi, na hivyo kutafakari namna mpya zinazoweza kuwaondoshea usumbufu huo.

Taarifa kutoka Bodi ya Korosha Tanzania zinaonesha kwamba bei ya kilogramu moja ya korosho ya tabaka la kwanza imeshuka kutoka Sh4,128 kwa msimu wa 2017/2018 mpaka Sh2,200 kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023. 

Hali hii pia imeenda sambamba na kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo la biashara, taarifa hizo zinaonesha. Kwa mfano, uzalishaji wa korosho umeshuka kutoka tani 313,826 kwa msimu wa 2017/2018 mpaka tani 188,360 kwa msimu wa kilimo wa 2022/2023. 

Wakati Serikali imekuwa ikihusisha anguko hili na athari za tabianchi, wakulima wanadhani uamuzi wao wa kuelekeza nguvu kwenye kilimo cha alizeti pia unaweza kuwa umechangia.

Upekee wa alizeti

Hassani Mpako, mkulima wa korosho ambaye sasa ameamua kulima alizeti, ni moja kati ya wakulima hawa ambaye anafichua siri ya wakulima wa alizeti kunufaika zaidi na zao hilo kuliko wakulima wa korosho kunufaika nalo. 

Mpako anasema kwamba hali ya ukosefu wa viwanda ambavyo vingeziongezea thamani korosho, pamoja na zao hilo kutegemea zaidi soko la nje, kunawapunguzia wakulima wake uwezo wa kufaidika nalo vile inavyopaswa.

SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Tabianchi Yatajwa Kuathiri Kilimo cha Korosho Lindi, Mtwara

“Kwa upande wa alizeti, hali ni tofauti kabisa,” alisema Mpako kwenye mahojiano na The Chanzo. “Viwanda vya kugeuza alizeti kuwa mafuta vipo hapa. Kuna soko kubwa la mafuta ya kula hapa wilayani na nchini kote kwa ujumla. Kwa kulima alizeti, tunalisambazia hilo soko na hivyo kupata fedha tunazohitaji wakati wa kufanya hivyo.”

Shija Agro-Processing, kilichopo Likongewele hapa Liwale, ni moja kati ya viwanda kadhaa vilivyopo mkoani Lindi vinavyojihusisha na utengenezaji wa mafuta ya kula kutoka kwenye zao la alizeti. Meneja wake, Issa Said, aliiambia The Chanzo kwamba msimu wa mwaka 2021/2022 waliweza kukamua tani 60 za alizeti. 

Baadhi ya wakulima wakiwa kwenye kiwanda kidogo cha kukamua alizeti cha Shija Agro-processing kilichopo Liwale, mkoani Lindi. PICHA | OMARI MIKOMA

Kwa msimu unaoendelea wa kilimo, yaani 2022/2023, Said anasema matarajio ni kupata tani nyingi zaidi kutokana na wakulima kuendelea kuongezeka kwenye vijiji mbalimbali wilayani hapa.

“Dalili zinaonesha kwamba, kutokana na mwenendo wa upokeaji wa mizigo, wananchi wengi wamehamasika,” alisema meneja huyo. “Alizeti imelimwa kwa wingi. Takribani kila kijiji, wakulima wamelichukulia kama ni zao la kimaendeleo kama mazao mengine, na tunategemea tutapokea mzigo mwingi zaidi.”

The Chanzo ilimuuliza Ally Kamuna, Katibu wa LSED, shirika linalojihusisha na uhamasishaji wa kilimo cha alizeti wilayani Liwale, ni kwa namna gani wakulima hao watahakikisha changamoto zilizopo kwenye zao la korosho hazitakuja pia kwenye zao la alizeti?

“Zao la alizeti, kama tunavyoendelea kushawishi, mkulima hatapata gharama ya kusafirisha, yaani anavuna kijijini kwake na kuweza kukamua pale kijijini kwake anaona ni zao linalolipa zaidi,” Kamuna alieleza. “Alizeti inalipa kwa kuuza kwa ajili ya kutengeneza mafuta, inalipa kwa kuitumia kama chakula, na inalipa kwa kutumia mashudu yake kulisha mifugo.”

Serikali ya bariki

Uamuzi huu wa wakulima kuikumbatia alizeti kama mkombozi wao unatekelezwa kwa baraka zote za Serikali, huku Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Mustapha Maghembe, akisema kwamba Serikali yenyewe imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kulima zao hilo.

“Zao la alizeti ni moja ya mazao ya kibiashara ambayo halmashauri, kwa kushirikiana na wadau wengine mbalimbali, imekuwa ikihamasisha kulima katika wilaya hii kwa lengo la kuanzisha chanzo kingine mbadala cha mapato kwa wakulima,” Maghembe alisema kwenye mahojiano yake na The Chanzo.

SOMA ZAIDI: Tozo, Pembejeo Zinavyowatesa Wakulima wa Korosho Mtwara

Moja kati ya hatua ambazo Serikali imekuwa ikichukua kuchochea kilimo cha zao hilo ni kugawa mbegu bure kwa wakulima wilayani humo ambapo mpaka sasa imegawa zaidi ya tani tano. Maghembe anajivunia hatua hii, akibainisha baadhi ya faida ambazo wilaya inapata kutokana na kilimo cha alizeti.

“Mafanikio makubwa sana ambayo tumeyapata mwaka jana [wa 2022] ni kwamba wilaya iliweza kujitosheleza kwa mafuta ya kula,” alisema afisa huyo. “Badala ya kununua mafuta ya kula kutoka nje, wilaya ilijitosheleza kabisa kwani wakulima walikuwa wanakamua mafuta yao, wanayatumia kwenye kaya lakini yale yaliyobaki yalikuwa yanauzwa kwa bei nafuu.”

“Bei ya mafuta [ya kula] ilishuka kutoka Sh9,000 kwa lita moja mpaka Sh5,000 ambayo tunayo mpaka sasa hivi kutokana na wingi wa alizeti ambayo tumezalisha mwaka jana,” aliongeza Maghembe. “Tunaona huo ni mwelekeo mzuri.”

Kwa kujiingiza kwenye kilimo cha alizeti, mkoa wa Lindi unaongeza orodha ya mikoa ambayo tayari wananchi wake wamekuwa wakijihusisha na kilimo hicho kwa miaka mingi sasa, ikiwemo ile ya Singida, Simiyu, Manyara, na Tabora.

Matumaini mapya

Wakulima wengi wa alizeti wilayani Liwale wanaonekana kuwa na matumaini kwamba zao hilo litawasaidia kuwakomboa kiuchumi, ikiwemo kuongeza kasi ya mafanikio ya juhudi zao za kujikwamua kutoka kwenye dimbwi la umasikini.

Tanzania kwa sasa inakadiriwa kuwa na uhitaji wa mafuta ya kula wa zaidi ya tani 650, 000. Hata hivyo, uzalishaji unakakadiriwa kuwa ni tani 290, 000 tu na kiasi cha tani 360, 000, sawa na asilimia 55, huagizwa kutoka nje ya nchi na kuigharimu Serikali kiasi cha Shilingi bilioni 470 kila mwaka.

SOMA ZAIDI: ‘Sitegemei Kuvuna Kitu’: Wakulima Mtwara Walia na Ukosefu wa Mvua

Ally Abdalla Mmou, mkulima wa alizeti wilayani Liwale, anatambua uwepo wa uhitaji huu wa mafuta ya kula, akiieleza The Chanzo kwamba baada ya kulima ekari moja na nusu na kupata gunia nne za zao hilo na kuona faida yake, amekusudia kulima eneo kubwa zaidi kwenye msimu unaokuja.

“Mipango yangu mwakani ni kuongeza shamba kwani mwaka huu nimelima ekari chache,” Mmou, baba wa watoto wawili, alisema. “Nitapanua eneo la shamba langu na kulifanyia kazi kwa wakati. Naamini mafaniko yatakuwa mara tatu ya haya ya sasa.”

Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *