Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeeleza kuwa limefikia makubaliano na Serikali ya Tanzania yatakayowezesha utolewaji wa mkopo nafuu wa dola za Kimarekani milioni 265.78 sawa na takribani shilingi bilioni 720 kupitia utekelezaji wa program ya mikopo nafuu ya IMF ya Extended Credit Facility (ECF).
Programu ya Extended Credit Facility-(ECF) inahusu upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii. Mkopo huu hutolewa kwa nchi zinazoendelea na zenye changamoto ya urari wa biashara na malipo ya nje (Balance Of Payment).
Mkopo huu ambao unategemea kuidhinishwa na Bodi ya Utendaji ya IMF, utaifanya Tanzania kupokea jumla ya dola milioni 758.11 sawa na shilingi trilioni 2.1 kupitia programu ya ECF na dola 114.07 sawa shilingi bilioni 310 kutoka fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia Resilient and Sustainable Fund (RSF).
Haya yamejiri baada ya timu ya IMF ikiongozwa na Mkuu wa IMF Tanzania, Charalambos Tsangarides kukamilisha ziara yao ya siku 15 iliyoanza Oktoba 2, 2024, ambapo walikutana na maafisa wa Serikali ya Tanzania jijini Dar es Salaam na Dodoma kufanya mapitio ya nne ya programu ya ECF na mapitio ya kwanza ya programu ya RSF.
Katika taarifa yake, IMF imeeleza kuridhishwa na kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania pamoja na vipaumbele vya kisera katika kuimarisha sera za fedha, ukusanyaji mapato, udhibiti mfumuko wa bei, unyumbulifu wa viwango vya kubadilisha fedha na maboresho ya mifumo ya matumizi ya Serikali.
“Hali ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania inaendelea vizuri mwaka 2024 huku shughuli za kiuchumi zikikua kwa takriban asilimia 5.4 katika nusu ya kwanza ya 2024 baada ya ukuaji wa asilimia 5.1 mwaka 2023,” taarifa ya IMF imeeleza, “mfumuko wa bei mwezi Septemba uliendelea kuwa tulivu kwa asilimia 3.1, ndani ya lengo la Benki ya Tanzania.”
Hata hivyo taarifa hiyo ya IMF imeeleza pia changamoto zinazoweza kuathiri ukuaji huu wa uchumi wa Tanzania ni pamoja na athari za migogoro ya kikanda inayoendelea, kutokutabirika kwa bei za bidhaa, changamoto za fedha za kigeni zinazotarajiwa pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
2 responses
Okay.
Jumla tunakua tumekopa shilingi ngapi mpaka sasa ? Kwa mwaka huu?
Ninaomba mkopo wa shiling 50000