Kurusha vitu ni kitendo kipya ambacho watoto hujifunza kufanya wakiwa na umri kati ya mwaka mmoja na minne, na ni kitu kinachowafurahisha sana. Watoto wanapojua kwamba wana uwezo wa kurusha vitu, inakuwa kama mchezo na mazoezi kwao.
Pia, wanavyorusha vitu, inakuwa ni sehemu ya kujifunza, hapa mtoto anajifunza kwamba kitu chochote anachorusha kinaanguka chini hakibaki juu. Watoto wadogo ni kama wanasayansi wachanga, kila mara wanadadisi, wanajaribu na kujifunza kutokana na majaribio yao.
Sababu za kisayansi zinazopelekea watoto kuwa na tabia ya kurusha vitu ni pamoja na
hatua na maendeleo ya ukuaji. Kutupa na kurusha vitu ni sehemu ya kawaida ya hatua za ukuaji wa mtoto inayomsaidia kujifunza juu ya sababu na matokeo, mjongeo, sauti, vishindo, na namna gani vitu hupaa na kutua au kujongea.
Huwasaidia pia kukuza ujuzi wa mjongeo wa mwili na jinsi ya ushirikiano au mawasiliano kati ya mikono na macho.
Kurusha vitu mara nyingi huwa ni njia ya watoto wadogo kuwasiliana kwa sababu katika umri huu wanakuwa bado hawana maneno na misamiati ya kutumia kujieleza. Hutumia njia hii wakati mwingine kuashiria kwamba wamemaliza jambo fulani, au kuonesha kwamba hawajaeleweka ishara zao za kuelezea jambo fulani.
SOMA ZAIDI: Fanya Haya Kumsaidia Mtoto Kuanza Kujisaidia Mwenyewe kwa Kutumia Poti au Choo
Wakati mwingine watoto hurusha vitu wanapokuwa na hasira, au mazingira waliyopo hayachangamshi. Hii hutokea kama njia pekee ya wao kuweza kuelezea hisia zao maana bado hawajamudu kudhibiti hisia.
Kutupa vitu pia husaidia watoto kuwasiliana na kushirikisha walezi wao na watoto wenzao na hivyo kujifunza lugha na ishara za mawasiliano zinazotumiwa na jamii zao na watu wa karibu yao.
Hivyo, tuelewe kwamba kurusha vitu ni sehemu ya kawaida ya hatua na maendeleo ya ukuaji, mchezo, udadisi na uchunguzi wa dunia inayowazunguka.
Hatari
Wazazi tunapaswa kuelewa kwamba pamoja na kwamba tabia hii ni sehemu muhimu ya hatua za ukuaji, bado kuna hatari mbalimbali zinazoweza kutokea ikiwa ni pamoja na mtoto kujiumiza, au kumuumiza mtu mwingine pamoja na kuharibu vitu akivirusha.
Hivyo basi, tunaweza kuwadhibiti, au kupunguza, na kuwafundisha kurusha vitu kwa usalama kwa kutumia mbinu zifuatazo.
SOMA ZAIDI: Michezo Haiwapotezei Muda Watoto, Inawajenga. Tuipe Kipaumbele
Kwanza, tuwaonyeshe vitu ambavyo wanaweza kurusha na ambavyo hawaruhusiwi kurusha. Mfano, tunaweza kumwambia mtoto kuwa anaweza kuurusha mpira ila akiwa nje tu.
Pia, tukiwa na mpira laini tutaweza kupunguza ajali nyumbani ikiwa mtoto amerusha mpira huo ndani ya nyumba. Tunaweza kufanya michezo kama kutumia kikapu ambacho wanaweza kurushia vitu himo.
Watoto wanapokuwa wanacheza muda mwingine wanaweza kurushiana vitu ambavyo vinaweza kuwaumiza kama vile mchanga, mawe, na kadhalika. Hivyo, ni vyema kuwaambia mapema kuwa vitu hivyo havipaswi kurushwa.
Kama tulivyosema hapo awali, kuna wakati pia watoto hurusha vitu kwa sababu wamekasirika, tunapoona hivyo, tunapaswa kuingilia kati na kutambua sababu ya hisia hiyo na kumtafutia kitu kingine cha kuchezea au kufanya.
Tujitahidi pia kuweka vitu hatarishi kama vile visu, mikasi, na kadhalika, mbali na eneo ambalo mtoto yupo, yaani tuhakikishe mtoto hawezi kuvifikia. Pale mtoto atakavyokuwa amekaa chini kucheza, tuweke vitu vyake – midoli, mipira laini, vigari – karibu ili akivirusha aweze kutambaa au kutembea kuvifuata na baadae tunaweza kusaidiana nao kuviokota na kupaweka safi mahali ambapo amechezea.
SOMA ZAIDI: Dondoo Chache za Kutuwezesha Wazazi Kujenga Mahusiano na Walimu kwa Malezi, Elimu ya Watoto
Hii inamfundisha mtoto kwamba ana jukumu la kufanya usafi sehemu alipopachafua. Tusitegemee kwamba anaweza kupanga, kuokota, au kufuta sehemu hiyo peke yake, haswa katika umri huo.
Tuwajengee mfano mzuri kwa kufanya vitu vya kawaida nyumbani kama kutupa makaratasi, au, uchafu kwenye pipa la taka, kutupia soksi au nguo kwenye tenga la nguo, na kadhalika.
Kurusha chakula
Kurusha chakula ni kitendo kingine ambacho watoto hupenda kufanya katika hatua hii ya ukuaji. Ili kuepuka kuchafua sakafu, au ukuta, na kuchezea chakula ni vyema mzazi, au mlezi, kukaa na mtoto wakati anakula ili atakapotaka kurusha chakula unaweza kumkanya kwa upole na kuonyesha msimamo kwamba ni marufuku kutupa chakula.
Kingine ambacho tunaweza kufanya ni kumpatia mtoto vyombo ambavyo havivunjiki kama vya mfupa au silikoni/mpira wakati anakula ili kuzuia ajali za hapa na pale. Pia, tuwawekee chakula kidogokidogo kwenye sahani na kuwaongezea kadri wanavyoendelea kula.
Wakati mwingine, watoto hurusha chakula kwa sababu amechoka kula au kama ishara kwamba ameshiba, tukitambua hilo basi tunapaswa kuwaonya kwa upole kabla ya kuwaondoa mezani.
SOMA ZAIDI: Fikra za Watoto Juu ya Ukuaji Wao
Ili kuwasaidia na kuwafundisha watoto kuacha kurusha vitu, tunapaswa kuwa wavumilivu na kujaribu kutokuchukulia kila kitendo cha kurusha kama kosa kubwa. Tukumbuke kwamba watoto hawafanyi hivyo kwa makusudi, bali ni sehemu ya furaha na kujifunza kwake.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.
One Response
Hongereni kwa kazi nzuri! Hakika ninajifunza kupitia nakala hizi zenu