Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeeleza leo Septemba 10,2024, kuwa imekamata Tani 1.8 ya Bangi inayofahamika kwa jina la ‘Skanka’ huku watuhumiwa watano wakitiwa mbaroni.
Akizungumza zaidi kuhusu aina hiyo ya Bangi iliyoanza kuingizwa nchini katika miaka ya hivi karibuni, Kamishna wa DCEA, Aretas Lyimo amefafanua kuwa bangi hiyo ya kusindika ina kiwango kikubwa cha kemikali ya Tetrahydrocannabinol (THC) jambo ambalo inaifanya iwe hatari zaidi.
Skanka imeitwa hivyo kutoka kwenye jina la kingereza ‘Skunk’ ambapo kwa maeneo mengi ya nchi za Magharibi bangi ya aina hiyo ilikua ikifahamika kwa jina lisilo rasmi ‘Skunk Weed’.
Jina la Skunk limetokana na harufu kali inayotolewa na bangi hiyo ambayo wajuzi wa mambo waliifananisha na mavi makali yanayonuka yanayotolewa na mnyama Kicheche (Skunk) pindi anapoona hatari.
Kemikali za Tetrahydrocannabinol (THC) ndizo zinazosababisha hali ya ulevi kwa watumiaji wa Bangi, ambapo kwa mujibu Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Duniani ya mwaka 2023 ilionesha kuwa takribani watu milioni 228 ni watumiaji wa bangi duniani. Kamishna Lyimo ameoinya jamii ya Watanzania kuwa makini na bangi hiyo yenye madhara makubwa.
“Kiambata hai cha THC kinaweza kusababisha kuharibu mfumo wa fahamu, akili na magonjwa yasiyoambukiza kama vile moyo,figo na ini. Matumizi ya Skanka kwa wajawazito yanaweza kusababisha madhara ya mtoto aliye tumboni ikiwemo kuathiri maendeleo ya ubongo na kuzaliwa na uzito mdogo,” alieleza Aretas Lyimo.
“Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali za kulevya Duniani iliweka bayana kuwa maeneo yaliyohalalisha matumizi ya bangi kumekuwa na ongezeko la watu wanaohitaji tiba kutokana na matumizi ya bangi, sambamba na kuongezeka kwa watu wenye matatizo ya akili na waliojaribu kujiua,” aliendelea kufafanua Lyimo.
SOMA: ‘Bangi Kama Tiba’:Serikali Yataka Umakini na Tafiti Juu ya Kuruhusu Matumizi ya Bangi
Lyimo alieleza kuwa Mamlaka hiyo imeanza utafiti wa kuichunguza bangi hiyo ya Skanka ili kuangalia sababu zinazoifanya iwe na madhara makubwa.
Watuhumiwa waliokamatwa katika operesheni iliyofanikisha kukamatwa kwa bangi hiyo ni pamoja na Richard Henry Mwanri (47) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Makonde na Felista Henry Mwanri mkazi wa Luguruni (70) ambaye ametajwa kama mmiliki wa nyumba zilipokamatwa dawa hizo za kulevya.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Richard Mwanri amekuwa akiingiza Bangi hizo akitumia mbinu mbalimbali kama kuchanganya na bidhaa zingine na kuzisambaza kwa wauzaji wengine nchini.
Watuhumiwa wengine waliokamatwa kwenye tukio hilo ni Athumani Koja Mohamed (58) mkazi wa Tanga, Omary Chande dereva bajaji mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam na Juma Abdalah Chapa (36) ambaye ni mkazi wa Kiwalani Dar es Salaam. Katika operesheni hiyo, gari aina ya Mitsubishi Pajero yenye namba za usajili T 551 CAB na bajaji yenye namba za usajili MC 844 CZV vilikamatwa.
Katika taarifa yake Kamishna Lyimo ametoa tahadhari kwa wamiliki wa nyumba kutoruhusu mizigo wasiyoifahamu kuwekwa katika nyumba zao. Lyimo pia ameeleza kuwa wanachunguza kama kuna mtandao wa kihalifu unaohusisha maofisa wa serikali katika mipaka mbalimbali ambapo bidhaa hizo zimekuwa zikipita.
“Lakini pia tutoe wito kwa watumishi wa serikali waliopo mipakani, haiwezekani dawa nyingi kiasi hiki zinapita mipakani bila wao kuwa na uelewa nazo bila wao kugundua. Kwa sababu ni vifurushi vikubwa ambavyo vinapita mipakani na hizi dawa zinachanganywa pia na bidhaa nyingine zinazopita mipakani,” alieleza Lyimo.
Mwaka 2023, ulivunja rekodi kwa bangi nyingi zaidi kukamatwa nchini, ambapo bangi tani 1,757 zilikamtwa. Kiwango hiki ni kikubwa zaidi kulinganisha na tani 326 zilizokamatwa kati ya mwaka 2014 mpaka mwaka 2022. Katika mwaka huo bangi kali ya Skanka ilikamatwa kilo 423.