Benki kuu ya tanzania imeutangazia umma wa Watanzania mabadiliko ya umiliki na majina mapya ya benki mbalimbali hapa nchini huku mabadiliko hayo yakitangazwa kuwa yameanza kufanyiwa kazi tangu Aprili mwaka huu kwa baadhi ya benki.
Katika taarifa iliyotolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, alibainisha kuwa mabadiliko haya yanakuja kufuatia hatua za kibiashara, muunganiko, na ununuzi wa hisa zilizofanyika kati ya benki hizo na taasisi nyingine za kifedha.
Katika mabadiliko hayo imeelezwa kuwa Benki Kuu ya Tanzania imeridhia ununuzi wa asilimia tisini na sita ya hisa za African Banking Corporation Tanzania Limited na Access Bank (Nigeria) Plc. Hivyo baada ya ununuzi huo, benki kuu ya Tanzania imeutangazia umma kuwa umiliki wa benki hiyo iliyokuwa inatambulika kama African Banking Corporation Tanzania Limited umebadilika.
“Kutokana na mabadiliko hayo, Benki Kuu ya Tanzania imetoa leseni ya biashara ya kibenki kwa jina jipya la Access Bank Tanzania Limited kuanzia tarehe 19 Septemba 2024” inasomeka taarifa hiyo rasmi kutoka benki kuu.
Ikumbukwe tu kuwa African Banking Corporation Tanzania Limited (BancABC Tanzania), ilianzishwa kama sehemu ya BancABC, huku ikianza shughuli zake nchini Tanzania mwaka 1996. BancABC awali ilikuwa chini ya usimamizi wa Atlas Mara, ambayo likuwa kifanya kazi katika nchi kadhaa za Afrika. Mwaka 2023, Access Bank yenye makao makuu nchini Nigeria ilinunua asilimia 96 ya hisa za BancABC Tanzania, hatua iliyosababisha mabadiliko makubwa katika umiliki wa benki hiyo.
Kufuatia ununuzi huu, BancABC Tanzania ilibadilishwa jina na kuwa Access Bank Tanzania Limited. Kubadilishwa kwa jina na mabadiliko ya umiliki yalipata idhini rasmi kutoka Benki Kuu ya Tanzania mwezi Septemba 2024, hivyo kuruhusu Access Bank Tanzania Limited kuendelea kufanya kazi kama benki ya kibiashara ndani ya nchi.
Aidha katika taarifa yake nyingine imeelezwa kuwa, Benki Kuu imeidhinisha mabadiliko ya Access Microfinance Bank (Tanzania) Limited, ambapo benki hiyo imenunuliwa kwa asilimia sitini na tano na kampuni ya Selcom Paytech Limited. Kutokana na mabadiliko haya ya umiliki, Access Microfinance Bank sasa imebadilisha jina na kuitwa Selcom Microfinance Bank Tanzania Limited.
Benki Kuu imeipa benki hii mpya leseni ya biashara ya benki ndogo za kibiashara(microfinance), inayoiwezesha kutoa huduma za kifedha kwa watu wa kipato cha chini na wafanyabiashara wadogo katika mikoa mbalimbali nchini.
Leseni hii mpya ilianza kutumika tarehe 22 Aprili 2024, na benki hiyo sasa inalenga kutumia teknolojia ya kisasa inayotolewa na Selcom Paytech Limited ili kufikia wateja wengi zaidi, hususan wale walioko katika maeneo yasiyofikiwa kwa urahisi na huduma za kibenki.
Kabla ya mabadiliko haya, Access Microfinance Bank Tanzania Limited (AMBT) ilianza shughuli zake Tanzania mwaka 2007 ikiwa tawi la Access Microfinance Holding AG, kwa lengo la kutoa huduma za kifedha hasa kwa jamii zisizo na huduma, ikijumuisha biashara ndogo na watu binafsi katika maeneo yasiyofikika kirahisi na huduma za benki. AMBT ilijikita katika kutoa mikopo na urahisi wa kifedha hasa kwa biashara ndogo na za kati.
Mwaka 2023, AMBT ilipitia mabadiliko makubwa wakati kampuni ya teknolojia ya kifedha ya Tanzania, Selcom Paytech Limited, iliponunua asilimia 65 ya hisa za benki hiyo. Selcom, kampuni inayomilikiwa na watanzania na iliyoanzishwa mwaka 2001, imekua kutoka kutoa huduma za muda wa maongezi wa awali hadi kuwa na huduma kamili za kifedha, ikijumuisha malipo ya simu, huduma za benki za uwakala, na mifumo ya miamala isiyo na fedha taslimu kwa biashara na wateja kote Tanzania. Ununuzi huu unaendana na dhamira ya Selcom ya kukuza huduma za kifedha za kidijitali na kufanya miamala isiyo ya fedha taslimu kuwa rahisi zaidi, hasa kwenye biashara ndogo na maeneo ya vijijini.
Katika hatua nyingine muhimu, Benki Kuu imeidhinisha muunganiko wa benki za jamii mbili, Kilimanjaro Co-operative Bank Limited na Tandahimba Co-operative Bank Limited na kupewa leseni rasmi ya kufanya kazi kama benki rasmi nchini Tanzania.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 30(1)(a) cha Sheria ya Taasisi za Kibenki na Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ya Tanzania imeidhinisha muunganiko wa benki mbili za jamii, yaani Kilimanjaro Co-operative Bank Limited na Tandahimba Co-operative Bank Limited, kuunda benki ya biashara inayoitwa Co-operative Bank of Tanzania Limited” inasomeka taarifa hiyo.
Benki Kuu imeipa benki hii mpya leseni ya biashara ya kibenki, ikiruhusu benki hii mpya kutoa huduma zake kama benki ya biashara katika mikoa yote ya Tanzania. Benki hii, ambayo ina makao makuu Dodoma, inatarajiwa kuchangia kukuza uchumi na kufikia jamii nyingi zaidi kwa kutoa huduma za kifedha zinazolenga maendeleo ya kiuchumi kwa watu wa vijijini na mijini. Leseni hii mpya ilianza rasmi kutumika tarehe 4 Oktoba 2024.
Kabla ya kuungana na kupewa leseni hii mpya, Kilimanjaro Co-operative Bank Limited (KCBL) na Tandahimba Community Bank Limited (TACOBA) zilianzishwa kama benki za ushirika zenye malengo ya kutoa huduma za kifedha kwa wakulima na wanachama wa vyama vya ushirika katika maeneo yao husika. KCBL ilianzishwa mkoani Kilimanjaro na ilijikita zaidi katika kuimarisha uchumi wa wakulima kupitia huduma za mikopo na usimamizi wa akiba kwa vyama vya ushirika vya kilimo.
Kwa upande mwingine, TACOBA ilikuwa na makao yake makuu mkoani Mtwara na ilihudumia jamii ya wakulima na wafanyabiashara wadogo kwa kuwapa mikopo midogo na huduma za akiba ili kuboresha hali ya maisha yao.
Mnamo mwaka 2023, wanahisa wa KCBL walipendekeza kuunganishwa kwa KCBL na TACOBA ili kuanzisha benki ya ushirika ya kitaifa, ambayo ingehudumia vyama vya ushirika kote nchini. Mchakato wa kuziunganisha benki hizi mbili ulilenga kujenga benki yenye mtaji mkubwa zaidi wa kukidhi mahitaji ya ushirika wa kitaifa, huku ikiwa na jukumu la kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa vyama vya ushirika na kufungua fursa za kifedha kwa wanachama wake. Ili kufanikisha mradi huu, CRDB ilichukua jukumu la kuongeza mtaji wa KCBL na TACOBA kwa kupitia uwekezaji wa kifedha na kuimarisha muundo wa usimamizi wa benki hizi.
Kupitia muungano huu, benki mpya ya ushirika inatarajiwa kuwa na matawi katika maeneo kadhaa nchini na kutoa huduma zinazolenga kuimarisha ushirika na uchumi wa vijijini kwa kushirikiana na taasisi za kifedha kama vile Mfuko wa Pembejeo za Kilimo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB).