Kwa sasa, Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) linahaha kuokoa mashindano yake ya Klabu Bingwa ya Dunia yaliyopangwa kufanyika mwakani nchini Marekani kutokana na Shirikisho la Wanasoka wa Kulipwa (FIFPRO) kufungua shauri Kamisheni ya Ulaya kupinga ongezeko la idadi ya mechi katika kalenda ya FIFA.
Shauri hilo linahusu kalenda ya michuano ya kimataifa kwa wanaume, hasa fainali zijazo za Kombe la Dunia na maamuzi kuhusu michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia itakayofanyika mwakani nchini Marekani.
FIFPRO imefungua shauri hilo kwa kushirikiana na Ligi za Ulaya, ikiwakilisha Chama cha Wachezaji wa Ulaya ambazo bodi zake zilifikia uamuzi wa kuchukua hatua za kisheria mwezi Julai mwaka huu wa 2024.
Katika shauri hilo, walalamikaji wanadai kuwa ongezeko la idadi ya mechi linalotokana na fainali za Kombe la Dunia kuongeza idadi ya timu kutoka 32 za sasa hadi 48, wakati Klabu Bingwa ya Dunia itakuwa na timu 32 kutoka nane za sasa, litaathiri usalama wa wachezaji, afya yao na kuweza kupunguza muda wa kusakata soka kwa kuwa watachoka upesi.
Ligi nazo hazikubaliani na mpango huo wa kuongeza idadi ya mechi za kimataifa, zikisema utaua mashindano ya kitaifa ndani ya nchi kwa kuwa yataathirika kiuchumi na uimara.
SOMA ZAIDI: Mashabiki Taifa Stars Watoke Wapi?
Walalamikaji waliwaambia waandishi wakati wa kutangaza kuwasilisha shauri lao kuwa FIFA imeonyesha kubeba majukumu yanayojikanganya kwa kuwa ndiyo taasisi inayoongoza mpira, lakini pia inataka kuwa muaandaaji wa mashindano, jambo linalosababisha igongane na ligi za taifa za nchi wanachama.
Wote kwa pamoja wanasema katika kufikia uamuzi wa kupanua mashindano yake, FIFA haikuwa na mchakato mzuri na ambao ni shirikishi kwa wadau ambao ni wachezaji na ligi za nchi na badala yake imetumia nguvu zake za kisheria kuendeleza maslahi yake kiuchumi kwa kudhoofisha wadau wake. Kwa hiyo, imetumia vibaya madaraka yake.
Kuona mbali
Wenzetu wameona mbali na wameajiri watu ambao wanaweza kutafsiri kwa haraka—kiuchumi, kijamii na kisiasa—uamuzi unaotangazwa kuhusu kuboresha, kupanua mashindano, au kupunguza, na hivyo kujua wadau wao wana nafasi gani katika uamuzi huo.
Na kwa sababu mpira ni uchumi na ajira, vyombo hivyo vinajua wapi pa kuipata haki yao, ndiyo maana haviendi tena FIFA kulalamika, bali kwenye mahakama za Umoja wa Ulaya, zenye divisheni maalum kwa ajili ya shughuli za mikataba, ajira, biashara, ushindani na mengineyo.
Hapa kwetu Tanzania, kuliona hilo inachukua muda sana, labda rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Fabrice Motsepe, atamke halafu huku tuitikie kama kibwagizo bila ya kujua kina maana gani.
SOMA ZAIDI: Tumeacha Mapinduzi Kwenye Klabu, Sasa Tunayumbisha Seckretarieti
Na kwa kuwa uamuzi huo wa kupanua mashindano unahusu kuongeza nafasi za wawakilishi wa Afrika kwenye Kombe la Dunia kutoka watano hadi tisa, ni vigumu kupinga hilo kwa sababu kila kiongozi anaona uwezekano wa nchi yake kwenda Kombe la Dunia unaongezeka, hivyo kuna siku ataweza kuwa kiongozi wa kwanza kuipeleka nchi yake kwenye fainali hizo kubwa duniani.
Na kwa kuwa fainali za Klabu Bingwa ya Dunia zimeongeza idadi ya timu na kufuzu kwake si kwa kupambana uwanjani msimu huo bali kwa takwimu za muda mrefu, basi hapo Usimba na Uyanga unaingia na malalamiko yanageuzwa kuwa ni wivu.
Athari zaonekana
Lakini kwa anayeona mbali, athari zimeanza kuonekana kwa angalau kidogo. Ligi Kuu ya Afrika Kusini nusura iizuie Mamelodi Sundowns kucheza mashindano mapya ya Ligi ya Mpira wa Miguu ya Afrika (AFL) baada ya CAF kuchelewa kuitaarifu. Ligi hiyo ilidai kuwa ilishapanga ratiba zake mapema na hivyo haitaweza kuibadilishia Sundowns mechi zake.
Baadaye, iliiruhusu na Sundowns wakawa mabingwa wa kwanza.
Kwa muda sasa, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, amekuwa akilalamikia uwingi wa mechi za ligi ndani ya muda mfupi na katika nchi ambayo ni kubwa kijiografia.
Baada ya mechi dhidi ya Coastal iliyofanyika Arusha, Gamondi alielezea jinsi alivyolazimika kusafiri kwenda sehemu tofauti ndani ya siku chache, akianzia kulazimika kwenda Zanzibar kucheza na Simba, baadaye kurudi Dar kucheza na JKT, halafu kwenda Arusha kucheza na Coastal na kurudi Dar kucheza na Azam, safari zilizofanyika ndani ya siku mbili kila moja.
SOMA ZAIDI: Serikali Ianze Kutoa Ruzuku kwa Vyama Teule vya Michezo
Na hiyo ni Yanga, ambayo, kama ilivyo kwa Simba na Azam, inaweza kutumia ndege kwenda umbali mrefu kama Mbeya, Arusha au Kagera, na hivyo kuweza kucheza mechi mikoa tofauti ndani ya muda mfupi.
Vipi hapo itakapofika mashindano hayo kuanza kuchezwa, maana yake ni kwamba ili kuyapisha, ligi zitakuwa zinalazimika kusimamasimama na hivyo kuwa na muda wa siku chache kucheza mechi za klabu za mashindano ya ndani.
Ndani ya hizo siku chache, timu zitalazimika kusafiri mikoa tofauti kucheza mechi, hali itakayokuwa si nzuri kiafya kwa wachezaji, na hali kadhalika si nzuri kiuchumi kwa kuwa wadhhamini hawatakuwa wakipata thamani ya fedha wanazotumbukiza kwenye mpira wa miguu.
Ushirikiano
Jambo kama hili linahitaji ushirikiano wa klabu katika kupaza sauti kutetea maslahi yao. Lakini ushabiki ukizidi, mambo ya msingi hayaonekani na hali ya ligi zetu itakuwa ngumu hadi kupoteza mvuto.
Umoja wa klabu unahitaji sauti moja ya Simba na Yanga na si kebehi na kejeli dhidi ya kila mmoja. Ukiangalia maamuzi mabovu yanayoendelea sasa hivi, huoni kama yanawakera Simba na Yanga, na kama ni jambo linalohitaji kukemewa na kuchukuliwa hatua sahihi.
SOMA ZAIDI: Tufuatilie Sakata la Man City kwa Makini Tukijitathmini
Badala ya kuona tatizo la uamuzi mbovu, kiongozi anaona kuna njama za refa kuinyima haki timu yake wakati katika mchezo huohuo, refa alifanya makossa mengi yaliyoinufaisha pia timu yake. Katika mazingira hayo, Simba na Yanga haziwezi kuwa na sauti moja kukemea uamuzi mbovu unaoendelea kuonakana hivi sasa, hasa baada ya mechi kuanza kuonyeshwa moja kwa moja na televisheni.
Upangaji wa ratiba unaobadilikabadilika unatakiwa usemwe kwa sauti moja.
Ili mpira wa miguu uwe na manufaa kwa klabu na wachezaji, ni muhimu sana Simba na Yanga wakaona umuhimu huu wa kuwa na sauti moja katika mambo ya msingi kama Real Madrid walivyokuwa kitu kimoja katika suala la Super League ya Ulaya na kupingana na klabu za Hispania kuizuia kampuni ya Kimarekani asilimia 10 ya haki za matangazo ya televisheni kwa miaka kumi.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.