Kumfundisha mtoto kujisaidia mwenyewe kwa kutumia poti, au choo, ni hatua kubwa katika safari yake ya ukuaji. Wataalamu wanasema kwamba watoto wengi huanza kuonyesha dalili za utayari wa kujifunza kujisaidia wenyewe kati ya miezi 18 na miezi 30, ingawa wengine wanaweza kuanza kabla ya miezi 18 na wengine huchukua muda zaidi kidogo.
Kusubiri hadi mtoto awe tayari kunasaidia kufanya mchakato huu kuwa rahisi kwa sisi wazazi na watoto wetu. Tafiti zaidi zinaonesha kwamba watoto wanapaswa kuanza kufundishwa kujisaidia wenyewe kwa wakati sahihi.
Watoto wanaojifunza kujisaidia wenyewe sana sana kabla ya miezi 18 wana uwezekano mkubwa wa kufanikiwa zaidi kujifunza. Lakini ni zipi dalili za kutambua kwamba mtoto yupo tayari kujifunza kujisaidia, na ni mbinu gani bora zinaweza kuwasaidia watoto wetu kuzoea kwenda msalani kwa utulivu na ufanisi?
Watoto, kama ambavyo tayari tunafahamu, hujifunza vizuri kwa kutazama mazingira yanayowazunguka. Hivyo, tunaweza kuwafundisha kutumia poti, au choo, kwa kuwaonesha picha, au kwa mfano binafsi. Hii itasaidia kutambua kwamba kutumia choo, au poti, ni kitu cha kawaida na sio jambo la kuogopa.
Pale mtoto akikataa kabisa kutumia poti, au choo, kujisaidia sio mbaya kusitisha kidogo na kujaribu tena baada ya siku kadhaa, au wiki. Wataalamu wa malezi na makuzi ya watoto hushauri kuwapa muda watoto kuzoea kutaka kutumia poti, au choo, kujisaidia wenyewe na tujitahidi kutokuwalazimisha pale wakikataa.
SOMA ZAIDI: Michezo Haiwapotezei Muda Watoto, Inawajenga. Tuipe Kipaumbele
Watoto wengi wanaanza kuonesha utayari wa kujifunza kujisaidia wenyewe kati ya umri wa miaka miwili hadi mitatu, ikitegema na ukuaji wa kipekee wa kila mtoto. Kuna dalili tofauti tofauti zilizofanyiwa utafiti ambazo zinaweza kuashiria utayari wa mtoto.
Kwa mfano, watoto wanaoweza kudhibiti haja ndogo na kubaki wakavu kwa angalau masaa mawili au kuamka wakiwa hawajajikojolea wakati wa usingizi, wanakua na udhibiti wa kibofu cha mkojo. Watoto hawa wanaweza kuwa wameanza kudhibiti mkojo na haja kubwa peke yao.
Pia, watoto wenye ratiba ya kuwa na haja kubwa kila siku wana mwelekeo mzuri wa kujifunza kwa urahisi, kwa sababu miili yao inakua tayari ina ratiba ya kutaka kujisaidia kwa wakati flani. Watoto wenye mpangilio wa haja kubwa mara kwa mara hujifunza kujisaidia bila usimamizi kwa haraka zaidi.
Dalili nyingine ni pale mtoto anapoanza kuhisi kukerwa na nepi chafu, au hali ya kutokua mkavu akijikojelea, na kuomba abadilishwe mara kwa mara. Hii huashiria kwamba mtoto anaanza kutambua kwamba anahitaji kwenda msalani kwa wakati fulani na anaweza kutumia maneno, au kwa ishara mbalimbai kumjulisha mzazi au mlezi.
Pia, mtoto akianza kuelewa na kufuata maelekezo rahisi kama “kaa kwenye poti” au ‘’chuchumaa’’ inaashiria kwamba yuko kwenye nafasi nzuri ya kujifunza na kujenga hamu ya kujitegemea. Watoto wanaoanza kuonesha hamu ya kufanya mambo wenyewe mara nyingi wana utayari wa kuchukua jukumu la kujisaidia.
SOMA ZAIDI: Dondoo Chache za Kutuwezesha Wazazi Kujenga Mahusiano na Walimu kwa Malezi, Elimu ya Watoto
Pamoja na hayo yote, mtoto anahitaji kuwa na uwezo wa kimwili wa kufika chooni, kuvua nguo, na kukaa kwenye poti, au choo, mwenyewe. Hii ni ishara kubwa kwamba anaweza kuanza kujifunza kujisaidia mwenyewe.
Pale tunapoona kwamba watoto wetu wanaanza kuonesha utayari wa kujisaidia wenyewe kwa kutumia poti, au choo, kama tulivyojadili hapo juu, tunaweza kutumia mbinu zifuatazo za kitaalamu kuwasaidia.
Kwanza kabisa, tunaweza kuanzisha ratiba ya kudumu ya kujisaidia; hii itasaidia kumjengea mazoea na tabia ya kutumia poti au kwenda msalani kwa muda flani.
Jambo la pili ni kuchagua vifaa sahihi vya mtoto kama poti (la umri wake) au kiti cha choo ambacho miguu ya mtoto inafikia, wazazi wengine huweka kigoda ambacho mtoto hukanyagia kupanda na kukaa wakati anatumia choo. Vifaa sahihi huwasaidia watoto kujenga ujasiri wanapojifunza kujisaidia wenyewe na kutumia msalani.
Wakati wa kumfundisha mtoto kutumia choo, changamoto mbalimbali zinaweza kutokea. Mtoto anaweza kukataa kutumia poti, au choo, kwa kuwa na uoga wa kukaa kwenye sehemu hizo au sauti ya kuflush. Ikiwa imetokea hivyo, inaweza kuashiria kwamba mtoto bado hajawa tayari, hivyo tunapawa kuwapa mda wa kuzoea jambo hili ambalo ni jipya kwao.
SOMA ZAIDI: Fikra za Watoto Juu ya Ukuaji Wao
Kwa kuwa watoto wanakuwa wanajifunza kutumia poti, au choo, ni kawaida sana mtoto kijikojolea, au kuwa na haja kubwa, kabla hajalifikia poti au choo. Hii ikitokea, tunashauriwa kujitahidi kutokukasirika, kuwafokea au kuwapiga. Tunapaswa kuwa waelewa na kuzungumza nao kwa upole, huku tukiwaelekeza kidogo kidogo mpaka atakapoweza.
Pia, tunashauriwa kuendelea kuwavalisha watoto nepi wakati wa usiku tunapoanza kuwafundisha kujisaidia wenyewe kwa sabau ni vigumu kwao kujidhibiti wakiwa uzingizini.
Tuelewe kwamba kumfundisha mtoto kujisaidia mwenyewe kwa kutumia poti, au choo, inahitaji uvumilivu na subira. Mafunzo haya yanaweza kuchukua miaka miwili hadi minne mpaka mtoto aweze kujisimamia mwenyewe.
Tujitahidi kutathmini tabia za watoto wetu ili tuweze kutambua dalili zilizotajwa hapo awali na kufuata mbinu zilizoshauriwa na wataalamu wa malezi na makuzi ya watoto.
Tusisahau pia kuwapongeza na kuwahimiza watoto pale wanapoanza kutumia poti, au choo, kwa kuzungumza nao, kuwaimbia nyimbo na hata kuwapa zawadi ndogo ndogo kila mara wakiweza kufanya hivyo.
Tunapaswa kujitahidi kuepuka kuwafokea, au kuwapiga, au kuwalazimisha kutumia poti, au choo, kwani tunaweza kupelekea mtoto kukataa kabisa kujifunza.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.