Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesitisha leseni za maudhui mtandaoni kwa chapa tatu za kampuni ya Mwananchi ikiwemo; The Citizen inayochapisha maudhui kwa kingereza, Mwananchi inayochapisha maudhui ya Kiswahili na Mwanaspoti inayochapisha maudhui ya michezo. Adhabu hii inakuja kufuatia video ya katuni iliyochapishwa na The Citizen katika kurasa zake za Instagram na X.
“Tarehe 01 Oktoba 2024, Mwananchi Communications Limited ilichapisha maudhui mjongeo na sauti (audio-visual content) kwenye mitandao yake ya kijamii, maudhui yaliyozuiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 16 ya Kanuni ya Maudhui Mtandaoni zilizorejewa hapo juu. Aidha, maudhui hayo yameleta tafsiri hasi kwa Taifa, jambo ambalo linaathiri na kuharibu umoja, amani na mshikamano wa kitaifa,” imeeleza taarifa rasmi ya TCRA kuhusu adhabu hiyo.
Adhabu hii inatolewa ikiwa ni siku moja toka gazeti la The Citizen kufuta video yake iliyotumia katuni kutoa ujumbe kuhusu matukio ya utekaji na watu kupotea Tanzania. The Citizen ilieleza kuwa iliamua kufuta video hiyo kutokana na kutafsiriwa isivyo sahihi.
“Tumeamua kuifuta video iliyochapishwa katika mitandao yetu ya X na Instagram mnamo Oktoba 1, 2024, video hiyo ilionesha matukio yaliyoibua wasiwasi kuhusu usalama na ulinzi wa watu Tanzania. Uamuzi wetu wa kuifuta video hiyo unatokana na video hiyo kutafsiriwa tofauti na makusudio halisi,” ilieleza The Citizen kwenye taarifa yake iliyosainiwa na Mhariri Mtendaji, Mpoki Thompson.
Video hiyo ilionesha katuni ya mtu mwenye mfanano na Rais Samia akiwa amekaa mbele ya luninga yake, mtu huyo kila alipokuwa akibadili luninga yake video zilizokuwa zikionekana zilihusu matukio ya utekaji na watu kupotea.
Video hiyo inaonekana kulandana na matukio halisi katika jamii, moja ya wahusika walionekana ni katuni iliyofanana na Edgar Mwakabela maarufu kama Sativa, aliyetekwa na kunusurika kuuwawa mnamo Juni 2024. Katika video hiyo maneno ambayo Mwakabela alitumia kwenye moja ya mahojiano yalitumika.
SOMA: Utata Kupotea Kwa Kiongozi Mwingine wa CHADEMA. Polisi Rukwa Wasema Hakuna Utekaji
Wahusika wengine wanaowasilishwa na katuni za video hiyo ni wanafamilia ambao wapendwa wao walipotea au kutekwa, huku sehemu kubwa matukio yaliyotumika yakiwa ni yale yaliyopatikana kwenye makala maalum ya The Chanzo kuhusu watu kutekwa au kupotea.
Watu hao walioonekana ni mfano mzee William Sije, ambapo sehemu ya maneno aliyoyaongea kwenye mahojiano yake ya mwisho aliyoyafanya na The Chanzo yaliweza kutumika kwenye video hiyo. Mtoto wa Mzee Sije, James Sije alikamwatwa na watu waliojitambulisha kuwa polisi mnamo Agosti 17, 2021, huko Mwanza, kijana huyo hakuonekana tena toka wakati huo.
Mzee Sije alifariki Agosti 17,2024, tarehe ambayo mtoto wake alipotea, ikiwa ni wiki tatu tu baada ya kuongea na The Chanzo.
Watu wengine waliowasilishwa kupitia katuni hiyo ni Pamoja Johari Songoro ambaye mume wake Lilenga Isaya Lilenga alipotea mnamo Mei 11, 2024. Pia Mzee Yusuph Chaula ambaye kijana wake Shadrack Chaula (24), alitekwa mnamo Agosti 02,2024, na mpaka leo hajaonekana. Huyu ndio yule kijana aliyejikuta matatani baada ya kuchoma picha ya Rais, na kusambaza video.
Mwingine aliyewasilishwa ni Zabibu Kassim Mwete mama ambaye kijana wake Issa Sango alipotea toka Januari 27,2023.
Adhabu hii kwa Mwananchi ni ya kipekee hasa kutokana na kuwa magazeti mengine ya kampuni hiyo ambayo hayakuchapisha habari hiyo pia yamefungiwa kuchapisha mitandaoni. Hii inajumuisha Mwananchi gazeti linalochapishwa maudhui ya Kiswahili mitandaoni na Mwanaspoti gazeti linalohusika na kuchapisha habari za michezo pekee.
Katika taarifa yake kuhusu kusitishwa kwa leseni zake, Kampuni ya Mwananchi imeahidi kuendelea kuwaletea wasomaji wake habari zake na maudhui bora yanayoliwezesha taifa kupitia nakala za kuchapisha za magazeti. Pia kampuni hiyo imeeleza kuwa inaendelea kuzungumza na Mamlaka ili kupata muafaka.