The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mashabiki Taifa Stars Watoke Wapi?

subscribe to our newsletter!

Kabla, wakati na baada ya timu ya taifa ya soka kucheza mechi ya michuano ya awali ya kuwania tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika, Afcon 2025, kulizuka mjadala kuhusu kupungua kwa hamasa ya Watanzania kuipenda timu yao.

Mjadala huo uliegemea kwenye hoja kwamba katika siku za karibuni Taifa Stars haipati mashabiki wengi inapocheza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na shutuma zikaenda kwa idara ya habari na mawasiliano kuwa haifanyi kazi yake vizuri.

Kibaya zaidi, hoja nyingine kubwa ikawa ni kutofanya vizuri kwa Taifa Stars inapocheza nyumbani, yaani kwenye Uwanja wa Mkapa tofauti na inapocheza ugenini. Kulikuwa na hoja kidogo hapo, angalau kwa wakati huu, kutokana na ukweli kwamba Stars ilitoka suluhu na Ethiopia kwenye Uwanja wa Mkapa na ikafungwa mabao 2-0 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo uwanjani hapo.

Lakini Stars ndiyo iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Zambia jijini Lusaka na baadaye kushinda kwa mabao 2-1 dhidi ya Guinea katika mechi ambayo iliyochezwa Ivory Coast kutokana na Guinea kutokuwa na uwanja unaofikia viwango vilivyowekwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) na lile la kimataifa (Fifa).

Ni kweli. Pamoja na umuhimu wa mechi ya Congo katika mechi ya kundi letu la Afcon 2025, haoikuonekna hamasa ya Watanzania kwenda kuishuhudia timu yao Uwanja wa Mkapa Zaidi ya wale walioisubiri kuiona kwenye runinga. 

Kwenye baa, migahawa na vibanda vya kuonyesha mechi, maarufu kama vibanda umiza, watu walijaa mapema kusubiri mechi hiyo dhidi ya Wacongio ambao walishakusanya pointi zote tisa katika mechi tatu za kwanza.

SOMA ZAIDI: Tumeacha Mapinduzi Kwenye Klabu, Sasa Tunayumbisha Seckretarieti

Tanzania ilikuwa inahitaji ushindi katika mchezo huo ili ifikishe pointi saba na hivyo kujisweka katika nafasi nzuri dhidi ya Guinea katika safari ya kuelekea Morocco kwenye fainali hizo.

Na zaidi ya yote, mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele alikuwa mmoja wa wachezaji wa Congio waliokuja jijini Dar es salaam kwa ajili ya mechi hiyo baada ya kufanya vizuri akiwa na Pyramids kwenye Ligi Kuu ya Misri.

Mazingira hayo yalitosha kuweka hamasa kubwa kwa mashabiki kwenda uwanjani kushuhudia timu yao ikisaka pointi tatu muhimu kwa hali na mali. Mbali na mazingira hayo, uzalendo wa kwenda kuipa nguvu timu iliyo katika nafasi nzuri ya kujirahisishia mazingira ya kufuzu, ungesababisha watu wengi wajitose kwenda kuishangilia kwa nguvu Stars iweze kufuzu.

Lakini hali ilikuwa tofauti kwenye Uwanja wa Mkapa. Mashabiki hawakuweza kuujaza uwanja unaoweza kuchukua watu 60,000. Kulikuwa na mapengo mengi uwanjani ambayo huenda yaliipa nguvu Congo kucheza watakavyo kwa kuwa hawakujiona kama wako ugenini. Ukichanganya na jumuiya ya Wacongo waishio Tanzania, ni Dhahiri timu yao ya taifa ilijihisi kuwa ni kama inacheza kwenye moja ya miji ya Congo DR.

Kitendo cha ofisa habari wa Shirikisho la Soka (TFF) kuonekana na kipaza sauti kinachotumiwa na wafanyabiashara ndogondogo kuuza bidhaa zao, akijaribu kushawishi mashabiki kuingia kwa wingi uwanjani, kiliwafanya wachambuzi wamjadili sana mtendaji huo wa TFF. 

Kwa mechi ya Taifa Stars inayohusisha Watanzania kutoka kila kona ya nchi, kipaza sauti kile hakikuwa chombo sahihi kuhamasisha mashabiki kujitokeza uwanja.

Ni kweli. Pengine hata idara hiyo kutokuwa na mkakati sahihi wa uhamasishaji, pia inaweza kuwa tatizo jingine. Lakini TFF kama taasisi ilikuwa na mpango gani zaidi ya kutegemea kile kilicho mezaji mwa idara ya habari na mawasiliano.

SOMA ZAIDI: Serikali Ianze Kutoa Ruzuku kwa Vyama Teule vya Michezo 

Siku hiyo mchana niliona video inayoonyesha kuwa kulikuwa na mechi za ligi ya wanawake zikiendelea kama kawaida. Maana yake, TFF ilishagawanya mashabiki; wale wanaofuatilia ligi nzuri ya wanawake, dhidi ya wale wanaofuatilia timu ya taifa.

Sijajua vizuri kuhusu Championship au ligi daraja la kwanza na mashindano mengine.

Ninachojua, kitu cha kwanza wakati timu ya taifa inapocheza; iwe ugenini au nyumbani, shughuli zote za mpira wa miguu zinasimama kuwapa nafasi wananchi kufuatilia timu yao bila ya vikwazo vyovyote. Yaani, huwezi kuruhusu mechi ya kirafiki au ya mashindano ichezwe Uwanja wa KMC Mwenge, wakati siku hiyo Taifa Stars inacheza na Congo DR au Guinea.

Ni dhambi kubwa hata kama muda wa kuanza mechi moja na nyingine ni tofauti sana. Ni lazima shughuli zote za soka zisimame siku hiyo, na ikiwezekana katika zile siku zote nne za maandalizi na mechi zilizowekwa na FIFA.

Hapa ndipo mashabiki watakapoweza kupanga mipango yao vizuri na kuipa nafasi Taifa Stars kwenye program zao. Nililiona hili wakati Tanzania ilipokuwa mwenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana walio na umri chini ya miaka 17.

Huku timu ya taifa inacheza, huku Simba, Yanga na nyingine zinacheza mechi za kirafiki. Ni dhahiri kuwa kwa utamaduni wetu, hakuna ambaye angeifuatilia timu ya vijana akaachana na mechi za kirafiki za vigogo hao.

Kwa hiyo, TFF kama taasisi haina budi kuhakikisha inakuwa na mkakati wa kujenga akili za Watanzania kuipa kipaumbele timu yao ya taifa kila inapocheza. Na inawezekana ikiwa tu, mashindano yote na mechi za kirafiki zitasimama katika kipindi cha kuelekea mechi ya taifa na wakati wa mechi hiyo ili akili za wananchi wote zielekezwe kwanza kwenye timu yao ya taifa.

SOMA ZAIDI: Tufuatilie Sakata la Man City kwa Makini Tukijitathmini 

TFF na idara yake ya habari si wa kulaumiwa pekee. Hivi sasa vyombo vya habari vinaona habari kubwa ya michezo ni lazima ihusishe Simba  na Yanga. Hata Gibri Silla wa Azam FC akifunga bao safi, ni lazima litahusishwa au kulinganishwa na bao lililofungwa na mchezaji wa Yanga au Simba ili habari ionekane nzuri.

Hata kabla, wakati na baada ya mechi dhidi ya Congo DR, uchambuzi na habari nzuri kuhusu Taifa Stars ulihusishwa na mambo yaliyokuwa yanaendelea katika maandalizi ya mechi ya watani hao wa jadi.

Pengine kwa kujitambua au kutojitambua, vyombo vya habari, hasa redio na magazeti, zilijikita kutangaza mechi ya Simba na Yanga licha ya ukweli kwamba Taifa Stars ilikuwa na mechi ngumu na muhimu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kwa namna moja au nyingine, vyombo vya habari vilihusika kuondoa akili ya Watanzania katika mechi inayoliunganisha taifa na kujikita zaidi kwenye mechi ambayo vyombo hivyo vilidhani kuwa ndiyo inawapatia wasomaji, wasikilizaji na watazamaji wengi au ndiyo ingeweza kuwafanya wachambuzi waonekane wanajua sana mpira wa miguu.

Katika mazingira hayo, mashabiki wa kujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa wangetoka wapi kama vyombo vya mawasiliano havikuiona umuhimu wa mchezo huo?

Lawama nyingine haina budi kuwa kwa shirikisho lenyewe. TFF haijaweka mazingira mazuri ya kuifanya Taifa Stars ifuatiliwe kwa karibu na mashabiki au Watanzania. 

Wakati mwingine hamasa ya mnashabiki hutokana na mtu au watu walio kwenye benchi la ufundi. Hawa watu wanakubalika kiasi cha shabiki kuacha shughuli zake na kwenda kuangalia walichoandaliwa?

Tangu kutimuliwa kwa kocha Mualgeria, Adel Amroucheza wakati wa fainali zilizopitra za Afcon, TFF haijatoa taarifa rasmi kuhusu mbadala wake. Na Hemed Morocco ameendelea kutambulishwa kama kocha wa muda. Niliwahi kusikia kiongozi wa TFF akisema mpango wao kwa sasa ni kuwapa makocha wazawa nafasi zaidi, lakini kwa nini basi isiwekwe bayana kwa wananchi ili wajue kuwa sasa ni mwendo wa wazawa pekee na kuamua wanachokijua?

SOMA ZAIDI: Sakata la Lawi, Kagoma ni Utapeli Katika Soka

Inaweza kuwa ni mkosi, lakini ni dhahiri kuwa  matokeo ya Taifa Stars bado hayajaweza kushitua Watanzania wengi na bado wanamponda kila timu inapofanya vibaya. Ongezeko la makocbha wazawa kwenye benchi la ufundi  pia halikufanyikja kimkakati aaidi ya watu kushituka walipowaona siku ya mechi ya Ethiopia.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo ni lazima yafanyike kimkakati na kwa hadhi ya timu ya taifa ili wananchi waone kuwa ni mali yao na wahoji kila wanaloona ni kosa na hivyo kuwa sehemu ya timu.

Kutowajali mashabiki katika kila kinachofanyika kwenye timu, hurudisha ari nyuma na hivyo si ajabu kuona uwanja ukiwa mtupu siku ambayo Taifa Stars inacheza.

Kwa hiyo, ni muhimu sana kwa TFF kutafakari vitu vyote kwa ujumla na kutafuta mkakati bora wa kuirudisha timu ya taifa kwa Watanzania ili wawe na uchungu nayo n a hivyo waone wana wajibu wa kujitokeza uwanjani kila inapocheza, iwe nyumbani au ugenini. Propaganda za vyombo vya habari pekee hazitoshi kuwezesha kuteka nyoyo za mashabiki.  

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts