Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimetoa wito kwa Jeshi la Polisi kuharakisha uchunguzi na kuwatia nguvuni wahusika waliosababisha kifo cha Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kilolo, Iringa, Christina Nimrod Nindi.
Taarifa za polisi zinaeleza kuwa Christina alivamiwa na vijana watatu nyumbani kwake katika Kijiji cha Ugwachanya Kitongoji cha Banawanu huko Iringa na kumshambulia kwa kumpiga risasi na kwa kitu chenye ncha kali.
Katika taarifa yake LHRC imelaani vikali matukio haya ya mauaji, na kueleza kuwa yanakwenda kinyume na Katiba ya Tanzania.
“Tukio hili ni mwendelezo wa matukio ya kihalifu yanayofanywa na watu wanaotambulika kwa jina la ‘wasiojulikana’ ambayo yamekuwa yakihatarisha usalama na uhai wa raia,” LHRC imeeleza katika taarifa yake.
“Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinalaani vikali mauaji haya ya kikatili kwani yanatishia usalama, uhai na kwenda kinyume na misingi ya Katiba na mikataba ya kimataifa na haki za kimsingi za kila binadamu,” iliongeza taarifa hiyo.
Tukio hili la kuuwawa kwa Christina linakuja ikiwa ni takribani miezi miwili toka mtendaji wa sekretarieti ya CHADEMA Ali Kibao atekwe na watu wasiojulikana mnamo Septemba 06, 2024, na mwili wake kuokotwa mnamo Septemba 08,2024, Polisi wanaeleza kuwa bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
2 responses
out of mood
polen ccm