Kwa kawaida, watoto huwa ni wagumu kugawana vitu vyao, jambo ambalo linatufikirisha sana wazazi, tukiogopa watoto wetu watakua na tabia ya uchoyo.
Mara nyingi, watoto hugombana wakipigania vifaa wanavyopenda kuchezea, au hugombania juu ya zamu ya kuchezea vifaa hivyo na hata vyakula. Hali hii hufanana na uwanja wa vita na huwachanganya sana wazazi na walezi.
Lakini je, unaweza kuamini kwamba watoto kutokukubali kugawana kitaalamu ni sehemu ya hatua muhimu ya ukuaji wao kihisia na kijamii, na si uchoyo kama ambavyo wengi wetu hudhani? Tafiti zinaonesha kwamba kugawana ni tabia inayofundishwa, na ni kitu ambacho watoto huiga na hukua nacho na siyo kuzaliwa nacho.
Kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitatu, dhana ya umiliki na kumiliki vitu ina uzito mkubwa. Katika hatua hii, bado wanajenga hisia zao binafsi na uelewa wa ulimwengu unaowazunguka.
Wataalamu wa saikolojia wanaelezea kipindi hiki kama kipindi cha “ubinafsi,” kumaanisha kuwa watoto wanazingatia zaidi mahitaji na matamanio yao wenyewe.
Umiliki binafsi
Hii haimaanishi kuwa ni wachoyo; badala yake, akili zao, kwa wakati huo, zimeundwa ili kutoa kipaumbele kwa usalama, faraja, kupata na kulinda wanachotaka. Kwa wakati huu, kipaumbele chao kinakuwa kwenye umiliki binafsi wa vitu mbalimbali.
SOMA ZAIDI: Fahamu Namna ya Upangaji wa Ratiba kwa Makuzi Bora ya Mtoto
Mtaalamu wa saikolojia ya makuzi na maendeleo ya watoto, Dk Jean Piaget, aliona kwamba watoto katika hatua hii ya ukuaji hawawezi kuelewa kwamba wengine wana mitazamo, au hisia, tofauti.
Wanaposhikilia kifaa cha kuchezea na kukataa kukiachia, si kwamba wanakataa kwa ubaya bali ni ishara ya uelewa wao mdogo wa kwamba mtu mwingine pia anaweza kukitaka kitu hicho. Akili zao bado zinajenga uwezo wa kuelewa hisia za wengine, jambo ambalo ni muhimu kwa kuelewa kwa nini kugawana ni muhimu.
Watoto wanapoanza kwenda shule ya awali, kawaida kati ya umri wa miaka mitatu na mitano, uelewa wao wa haki huanza kuongezeka. Katika umri huu, wanakuwa na ufahamu zaidi wa mienendo ya kijamii inayowazunguka.
Hata hivyo, watoto kugawana katika hatua hii mara nyingi ni kama kuna faida kwao. Mfano “Nitakupa kigari hiki uchezee kama utanipa mpira wako.”
Tafiti zinaonyesha kwamba watoto huanza kujifunza taratibu kuwa na huruma, wanajifunza kuelewa jinsi matendo yao yanavyoathiri wengine. Huruma inawawezesha watoto kuanza kutambua hisia za wengine, na ukuaji huu wa kihisia hujenga msingi wa watoto kuweza kujumuika na watu wengine katika jamii na kujifunza tabia chanya kama kugawana. Hata hivyo, hii huchukua muda mpaka mtoto azoee.
Dhana ya haki
Kufikia umri wa miaka sita au saba, watoto wengi huanza kuelewa dhana ya haki na wana uwezo mzuri wa kugawana vitu bila kulazimika kupata kitu badala yake. Mabadiliko haya mara nyingi yanatokana na kuongezeka kwa ushirikiano na kujichanganya kijamii kupitia marafiki, wakiwa shuleni, na mwongozo wa wazazi wakiwa katika familia.
SOMA ZAIDI: Ulikuwa Unafahamu Kwamba Kuongopa ni Sehemu ya Makuzi ya Mtoto?
Katika hatua hii, watoto huanza kuelewa kwamba kugawana kunachochea ushirikiano, urafiki, na uaminifu. Tafiti kutoka kwa wataalamu wa maendeleo ya watoto zinaonesha kwamba ushawishi wa rika, au peer influence kwa kimombo, ni muhimu katika kuhamasisha tabia za kugawana.
Watoto wanajifunza kutoka kwa watoto wenzao na wanaposhiriki katika shughuli za vikundi mara kwa mara wana uwezekano mkubwa wa kugawana, si kwa wajibu bali kutokana na ufahamu wao unaokua wakiwa pamoja.
Ni muhimu kutambua kuwa bado kutakua na wakati ambapo mtoto atagoma kugawana vitu na wenzake, lakini tabia hii haipaswi kuonekana kama ni kushindwa kujifunza, bali kama mabadiliko ya kawaida katika ukuaji wao wa kihisia na kijamii.
Ni muhimu kwa sisi wazazi kutambua kwamba mtoto kuwa na hisia za umiliki, au possessiveness kwa kimombo, sio lazima kuwa jambo baya, na haimaanishi kwamba mtoto ni mchoyo.
Umiliki katika hatua fulani za maendeleo huwasaidia watoto kuimarisha ufahamu wao juu ya utambulisho wao. Wataalamu wa saikolojia ya mtoto wanaamini kuwa hitaji hili la kumiliki huwafundisha watoto mipaka muhimu, ikiwa ni pamoja na kuelewa nini ni chao na kuheshimu kinachomilikiwa na wengine.
Badala ya kuwalazimisha watoto kugawana kwa nguvu, wazazi tunaweza kuwasaidia kwa kuwaongoza. Tuwaeleze kwa nini kugawana ni muhimu na tuwaoneshe tabia za kugawana kwa kuwa mfano bora kwao, maana sisi wenyewe tukiwa wachoyo, watoto wetu watakuwa na tabia hiyo.
SOMA ZAIDI: Ni Zipi Tabia Zinazoweza Kutufanya Tuwe Wazazi Bora Kwa Watoto Wetu?
Pale mtoto atakapomgawia mwenzake kitu chake kwa hiari, tujitahidi kumpomgegeza, na pale atakapokataa, tuzungumze nae na siyo kuwaadhibu kila mara, au kuwalazimisha. Kumlazimisha mtoto kugawana wakati mwingine kunaweza kusababisha chuki kati yake na sisi wazazi au na watoto wenzake.
Dondoo
Tunawezaje kuwahamasisha watoto kugawana bila kuwalazimisha na kutumia ukali?
Ili kuwasaidia watoto wetu kupenda na kujua umuhimu wa kugawana, ni lazima kufanya nao mazoezi madogomadogo.
Wanapoenda kucheza na watoto wenzao, tuwakumbushe kwa upole kuhusu kugawana na kushirikiana wakati wa kucheza. Tunaweza kumwambia mtoto, “Inaonekana rafiki yako angetamani sana kuchezea mpira wako, si tunaweza kumgawia acheze kwa dakika chache?”
Pia, kutoa mbadala, au kupanga zamu za kuchezea kitu, kunaweza pia kufanya mchakato huu usiwe mgumu sana kwa mtoto.
Katika baadhi ya matukio, watoto wanaweza kugawana kwa urahisi wanapopewa udhibiti. Kwa mfano, tunaweza kumwambia mtoto, “Ungependa kumgawia mwenzako mdoli wako sasa au baada ya dakika tano?” Kwa njia hii, mtoto anajisikia kuwa ana mamlaka, au nguvu, ya kufanya uchaguzi, hivyo ana uwezekano mkubwa wa kugawana kwa hiari.
Kuelewa kwamba kugawana ni tabia inayofundishwa kunaweza kubadilisha jinsi sisi, kama wazazi, tunavyolikabili jambo hilo. Badala ya kuona kama sifa ambayo watoto wanayo au hawana, tunaweza kuiona kama sehemu ya ukuaji wao wa kijamii na kihisia.
SOMA ZAIDI: Tunachoweza Kufanya Wazazi Kuwanusuru Watoto Wetu na Matatizo ya Afya ya Akili
Watakapojifunza kuhusu haki, huruma, na ushirikiano, watoto wataunda njia zao za kugawana kwa namna inayolingana na umri wao na jinsi tunavyowaongoza.
Basi, tujitahidi kuwa wavumilivu na wapole pale mtoto atakaposhikilia mpira, au mdoli, wake na kukataa kugawana na rafiki, au ndugu yake. Tuchukue muda kutafakari na kukumbuka kuwa ni sehemu ya ukuaji na maendeleo yake.
Kadri watakavyozidi kukua na tukiwaongoza vizuri, watoto wetu watakuja kuwa watu wakarimu, wenye huruma, na ambao wanaelewa thamani ya kutoa na kushirikiana.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.