The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Watoto wa Miaka Mitano Wana Harakati Nyingi. Mbinu Hizi Zitakusaidia Kukabiliana Vizuri

Katika umri huu, watoto hupitia hatua kubwa za ukuaji za kimwili, hatua zenye harakati nyingi zinazotufurahisha na pengine kutukwaza sana wazazi.

subscribe to our newsletter!

Kama wewe ni mzazi, au mlezi, wa mtoto wa miaka mitano, huenda tayari umeshaona kwamba wana shauku isiyoisha ya kudadisi na kujifunza na kugundua dunia na wana maswali mengi mno. Katika umri huu, watoto hupitia hatua kubwa za ukuaji za kimwili, hatua zenye harakati nyingi zinazotufurahisha na pengine kutukwaza sana wazazi.

Katika umri huu, watoto hukua kwa kasi na uwezo wao wa kutumia misuli ya miili yao kufanya vitu mbalimbali pia hukua. Wataalamu wanatueleza kwamba mabadiliko haya husababishwa na ukuaji wa sehemu ya ubongo iitwayo cerebellum, inayohusika na uratibu wa mwili.

Shughuli kama kuogelea, kupanda, au kukwea, vitu, na kukimbia kimbia huchochea ukuaji huu wa kifiziolojia na kuimarisha uwezo wa mwili. Madaktari wanapendekeza watoto wawe na shughuli tofauti zinazochangamsha mwili ili kuimarisha misuli yao na kukuza tabia za kiafya ambazo zitadumu kwa maisha yote.

Hata hivyo, ukuaji huu mara nyingi huambatana na hali ya kutotulia maana dakika moja mtoto amekaa chini na nyigine amepanda juu ya kochi au dirisha au amekimbilia chumbani, na kadhalika. 

Dk Angela Duckworth, mwanasaikolojia maarufu wa watoto, anabainisha kuwa watoto wa miaka mitano wanakuwa hawatulii sehemu moja kwa sababu sehemu za ubongo zinazodhibiti utulivu hazijakua kikamilifu. Ubongo wao unawaelekeza watembe tembee, wakimbie, waruke, na kadhalika.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Watoto Wadogo Wanapenda Kurusha Vitu?

Tafiti nyingi zinaonyesha umuhimu wa watoto kuwa na shughuli tofauti za kifiziolojia katika ukuaji wao. Tafiti hizi zinaonyesha kuwa shughuli hizo hupunguza msongo wa mawazo, huongeza umakini, na hata kuboresha uwezo wa kutatua matatizo kwa watoto. Chama cha Moyo cha Marekani kinapendekeza watoto washiriki angalau dakika 30 kwa siku katika shughuli za kuchangamsha mwili, ikiwemo michezo.

Mahusiano

Katika umri huu wa miaka mitano, watoto huanza kujenga mahusiano na wenzao, na wakati mwingine hupenda kukutana na watoto wenzao ili wacheze. Sasa pata picha una watoto sita nyumbani kwako wa umri huu na wote wanakimbia kimbia na kuparamia vitu na kuuliza maswali kwa wakati mmoja. 

Unaweza hisi kuchanganyikiwa na kukosa uvumilivu. Hivyo, kuepukana na hali hii na kuwawezesha watoto wetu kucheza vizuri na wenzao, wataalamu wa maendeleo ya watoto wanapendekeza mbinu mbalimbali zinazoweza kumsaidia mzazi, au mlezi, kwenye mchakato huo.

Hizi ni pamoja na kuchagua na kuamua idadi ya watoto wanaokuja kucheza nyumbani. Watoto wawili wanapocheza pamoja wanapata nafasi nzuri ya kujifunza kushirikiana kuliko wakiwa katika kundi kubwa, ambapo kuna uwezekano wa wengine kujiona wamesahaulika.

Wazazi na walezi pia tunaweza kuweka muda wa kawaida wa kucheza: Dakika 60 au 120 ni muda mzuri wa kucheza. Ikiwa mambo yanaenda vizuri, unaweza kuongeza muda kidogo, lakini ni bora kumaliza wakati watoto bado wanafurahia na hawajachoka sana.

SOMA ZAIDI: Fanya Haya Kumsaidia Mtoto Kuanza Kujisaidia Mwenyewe kwa Kutumia Poti au Choo

Tutoe mwongozo wa sheria za nyumbani: Tuhakikishe kuwa, watoto wanaokuja kucheza wanaheshimu sheria za nyumba yetu. Tuwahimize watoto wetu kuwa mfano hai na mzuri kwa marafiki zao, kama sheria ni kwamba watoto hawapandi juu ya meza, au hawakimbii ndani, basi watoto wote wanapaswa kufuata sheria hiyo. Hii inasaidia kudumisha usalama, nidhamu na heshima kwa wote.

Kingine cha kufahamu ni kwamba watoto wa umri huu wana nguvu sana ndiyo maana wanaweza kuwa wamechoka ila bado wataendelea kucheza na wakati mwingine wao wenyewe hawatambui kwamba wamechoka, hii ni sifa moja maarufu kwa watoto wa umri huu. 

Kwa mujibu wa Dk Stephen Porges, mtaalamu wa neva, hali hii inahusiana na ukuaji wa interoception, au uwezo wa kutambua hisia za ndani za mwili kama uchovu au njaa. 

Ili kuwasaidia watoto katika hili, tunapaswa kuwa na ratiba thabiti ya kupumzika na kulala, kuwapatia watoto shughuli ambazo zinachangamsha ubongo kama kusoma vitabu na kuchunguza mienendo ya watoto ili kutambua kama wmechoka na kuwahimiza wapumzike.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts