Umoja wa Ulaya (EU) umetangaza kuzuia ndege za shirika la ndege la Air Tanzania kuingia katika anga la nchi wanachama wa umoja huo, ambazo ni jumla ya nchi 27, kwa kile ambacho jumuiya hiyo imeeleza kuwa shirika hilo halijakidhi vigezo vya usalama wa anga vya kimataifa.
“Umoja wa Ulaya leo umerekebisha orodha yake ya mashirika ya ndege yanayozuiwa kuingia, au kuwekewa vikwazo vya kiutendaji katika kuingia Umoja wa Ulaya,” taarifa hiyo ambayo The Chanzo imeiona inaeleza. “Kutokana na taarifa hii, Air Tanzania imeongezwa kwenye orodha hiyo.”
Taarifa hiyo inaeleza zaidi kuwa sababu kubwa ya kuiongeza Air Tanzania kwenye mashirika yaliyozuiwa ni zile za kiusalama wa anga ambazo zimeainishwa na Wakala wa Usalama wa Anga wa Umoja wa Ulaya (EASA).
Kutokana na taarifa hiyo, Air Tanzania inakuwa sehemu ya mashirika 129 yaliyozuiwa kuingia Umoja wa Ulaya. Air Tanzania imejumuishwa pamoja na mashirika saba mengine ambayo taarifa hiyo imetaja kuwa yana changamoto kubwa, ikiwemo Air Zimbabwe la Zimbabwe, Avior Airlines la Venezuela, Blue Wing Airlines la Suriname, Iran Aseman Airlines la Iran, Fly Baghdad la Iraq and Iraqi Airways la Iraq.
Akizungumzia orodha hiyo, Kamishna wa Usafiri Endelevu na Utalii Umoja wa Ulaya, Apostolos Tzitzikostas, amenukuliwa akisema kuwa yuko tayari kushirikiana na Air Tanzania kuiwezesha kukidhi vigezo husika.
“Uamuzi wa kuijumuisha Air Tanzania katika Orodha ya Usalama wa Anga ya EU ni kwa sababu ya dhamira yetu thabiti ya kuhakikisha kuwa kuna viwango vya juu zaidi vya usalama kwa abiria barani Ulaya na duniani kote,” amesema Tzitzikostas.
“Tunawahimiza Air Tanzania kuchukua hatua za haraka na thabiti kushughulikia masuala haya ya usalama wa anga. Kamisheni yetu itakuwa tayari kutoa msaada kwa mamlaka za Tanzania katika kuboresha usalama wa ndege za Air Tanzania na kuwezesha kuweza kufikia vigezo vyote vya usalama wa ndege kimataifa,” Tzitzikostas anaeleza.
Toka mwaka 2016, Tanzania imekuwa ikiboresha shirika lake la Air Tanzania, hasa kwa kununua ndege mpya. Shirika hilo kwa sasa lina ndege kadhaa, ikiwemo ndege mbili za Boeing 787-8 Dreamliners, ndege tano za Dash 8 Q 400, ndege nne za Airbus A220-300, ndege ya mizigo Boeing 767-300F, na ndege tatu za Boeing 737- MAX 9.
Air Tanzania imeweza kuwa na safari katika maeneo 14 ya ndani ya nchi, maeneo nane ya kikanda na maeneo matatu nje ya Afrika, yaani China, India na Dubai. Taarifa hii ya Umoja wa Ulaya inaweza kuwa kikwazo kipya ambacho shirika hilo la ndege litategemewa kukabiliana nacho.
The Chanzo ilimtafuta Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, kwa kumtumia ujumbe WhatsApp, pamoja na kumpigia ili kufahamu kama Serikali imepata taarifa hizi, na kama kuna hatua zozote imepanga kuchukua kwa sasa. Hata hivyo, mpaka tunachapisha habari hii, Mbarawa hakuwa ametoa mrejesho.
Akiongea kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii,Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa aliweza kufafanua zaidi juu ya taarifa hiyo.
“Ningependa Watanzania wajue shirika letu la ndege halijaanza safari za ulaya na halijafanya safari za ulaya, isipokuwa shirika letu la ndege lipo katika mchakato wa kufanya safari zake ulaya, na katika kufikia hatua hiyo ziko hatua ambazo zinapaswa zitimizwe ya kila eneo kila ukanda na taratibu zake,” alifafanua Msigwa.
Na kuongeza: “Na hivi ninavyozungumza wataalamu kutoka mamlaka zinazosimamia masuala ya anga Ulaya wapo Tanzania, wanaendelea kujadiliana na mamlaka za Tanzania namna ya kufikia hatua ambayo shirika letu litaanza kutoa huduma katika anga la ulaya. Mwakani mapema, wataalamu kutoka mamlaka za Umoja wa Ulaya watakuja nchini kukamilisha taratibu hizi, ili mara moja tuanze safari za ulaya.”
5 responses
Ni hatari na huzuni
Hii nchi haijawahi kuwa serious na jambo lolote, sio sgr sio ATCL kote tabu tupu. Swali la kujiuliza ni kwamba je Tunaviongozi ambao wana uchungu na hili taifa?
Wazungu wanatuonea sana kila tukikukuluka wanatafuta sababu ya kutuludisha nyuma Africa tuna shida lkn wao ndiyo wanatusababishia shida zaidi kwani hawataki tujiendeshe kenge hawa
Kama hatufanyi safari za EU then the prohibition is hot air.hahaha. by the way naona ni Moja ya kuzuia ushindani wa kibiashara TU.since when hawa jamaa wakatukubali..
Ni dharau TU.
Nassoro Mbweze unawatukana EU kwa kukataa kuruhusu ndege zetu – lakini katika toleo hili hili la Chanzo kuna habari ya EU kutupatia mabilioni ya misaada nasi tumeyapokea kwa mikono miwili ! Usiwe mnafiki ndugu yangu.