The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Una Mtoto Mwenye Umri Kati ya Miaka Miwili na Sita? Haya Yatakusaidia Kumjengea Nidhamu

Kwa kuwekeza katika nidhamu chanya, tunawaandaa watoto wetu kwa maisha yenye mafanikio na mahusiano mazuri.

subscribe to our newsletter!

Kujenga nidhamu ya mtoto huenda sambamba na umri alionao kwa wakati huo, na vyote viwili hutegemea hatua ya ukuaji wa ubongo aliyopo mtoto husika ambapo hatua ya ukuaji wa ubongo humsaidia mtoto kukabiliana na hisia zake. 

Ubongo wa mtoto mwenye umri kati ya miaka miwili hadi sita hukua kwa kasi sana, ambapo hisia zao huwa juu, lakini uwezo wa kudhibiti hisia hizo bado huwa haujakomaa. 

Watoto wa umri huu wanaweza kuonyesha tabia kama kurusha vitu wakiwa na hasira, kukataa kufuata maagizo, au kulia kwa nguvu wanapokosa wanachotaka. Ingawa wazazi wengi huchukulia tabia hizi kama ukosefu wa nidhamu, ukweli ni kwamba hali hizi ni za kawaida na zinaweza kudhibitiwa kwa msaada wetu sisi wazazi.

Kwa nini watoto hukosea? Ni kwa sababu sehemu ya mbele ya ubongo wa mtoto, ambayo kwa kitaalamu inatiwa prefrontal cortex, inayohusika na fikra na udhibiti wa hisia, bado haijakomaa. 

Hii ina maana kwamba watoto wanategemea zaidi hisia zao badala ya kufikiria matokeo ya hisia hizo. Kwa sababu hiyo, wanakosea mara kwa mara bila kuelewa athari za tabia zao.

Dk Daniel Siegel, profesa wa saikolojia na mwandishi wa kitabu cha The Whole-Brain Child, anasisitiza kwamba watoto wanapokosea wanahitaji kuongozwa na sio kuadhibiwa au kuaibishwa. Hapa ndipo dhana ya nidhamu chanya inapoingia, kwa kuwafundisha watoto kudhibiti hisia na tabia zao kwa njia zinazowajenga badala ya kuwaumiza.

SOMA ZAIDI: Watoto wa Miaka Mitano Wana Harakati Nyingi. Mbinu Hizi Zitakusaidia Kukabiliana Vizuri

Katika tamaduni nyingi, adhabu za kimwili kama viboko na zile za kihisia kama vile kufoka bado zinachukuliwa kuwa njia sahihi ya kuwaadabisha watoto. Ingawa zinaweza kuleta matokeo ya haraka, tafiti zinaonyesha kwamba viboko na kufoka mara nyingi husababisha hofu na nidhamu ya woga badala ya kuelewa. 

Adhabu hizi zinaweza kuathiri vibaya afya ya akili na kujiamini kwa mtoto, zinaongeza tabia ya fujo na kupunguza uwezo wa kujidhibiti na zinadhoofisha uhusiano kati ya mzazi na mtoto. 

Pia, adhabu hizi zinaweza kumuumiza mtoto, kusababisha majeraha na hata kifo kama tulivyosikia taarifa ya hivi karibuni ya mtoto Chloy aliyepoteza maisha baada ya kuchapwa na mwalimu wake.

Kwa mfano, Chama cha Madaktari wa Watoto cha Marekani (AAP) kimebaini kuwa adhabu za kimwili zinaweza kujenga tabia ya ukatili kwa watoto wanapokuwa watu wazima, kwani hujifunza kutumia vurugu na ubabe kutatua migogoro na changamoto. 

Nidhamu ya hofu haijengi nidhamu ya kweli bali nidhamu ya woga na tabia za udanganyifu.

Ili kuwasaidia watoto kukuza nidhamu ya kweli, tunapaswa kutambua hisia za mtoto. Watoto mara nyingi hukosea kwa sababu hisia zao zimewaelemea. Tunapowatambua na kuthibitisha hisia zao, tunawasaidia kuelewa makosa yao na jinsi ya kuyarekebisha. 

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Watoto Wadogo Wanapenda Kurusha Vitu?

Kwa mfano, tunapomwambia mtoto aliyekasirika, “Ninaelewa umechukia, lakini kumpiga mwenzako sio sahihi. Njoo uniambie ukiwa na hasira badala ya kumpiga mwenzako,” tunamfundisha njia bora ya kudhibiti hasira yake.

Watoto pia hujifunza vizuri wanapojua wazi kinachotarajiwa kutoka kwao. Wazazi wanapaswa kuwaelekeza watoto kuhusu sheria za nyumbani kwa upendo na kuwakumbusha mara kwa mara. 

Mifano ya mipaka dhahiri inaweza kuwa, “Tunasafisha meza baada ya kula” au “Hatusemi maneno ya ya matusi.”

Au, badala ya kuwaadhibu, tunaweza kuwasaidia watoto kujifunza kutatua changamoto zao. Kwa mfano, tunapomuuliza mtoto kwa upendo, “Kwa nini unalia?” au “Nini kimekukasirisha?” tunawasaidia kutambua sababu za hisia zao. Hii huwafundisha kufikiria kabla ya kutenda na kuwapa ujuzi wa kutatua migogoro.

Watoto pia hujifunza zaidi kwa kuiga tabia za watu wazima wanaowazunguka. Tukiwaonesha nidhamu, heshima, na jinsi ya kushughulikia changamoto kwa utulivu, nao pia watajifunza tabia hizo. Hii inajumuisha jinsi tunavyoongea, tunavyofanya kazi, na tunavyoshughulikia hisia zetu.

Tunapochagua mbinu mbadala za adhabu, tunaimarisha uhusiano wa heshima na uaminifu kati yetu na watoto. Hili linawafanya watoto kuwa tayari zaidi kushirikiana na kujifunza kutoka kwetu.

SOMA ZAIDI: Fanya Haya Kumsaidia Mtoto Kuanza Kujisaidia Mwenyewe kwa Kutumia Poti au Choo

Mbinu hizi husaidia watoto kudhibiti tabia zao, na pia kujenga ustadi muhimu wa maisha kama kudhibiti hisia, kutatua changamoto, na kuonyesha huruma kwa wengine. Tunapowasaidia watoto kuelewa makosa yao badala ya kuwaadhibu, tunawajengea msingi imara wa maadili, heshima, na uwajibikaji.

Kwa kuwekeza katika nidhamu chanya, tunawaandaa watoto wetu kwa maisha yenye mafanikio na mahusiano mazuri. 

Badala ya kuogopa mamlaka, wanajifunza kuiheshimu. Badala ya kutenda kwa hasira, wanajifunza kutenda kwa busara. Hatimaye, tunachangia kuunda kizazi chenye nidhamu ya kweli na uwezo wa kuishi kwa maelewano na wengine.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Kongole na asanteni sana kwa makala hii nzuri kuhusu malezi ya watoto. Nitawafuatilia zaidi ili kujifunza mbinu nzuri za kuwalea na kukuza fahamu za watoto.
    Asante.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts