Hotuba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ilikatishwa na waombolezaji katika msiba wa Marehemu Ali Kibao, wakati Waziri huyo akifanya dua maalum leo Septemba 09,2024, katika msiba huo uliofanyika mkoani Tanga.
Wakati akiendelea na dua hiyo, waombolezaji walianza kupiga kelele huku wengine wakimtaka ajiuzulu, hali hiyo ilizua sintofahamu na kumbidi Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kuingilia kati kutuliza mambo.
“Naomba tukae kimya tumalize sehemu ya hotuba, namwomba Mheshimiwa Waziri amalizie hotuba yake. Hatuwezi kufikia mahali pa kuvurugiana heshima kwa kiwango hicho,”Alieleza Mbowe.
“Waziri atamaliza hotuba yake halafu mimi nitamaliza hotuba zote, Mheshimiwa Waziri tafadhili njoo malizia hotuba yako,” Mbowe alimkaribisha tena Masauni katika tukio lilochukua takribani dakika saba mpaka hali kutulia.
Baada ya kauli ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Masauni aliendelea na hotuba yake ambapo alianza kwa kutoa salamu za rambirambi kutoka kwa Rais Samia, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.
“Tumesikitishwa sana na kusononeshwa na kuhuzunishwa ni jambo ambalo kwa kweli halikupaswa kutokoea hasa katika nchi yetu ambayo miaka yote tumekuwa tukijivunia juu ya usalama na amani katika nchi hii,” alieleza Masauni.
“Niwahakikishie waombolezaji wote hususani familia, kama serikali hatutaliacha liende hivi hivi, maelekezo ya mheshimiwa Rais yameshaanza kutekelezwa na hatua zitachukuliwa kwa wale wote watakaobainika kuhusika.”
“Nitoe wito kwa mtu yeyote kuacha kushutumu badala yake kama ana kielelezo cha mtu yeyote kuhusika na jambo hili akiwasilishe ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kusaidia kuweza kupata wahusika na waweze kuchukuliwa hatua,” aliongeza Masauni huku waombolezaji wakisikiliza kwa utulivu.
Masauni alisisitiza kuwa serikali haitavumilia jambo lolote linalokiuka haki za watu ikiwemo haki ya kuishi.
One Response
Ajiuzuru haraka sana. Kitendo hicho kutokea mwenye dhamana ni yeye alipaswa kutengeneza mifumo ya kuzuia hayo na hio ndo kazi yake na ameshindwa kuifanya. Huu ni moja kati ya misiba mingi iliotokea chini yake.