The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Sakata la Lissu Kushitaki Kampuni ya Mawasiliano, Wanasheria Wafunguka

Mawakili wasema hata kama kampuni hiyo ilishauzwa, Lissu anaweza kuishtaki na akashinda kutokana na ushahidi atakaouwasilisha.

subscribe to our newsletter!

Mbeya. Septemba 25, 2024, Makamu Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA, Tundu Lissu, alitangaza uamuzi wa kuishtaki kampuni ya mawasiliano ya Tigo ilyokuwa inamilikiwa na kampuni mama ya Millicom kwenye mahakama za kimataifa, baada ya kudai kuwa kampuni hiyo ilihusika katika kutoa taarifa zake, taarifa ambazo anadai ziliwezesha  shambulio lake la risasi mnamo Septemba 07, 2017. 

Shambulio hilo lilifanyika majira ya mchana, Lissu alipokuwa akitokea bungeni akielekea nyumbani kwake Area D, jijini Dodoma, ambapo washambuliaji walivamia gari lake na kulipiga risasi 38, huku risasi 16 zilimpata katika sehemu mbalimbali za mwili wake kupelekea makovu na ulemavu wa kudumu baada ya kupata matibabu.

Baada ya kupita miaka saba tangu lilipotokea tukio hilo, Septemba 24, 2024, gazeti la The Guardian liliibua taarifa za madai ya Millicom kuhusika kutoa taarifa binasfi za Lissu kwa Serikali, kutokana na ushahidi uliowasilishwa kwenye Mahakama moja huko Uingereza ambako mfanyakazi wa zamani wa Millicom hapa Tanzania, Michael Clifford, anaishitaki kampuni hiyo kwa madai ya kufukuzwa kazi baada ya kufichua kashfa hiyo.

Clifford alifanya uchunguzi wa kina kuhusina na vitendo vya kampuni hiyo kutoa taarifa za Lissu na baada ya kukamilisha uchunguzi wake aliwasilisha ripoti kwa waliokuwa watendaji wake wakuu, ripoti ambayo ilieleza jinsi kampuni hiyo ya mawasiliano  ilivyokuwa ikitoa taarifa za mteja wao tangu Agosti 22, 2017, kwa njia ya WhatsApp. 

Baada ya Clifford kufichua kashfa hiyo mahusiano yake na watendaji wakuu wa kampuni yalianza kuzorota na ilipofika mwaka 2019 akafukuzwa kazi. Hivyo, Clifford akaamua kuishtaki kampuni hiyo akidai kuwa hakufukuzwa kihalali kwani madai ya kutimuliwa kwake yalitokana na yeye kuibua kashfa hiyo. 

“Sikwenda Mahakamani kwa sababu sikuwa na ushahidi wa kutosha lakini sasa tunao ushahidi unaotosheleza kufungua kesi,” alisema Lissu wakati akizungumza na vyombo vya habari kwenye makao makuu ya chama hicho yaliyopo Mikocheni, Dar es Salaam. 

“Tunataka tujue ukweli [wa ni] nani aliyetoa amri niuawe. Watuletee ushahidi wamseme wao nani aliyewaambia Tigo wanifuatilie. Tunataka majina na vyeo, kama walilipwa, kama Tigo walilipwa watuambie walilipwa kiasi gani?”

Lissu ambaye alikuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya CHADEMA kwenye uchaguzi mkuu wa 2020 aliendelea kusema “leo [Sept 25] nimezungumza na [wakili wangu] Bob Amsterdam. Nimemwambia una mamlaka kamili ya kulianzisha. Kulianzisha dhidi ya Millicom, Tigo na dhidi ya Serikali ya Tanzania. Imani yangu tutawapata na namna ya kuwapata ni kushughulika nao kwenye hizo mahakama waliko, ambako Serikali ya Tanzania haiwezi ikapiga simu kwa jaji.”

Siku ya Oktoba 8, 2024 kupitia mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter) Lissu alituma ujumbe na picha ikimuonesha akiwa pamoja na mwanasheria wake Bob Amsterdam, lakini hakufafanua zaidi hatua wanazochukua kuanza kesi hiyo.

Hata hivyo, kampuni ya Tigo hapa Tanzania kwa sasa si sehemu ya kampuni ya mawasiliano ya Millicom tangu Aprili 2022 kwani kampuni hiyo iliiuzwa kwenda kwa kampuni ya Madagascar ya Axian Group ambayo kwa kushirikiana na mfanyabiashara maarufu hapa nchini, Rostam Aziz, waliinunua Tigo kwa dola za Kimarekani milioni 100 sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 233. 

Tigo yakanusha kuhusika

Katika taarifa yake kampuni ya Tigo ambayo sasa ipo chini ya Honora Tanzania Public Limited imejitoa kuhusika katika madai hayo kwa kusema kuwa haifahamu kinachoendelea katika kesi iliyofunguliwa London inayomuhusu aliyekuwa mmiliki wa zamani.

“Kampuni mama ya sasa ya Tigo haikuwa mmiliki wake wakati tukio lililoripotiwa likitokea” imesema taarifa hiyo.

Taarifa ya kampuni hiyo iliendelea kwa kuwahakikishia wateja wake kuwa itaendelea kulinda binafsi taarifa zao kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Haki ya Lissu kupatikana?

Katika mazingira hayo The Chanzo ilimtafuta Wakili Fulgance Massawe na kutaka kufahamu endapo Lissu ataweza kuwashtaki Tigo na kupata haki yake hivi sasa, ikiwa kampuni hiyo tayari inamilikiwa na kampuni nyingine ambayo haikuwepo wakati wa utoaji wa taarifa hizo. 

“Inategemea na ushahidi alionao wa kuonesha ushiriki wa hao wanahisa katika huo uvujishaji [wa taarifa] kwenye sera za hiyo kampuni. Je, ni kwa namna gani wamekuwa wakikaa na taarifa za watu pamoja na mambo mengine,” Massawe ambaye pia Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) anasema. 

Massawe anaendelea kueleza kuwa mpango wa Lissu wa kwenda kufungua kesi kwenye Mahakama za kimataifa utarahisisha mchakato wa kupatikana kwa haki yake kwani kwenye nchi kama Uingereza kuna sheria inayowajibisha makampuni yaliyosajiliwa kule au yameorodheshwa kwenye masoko yao na yakabainika kufanya makosa kwenye maeneo yanayofanya kazi. 

“Ina maana kama ushahidi wao utaonesha kwamba Millicom anahusika kwa njia yoyote ile ni rahisi kwenda kumshtaki kule Uingereza. Sasa uzuri, kwa wenzetu hawana hizo sheria tulizonazo Tanzania, kwa hiyo kulingana na ushahidi walionao na mambo mengine ni rahisi tu kwenda kumshtaki hata mmiliki yule wa zamani, muhimu tu wawe na ushahidi.” 

Mali na madeni

Wakili Jebra Kambole ameiambia The Chanzo kuwa mazingira mengine yanayoweza kumsaidia Lissu kupata haki ya ni kwamba pale mtu anaponunua kampuni hununua mali pamoja na madeni, na madeni moja wapo ni madai. Hivyo, katika mazingira hayo hata kama wamiliki wa Tigo ni wengine hivi sasa bado wanaweza kuwajibika kwa kuingilia taarifa zake wakati huo. 

“Huwezi ukasema kwamba nilinunua kampuni ina deni, au nilinunua kampuni ina mgogoro, au nilinunua kampuni ambayo ilinunua shamba fulani kinyume na sheria basi wewe usishtakiwe.” 

Kambole anaendelea kuzungumza “kama ulinunua kampuni ambayo ilifanya vitu ambavyo ni kinyume cha sheria na matendo yake yatakuwa ni miongoni mwa vitu ambavyo utawajibika navyo.” 

“Mimi naamini kwamba bado [Tigo] watawajibika kwa sababu hayo matendo yalifanywa na hiyo kampuni ambayo wao wameinunua. Huwezi kununua mazuri tu, na mabaya yake unanunua.” 

Kwa upande mwingine sio mara ya kwanza Lissu kuituhumu Serikali kuhusika katika njama za kushambuliwa na risasi, ambapo mara kadhaa Serikali imekuwa ikikanusha na kusisitiza kuwa uchunguzi unaendelea licha ya kukamishwa na masuala kadhaa waliyoyataja kwa kipindi tofauti.

Akiongea kupitia mtandao wa Club House Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni hapo Juni 4, 2023 katika mjadala uliondaliwa na Msemaji wa Serikali, alisema kuwa matumaini juu ya uchunguzi wa kesi ya Lissu yameongezeka kufuatia Lissu kuwepo nchini tofauti na hapo awali ambapo alikuwa nje ya nchi.

“Nitoe wito kwa muhusika mwenyewe pamoja na wengine, watakaoweza kusaidia suala hilo ili liweze kukamilika kwa haraka, hatimaye wahusika waweze kupatikana na kufikishwa katika mkondo wa sheria kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi,” amesema Masauni.

Siyo Lissu pekee

Lissu siyo Mtanzania pekee ambaye ameibuka kudai kuwa Serikali ya awamu ya tano ilihusika kufuatilia mawasiliano yake kupitia kuchukua taarifa kwenye mitandao ya simu, na kufanikiwa kumdhuru. Mtanzania mwingine aliyeibuka kudai hivyo ni Erick Kabendera ambaye yeye alikuwa ni mwandishi wa habari za uchunguzi. 

Kabendera anadai kuwa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom ilihusika kutoa taarifa zake kwa mamlaka, taarifa ambazo zilirahisisha mchakato wa yeye kutekwa mnamo Julai 27, 2019, alipokuwa nyumbani kwake maeneo ya Mbweni. 

Julai 2024 Kabendera alifungua kesi katika Mhakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam akiishtaki Vodacom kwa kuhusika na kutekwa kwake, na akiitaka imlipe bilioni 29 kama fidia ya madhira aliyopitia baada ya kutekwa.  

Septemba 2024 Mahakama ikaifuta kesi hiyo baada ya Vodacom kuweka pingamizi kuwa kesi hiyo imefunguliwa nje ya muda. Hata hivyo, Oktoba 1, 2024, Kabendera alitangaza kuwa ataukatia rufaa uamuzi huo kwa kuwa yeye na wanasheria wake wanaamini kuwa kesi yao ina mashiko na inastahili kusikilizwa ili waweze kuwasilisha ushahidi wao. 

Wakili aeleza kitakachompa ushindi Lissu 

Kwa mujibu wa Wakili Kassim Waititi, Lissu anaweza kupata ushindi kama atakuwa na vielelezo viwili ambavyo vitathibitisha kuwa kosa hilo lilitendeka. Kitu cha kwanza ni vielelezo vya kuthibitisha kuwa taarifa zake binasfi zilitolewa ridhaa yake, na cha pili ni suala la taarifa zake kutolewa kwa uzembe au kwa nia ovu. 

“Kama ataweza kuthibitisha kwamba moja kulikuwa na uzembe na uzembe huo umepelekea yeye kuathirika na kuteseka [basi] anathibitisha anakuwa na haki. Lakini pia, akithibitisha kama kulikuwa na nia ovu na kukawa na ushahidi ambao utakuwa dhahiri atapata haki yake.” 

“Mwisho kama anaona kwamba anaona kwamba taarifa zake, au haki ya ulinzi wa taarifa binasfi ilikiukwa na anahuo ushahidi anapata haki yake pasipokujali chochote. Msingi wa haya yote ni kuwa na vielelezo juu ya madai ambayo anayo huyo mwanasiasa,” Waititi aliieleza The Chanzo kwenye mazungumzo yaliyofanyika kwa njia ya simu. 

Modesta Mwambene ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mbeya. Anapatikana kupitia mwambemo@gmail.com  

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts