“Mzazi ni daktari” ni kauli inayobeba uhalisia na maana kubwa. Ingawa sisi wazazi sio madaktari tuliohitimu taaluma hiyo, lakini tuna jukumu muhimu sana katika kuhakikisha afya na ustawi wa watoto wetu kihisia, kimwili, kiakili na kijamii kwa ujumla.
Wazazi tuna uwezo wa kuimarisha afya ya watoto wetu kwa sababu tunapokuwa tunajali na kufuatilia afya yao ndipo tunapothibitisha kuwa wazazi ni madaktari.
Wazazi tunaweza kutambua ishara za ugonjwa au matatizo ya maendeleo ya watoto wetu mapema kuliko mtu mwingine yeyote. Tunajua tabia za kawaida na zisizo za kawaida kwa watoto wetu na tunaweza kutambua mabadiliko madogo yanayoashiria matatizo. Kwa mfano, wazazi tunaweza kujua kwa haraka kuwa watoto wetu wana dalili za homa kwa kuwashika tu au kwa kuangalia mabadiliko ya tabia zao.
Wazazi tunaweza kutoa huduma ya kwanza ya msingi kwa watoto wetu wakati wa dharura. Tunaweza kujua nini cha kufanya wakati wa homa, au majeraha madogo. Tangu enzi za bibi zetu watoto wanapokuwa na homa, mzazi huchukua maji ya kawaida na kitambaa ili kumkanda mtoto kwa nia ya kupunguza joto, pia kumpatia mtoto dawa kama panadol ili kuweza kupunguza joto kabla ya kumpeleka mtoto hospitali. Hivyo, kama wazazi makini tujitahidi kuwa na akiba za dawa na vifaa vya huduma ya kwanza kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya ghafla ya afya za watoto wetu.
SOMA ZAIDI: Ni Zipi Tabia Zinazoweza Kutufanya Tuwe Wazazi Bora Kwa Watoto Wetu?
Katika ufuatiliaji wa afya, wazazi tuna jukumu la kuhakikisha watoto wetu wanapokea chanjo zote zinazohitajika kuzuia magonjwa kama polio, pepopunda, kuharisha, minyoo, surua n.k, Tunahakikisha wanafanyiwa vipimo vya afya mara kwa mara na wanapata huduma zote muhimu za afya pia, tunafuatilia kwa karibu afya ya watoto wetu na kumuuliza daktari maswali kuhusu afya zao.
Wazazi tuna nafasi ya pekee ya kuwa na uelewa wa maendeleo ya watoto wetu na tunaweza kutambua kama mtoto anakua kwa kasi inayotarajiwa na kama kuna ucheleweshaji wowote wa maendeleo. Wazazi tunaelewa maendeleo katika kila hatua ya ukuaji wa watoto wetu, kwa mfano kwa kawaida kuanzia miezi minne mtoto huwa anaanza kukaa baada ya kukaa inafuata hatua ya kutambaa na baadae kutembea na wengine huanza kusimama wakiwa na mwaka mmoja mpaka miwili ndipo mtoto anapoanza kutembea.
Maendeleo ya mtoto yakiwa kinyume na hapo mzazi ataanza kupata wasiwasi na kuomba ushauri wa wataalamu wa afya na malezi. Katika kipindi hiki utakuta wazazi wengi wanazingatia vyakula maalum vyenye kila aina ya virutubisho na kuhakikisha wanawanyonywesha watoto ipasavyo ili wakue katika hatua stahilki na wasipate maradhi ya utapiamlo.
Katika usalama wa mazingira, wazazi tuna jukumu la kuhakikisha kuwa mazingira ya nyumbani na wanayocheza watoto ni salama kwa watoto wetu na kwamba wanapata muda wa kutosha wa kulala na wanalala kwa wakati. Mazingira yasiyo salama ni hatari kwa watoto wetu kwa sababu huweza kusababisha watoto kufanyiwa vitendo vya kikatili kama vile kubakwa, kulawitiwa au kujiingiza kwenye tabia zisizo njema katika jamii kama wizi n.k.
Lakini pia watoto wadogo kabisa wanaweza kujiumiza na kupata majeraha, hivyo utakuta wazazi wanahakikisha vitu hatarishi kama visu, dawa, moto, ndoo za maji, mabwawa ya kuogelea, umeme n.k vinawekwa mbali na watoto ili kulinda afya zao.
SOMA ZAIDI: Tunachoweza Kufanya Wazazi Kuwanusuru Watoto Wetu na Matatizo ya Afya ya Akili
Tukizungumzia msaada wa kihisia wazazi tunaweza kuwa chanzo kikubwa cha msaada kwa watoto wetu kwa kuwafariji, kuwatia moyo, kuwaonesha upendo, kuwajali, kuwasikiliza na kuwafundisha jinsi ya kukabiliana na hisia zao. Ni muhimu sana kwa mtoto kupata msaada wa kihisia kwa sababu humjengea kujiamini na kuwa vizuri kiakili hasa katika ukuaji wake na masomo yake.
Wataalamu wa afya ya akili wanaamini kuwa hata watoto wadogo kabisa wanapitia sonona kama mazingira na afya ya akili ya wazazi itakuwa imeathiriwa na changamoto za maisha.
Kwa kumalizia, tutambue nafasi ya kipekee ambayo kila mzazi anayo katika afya ya mtoto. Kuwa daktari wa kwanza wa watoto wetu ni jukumu la muhimu mno na linalohitaji umakini na nia ya kutaka kuwajua na kuwasimamia watoto kikamilifu kama mzazi.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.