Inawezekana kwa miaka mingi ijayo wanafunzi na wanazuoni wataendelea kujifunza kuhusu ufanisi uliowezesha Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuweka historia ya kuwaandikisha Watanzania takribani wote katika zoezi la uandikishaji la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara hiyo takribani Watanzania 31,282,331 wamejiandikisha kupiga kura katika zoezi lililoanza Oktoba 11 mpaka Oktoba 20,2024. Kwa kulinganisha na takwimu za Sensa ilizofanyika mwaka 2022 ambapo zilionesha watu wenye umri wa miaka kumi na sita na kuendelea walikua 32,988,131, kitakwimu kama tukipunguza idadi ya vifo na wale ambao mpaka wakati wa uchaguzi bado watakua na miaka 17, basi kuna uwezekano mkubwa Wizara ya TAMISEMI imeweza kuwasajili Watanzania wote wenye sifa za kupiga kura.
Deus Kibamba ni mwanazuoni ambaye amekua mwangalizi wa zoezi hili toka lilipoanza, yeye kwa upande wake ameiambia The Chanzo anashangaa lakini pia amesema ni jambo la kushukuru namna takwimu zinavyoonekana.
“Kinachonishangaza sio wingi wa kujiandikisha mimi kwangu kinachonishangaza ni kasi iliyotumika kutoa majumuisho,” anaeleza Kibamba.
“Mimi ni mwangalizi wa uchaguzi, kwa hiyo nimetembelea vituo vingi katika mikoa kibao Tanzania, nikiwa naangalia mwenendo wa uandikishaji huko nikakuta uandikishaji ulikua unafanyika very manual,[bila kutumia teknologia]. Nikadhani itachukua kama siku nne kwa Waziri, Wizara yenyewe kukusanya hizo takwimu, watu wahesabu halafu watume Wizara izijumuishe ndipo takwimu zimfikie Waziri,” anaeleza Kibamba mdau mwenye uzoefu wa kuangalia chaguzi ndani na nje ya Afrika.
Waziri Mchengerwa alipoulizwa kuhusu namna wanavyopata takwimu huku uandikishaji ukifanyika bila kutumia teknologia alieleza ni kutokana na uwepo wa maofisa wa Wizara hiyo kila kona.
“Tulijipanga vizuri kuhakikisha kwamba maofisa wetu wapo katika kila ngazi, kuanzia ngazi ya chini kabisa kwenye vitongoji kwenye vijiji kote kuna maafisa ambao wamefanya kazi kubwa kuhakikisha kila siku tunakua na takwimu, kila siku ambapo tunakamilisha utekelezaji wa uandikishaji tunakua na takwimu,” alifafanua Mchengerwa alipoongea na waandishi wa habari jana Oktoba 21,2024.
Baadhi ya mikoa iliyoongoza katika uandikishaji ni pamoja na Pwani, Tanga, Mwanza na Dodoma.
Msemaji wa Chama cha Mapinduzi, Amos Makalla anaeleza kuwa mwitikio ulionekana katika Takwimu za TAMISEMI ni kwa sababu ya kukubalika na maendeleo ambayo chama hicho kimeleta.
“Mwitikio huu wa kujiandikisha kwa kiasi kikubwa umetokana na moja kukubalika kwa Serikali ya CCM na hasa utekelezaji wa ilani, anaeleza Makala alipoongea na waandishi wa habari leo, “zoezi hili limefanikiwa kwa sababu wananchi wanakubali utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.”
Baadhi ya maeneo yenye watu wengi kama Dar es Salaam zoezi hili linaonekana kupekua kila kona. Kwa kutumia takwimu za Sensa kwa Dar es Salaam ni watu 115,274 pekee ambao hawajajiandikisha kupiga kura Serikali za Mitaa, huku kwa Jiji la Dodoma na Mwanza idadi ikipitiliza hata ile ya idadi rasmi ya watu kwa mujibu wa takwimu za Sensa ambazo huchukua muda mrefu kubadilika.
Mwanaharakati Ananilea Nkya ambaye ni mmoja ya watu waliofungua kesi ya kupinga TAMISEMI kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa yeye anaonesha kutokuziamini takwimu hizo.
“Nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kwamba Watanzania milioni 31 wenye umri wa kuanzia miaka 18 wamejiandikisha kupiga kura uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu 2024,” anaeleza Nkya.
“Sababu ya kutokuamini kuwa watu milioni 31 wameandikishwa ni chombo kinachoendesha na kuratibu uchaguzi huo, kwa vile Waziri wa TAMISEMI ana maslahi na uchaguzi huo, kwa vile chama chake CCM kinagombea uchaguzi huo na kwa hiyo akiwa kama msimamizi Mkuu wa TAMISEMI anaweza kufanya udanganyifu wowote kwa faida ya chama chake,” anaeleza zaidi Nkya
SOMA ZAIDI: Je, Uchaguzi Serikali za Mitaa 2024 Utaongeza Wanawake Wenyeviti wa Vijiji?
Nkya anatolea mifano ya malalamiko ya watoto wenye umri chini ya miaka 18 kujiandikisha. Mpaka hivi leo Oktoba 22, 2024, video mbalimbali zimeendelea kusambaa mitandaoni, huku moja ya video inayoendelea kuzua gumzo ni ile ya wanafunzi wa kidato cha kwanza wakishangaa kuona majina yao katika mabandiko ya usajili.
Waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa alilitolea ufafanuzi suala hili na kueleza kuwa hakukua na ushahidi wowote kuwa kulikua na uandikishaji wa watu wenye umri chini ya miaka kumi na nane.
“Tunasikia kwenye mitandao ya kijamii, lakini hakuna popote ambapo kijana wa chini ya miaka kumi na nane ameandikishwa nchini Tanzania,” alisema Mchengerwa.
Mchengerwa alifafanua zaidi kuwa uwepo wa mawakala unafanya uchaguzi huo uwe wazi na uhuru.
“Niseme tu mchakato umekuwa wazi na uhuru kwa sababu kila kituo ambacho pengine mtu anaweza akakilalamikia kina mawakala wa vyama vyote. Sasa jukumu la nani aweke wakala wapi, hilo sio la kwetu, kama kuna sehemu kuna changamoto zimeibuka mawakala wa eneo husika wanaweza kutuambia,” alisisitiza Mchengerwa.
SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Katiba Yatajwa Kuwa Suluhu ya Uchaguzi Huru na wa Haki
Thomas Kibwana ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa kwa upande wake anaeleza kuwa idadi kubwa ya watu kujisajili inatokana pia na ongezeko la watu wenye sifa Tanzania.
“Kuna ongezeko kubwa la vijana ambao mwaka 2019 hawakuwa na vigezo vya kupiga kura ila kwa sasa wana vigezo,” anaeleza Kibwana
“Kuna baadhi ya watu waliojitokeza kudai kwamba takwimu hizo zimepikwa, inabidi tutambue kwamba kila siku tunahamasisha watu kupiga kura, inashangaza watu wanapokuwa wengi tunalalamikia kuwa takwimu zimepikwa, kikubwa ni kuwa orodha ya waliojiandikisha itawekwa hadharani,” anaongeza Kibwana.
2 responses
Figures don’t lie. Sensa 52% yetu ni vijana, walio jiandikisha ni karibu 50% ya sisi wote. Kuorodhesha watu mln31 kwa siku 10 kwa kutumia nyenzo duni ya kalamu na karatasi, kukosa hamasa (Mhe Utouh), hadi kuhonga Nyama, kukamatwa walio ripoti kugushi majina, hiyo 31mln unaipataje
My tweet on 21/10. I believe these figures by Mhe @mchengerwa were doctored
Kwa mwendo huu kama malalamiko hayatasikilizwa basi vyama vyote vya upinzani visusie uchaguzi