Agosti 16,2024, Mwanaharakati Deusdedith Soka akiwa katika ofisi za The Chanzo aliongea maneno ambayo yalikua kama maneno ya mtu aliyeona hatari kubwa mbele yake. Soka aliiambia The Chanzo kuwa maisha yake yako hatarini na akaendelea kuongea kama mtu anaoyeongea na watekaji wake.
“Yaani kuna ile tunasema kwamba basi mmechukua kila kitu; basi msituteke, msituumize, mtuachie ule uhai wetu tuishi, tuachieni uhai, tuachieni tufurahi. Unaanza kuchukua mmoja mmoja kama mwewe anavyochukua vifaranga,” alieleza Soka. Siku mbili baada ya hapo, Soka alitekwa mnamo Agosti 18,2024, ambapo hajaonekana mpaka leo.
Katika hali ya kipekee, leo Septemba 09,2024, Godbless Lema, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini ameongea maneno yanayofanana na Soka akieleza hali ya hatari anaoyoiona mbele yake, hii ni baada ya rafiki yake na kiongozi mwenzake wa CHADEMA, Ali Kibao kuuwawa baada ya kutekwa mnamo Septemba 06,2024.
“Mheshimiwa Waziri wakati unaingia hapa naona tena meseji nyingine ya kwamba mimi na Boni tukiweza mwezi huu kuishi bila kutekwa na kuuwawa tushukuru Mungu. Mheshimiwa Waziri mimi nimeshakufa jana, familia zetu zinalia na leo nahudhuria mazishi ya rafiki yangu,” alieleza Lema akielekeza hotuba yake kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni.
“Mimi sasa nikirudi kwenda Arusha sijui kama nitafika salama, mtoto wangu analia, mke wangu analia. Mheshimiwa Waziri nilimuahidi mtoto wangu nitakuwepo kwenye Send-Off yake siku moja, ana miaka 15, nisaidie tu siku moja akiolewa niwepo, mnatuumiza,” aliongeza Lema.
Katika msiba huo Masauni alitoa rai watu kuacha kutoa shutuma badala yake wapeleke vielelezo husika ili wahalifu waliofanya mauaji wakamatwe.