Malengo ya elimu kwa mtoto yanategemea sana ushirikiano baina ya walimu na wazazi. Katika suala zima la elimu ya mtoto, wazazi na walimu tunapaswa kushirikiana ili kufikia lengo kuu, ambalo ni kuona watoto wanajifunza kwa ufanisi na kufanya vizuri katika masomo yao na katika maisha yao ya baadae.
Licha ya kuwa na lengo hili bado kuna changamoto za hapa na pale katika kujenga ushirikiano kati ya wazazi na walimu. Tafiti zinaonesha kuwa mawasiliano na ushirikiano imara kati ya wazazi na walimu huathiri moja kwa moja utendaji wa mtoto kitaaluma na kitabia.
Mazingira ya nyumbani na shuleni ndiyo yanayoongoza maisha ya mtoto kwa nafasi kubwa. Mazingira haya mawili yanapofanya kazi pamoja, mtoto anapata faida nyingi kwa njia tofauti. Tafiti zinaonesha kuwa wanafunzi ambao wazazi wao wanahusishwa kikamilifu katika elimu yao huwa na alama za juu, mahudhurio bora, na huwa na stadi bora za kijamii.
Pili, watoto huwa na mabadiliko chanya ya tabia. Watoto ambao wazazi wao wanajenga na kudumisha mawasiliano mazuri na thabiti na walimu wao huwa na uwezekano mdogo wa kuwa na matatizo ya kitabia.
Jambo la tatu ni ukuaji wa kihisia na kijamii. Mahusiano ya ushirikiano kati ya wazazi na walimu huwasaidia watoto kujenga hisia za usalama, wakijua kuwa wale watu wazima muhimu katika maisha yao wamejipanga kuwasaidia katika ukuaji wao pale watakapopitia changamoto zozote shuleni na nyumbani.
SOMA ZAIDI: Fikra za Watoto Juu ya Ukuaji Wao
Je, wazazi tunawezaje kushirikiana vyema na walimu ili kutengeneza mazingira yatakayowawezesha watoto wetu kujifunza vizuri?
Kujenga ushirikiano mzuri kati ya wazazi na walimu si jambo linaloweza kufanyika mara moja—huhitaji jitihada, mawasiliano ya wazi, na kuheshimiana. Wazazi tunaweza kufuata mbinu kadhaa kufanikisha hili.
Tunaweza kuanza kwa kuanzisha mawasiliano ya wazi mapema, tusisubiri mikutano ya wazazi na walimu, au changamoto za kitaaluma, kutokea. Tuanze kujenga uhusiano na walimu wa watoto wetu mwanzoni mwa mwaka wa masomo pale tu tunapokwenda kuwaandikisha, kuwasajili, shuleni.
Kisha, tuwe tunafuatilia na kujadliana mara kwa mara maendeleo ya mtoto na changamoto zozote pamoja na mafanikio yote ya mtoto. Pia, tujitahidi kuonesha nia ya kutaka kuwasaidia watoto wetu katika safari yao ya elimu.
Tushiriki moja kwa moja katika masuala ya mtoto shuleni, mfano, kuhudhuria hafla za shule, kujitolea kwa hali au mali inapowezekana, na kuonyesha nia ya dhati ya kutaka kufahamu maisha ya kitaaluma ya watoto wetu. Hii haitatusaidia tu kuwa na taarifa za watoto, lakini pia inawaonesha watoto wetu kuwa elimu ni kipaumbele.
SOMA ZAIDI: Fahamu Namna ya Upangaji wa Ratiba kwa Makuzi Bora ya Mtoto
Tujitahidi kuheshimu mchango na mawazo ya walimu. Tupende, tusipende, walimu wanautaalamu wa kipekee wa kutoa muongozo, au ushauri, kama jinsi sisi wazazi tuna utaalamu wetu wa malezi.
Sisi tunawafahamu watoto wetu vizuri, lakini walimu wanaleta maarifa ya kitaalamu juu ya mikakati ya kielimu na mienendo ya watoto darasani. Tukiwachukulia walimu kama wasaidizi badala ya wapinzani, tutaimarisha ushirikiano wetu.
Ikiwa changamoto imetokea tuwakabili walimu kwa mtazamo wa kushirikiana badala ya kugombana nao. Kulingana na aina ya changamoto, tunaweza kutoa maoni yetu kwa heshima na kuuliza mtazamo wao pia. Kwa pamoja, tunaweza kubuni mikakati ya kushughulikia changamoto hizo kwa ufanisi.
Tunaelewa kuwa kuna muda ratiba na shuguli zetu zinatubana na kufanya mawasiliano ya mara kwa mara kuwa magumu. Ila tunaweza kujitahidi kutumia simu, au barua pepe, kuzungumza, au kutuma jumbe fupi, kurahisisha mawasiliano kati yetu na walimu wa watoto wetu.
Na kuna wakati mwingine wazazi huwa tunakuwa na wasiwasi kuhusu kuzungumza na walimu, tukihofia kuhukumiwa, au kutokuwa na uhakika wa jinsi ya kutimiza mahitaji ya kielimu ya watoto wetu. Lakini inatubidi kujenga ujasiri na kuwa na mazungumzo ya wazi na walimu na hata uongozi wa shule kuhusu changamoto hizo.
Ili watoto wetu waweze kufanya vizuri katika safari yao ya elimu, hatuna budi bali kushirikiana na kujenga mahusiano mema na walimu wao.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.