Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania na Benki ya TCB zimekanusha taarifa zilizosambaa mtandaoni kuwa huduma ya M-Koba inaelekea kufungwa na Serikali kutokana na madeni.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari na ujumbe mfupi kwa wateja wao, Vodacom na Benki ya TCB wameeleza kuwa taarifa za kufungwa kwa M-Koba ni za uongo na uzushi zilizolenga kuleta taharuki kwenye jamii.
“Tafadhari puuza taarifa za uongo zinazosema kuwa M-Koba inaelekea kufungwa,” inasomeka sehemu ya ujumbe mfupi waliotumiwa wateja wa huduma hiyo wa mtandao wa Vodacom Tanzania.
Huduma ya kifedha ya M-Koba ilianzishwa takribani miaka minne iliyopita na Benki ya TCB ambayo inamilikiwa na Serikali kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania wakifanya kazi chini ya usimamizi wa Benki kuu ya Tanzania (BOT).
Huduma hii inawawezesha wateja wake walio kwenye vikundi kama vile VICOBA, familia na vikundi vingine vya kijamii kwa ujumla kuweza kuchangisha na kuhifadhi fedha zao kidijitali.
Tangu kuanzishwa kwa huduma hii imekuwa na mwitikio mkubwa kwa vikundi ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23 pekee, Vodacom Tanzania ilieleza kuwa takribani bilioni 160 ziliwekwa na vikundi.
Huduma hii pia inatajwa kuweza kufikiwa kwa kiwango kikubwa na wanawake ambao katika ngazi ya jamii wanatajwa kuwa ndio washiriki wakubwa katika vikundi vya kusaidiana na kukopeshana.
SOMA ZAIDI: Tumezungumza na Vijana Kumi Waliojiajiri Kupata Uzoefu Wao. Hiki Hapa Ndicho Walichotuambia
Hii inathibitishwa katika taarifa ya fedha ya Vodacom Tanzania ya mwaka wa fedha 2023/24, imeeleza kuwa asilimia 60 ya miamala ya M-Koba iliyoanzishwa katika kipindi hiko, ilianzishwa na wateja wake ambao ni wanawake.
Katika hatua nyingine Vodacom Tanzania na Benki ya TCB zimewahakikishia wateja wake kuwa suala la usalama wa wateja na akaunti zao ni kipaumbele cha juu kwao, na wataendelea kudumisha uaminifu katika huduma zote za kifedha.
One Response
Naomba Sana M KOBA kuboresha huduma zenu hususan pale mtu anaponunua hisa Au kufanya michango mingine ya kikundi taarifa za miamala yake ziletwe haraka na si hadi tupige huduma kwa wateja. Vilelvile KUWEKWE OPTION YA KATIBU KUTUMA JUMBE kwa wanakikundi moja kwa moja huko huko kwenye APPLICATION ya M PESA na si Kutumia jumbe za kawaida tu.