Dar es Salaam. Leo Disemba 16, 2024, zinatimia siku 100 tangu aliyekuwa mwanasiasa mwandamizi wa chama cha upinzani cha CHADEMA, Ali Mohamed Kibao, alipotekwa Septemba 6, 2024, na mwili wake kupatikana Ununio, Dar es Salaam, Septemba 7, 2024, akiwa ameuwawa huku mwili wake ukiwa umeharibiwa vibaya.
Tukio hilo liliteka hisia za wengi, na Septemba 8,2024, siku ambayo ndugu walienda kuutambua mwili wa Kibao katika hospitali ya Mwananyamala, Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kurasa zake mitandaoni aliagiza uchunguzi ufanyike.
“Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,”alieleza Rais Samia.
Hata hivyo, mpaka tukiwa tunaandika habari hii hakuna taarifa zozote zinazohusiana na uchunguzi wa mauaji ya kada huyo wa upinzani.
Hali hiyo ikatufanya tumtafute msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime, tukitaka kufahamu kama bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na mpaka sasa umefikia wapi?
Akizungumza kwa njia ya simu na The Chanzo, Misime alielekeza kuwa atumiwe ujumbe mfupi kuhusiana na kile tunachohitaji kukifahamu. Tulimtumia ujumbe kwa njia ya WhatsApp ambapo licha ya kuuona hatukupokea majibu yoyote mpaka tunachapisha habari hii.
Imani yetu ni ndogo
Oktoba 25, 2024, mmoja wa watoto wa Kibao, Mohamed Ali Kibao, kwa niaba ya familia alijitokeza hadharani na kumsihi Rais Samia aingilie kati kwa kuhakikisha haki inatendeka dhidi ya watu waliohusika na uhalifu huo.
Mohamed alieleza kuwa mpaka siku hiyo hakuna walilokuwa wanalijua kuhusiana na uchunguzi wa mauaji ya kikatili ya baba yao.
“Tunaomba uwazi kidogo katika harakati za uchunguzi huu kwa sababu mpaka sasa ilichukua karibu wiki mbili baada ya mauaji polisi kuja kuongea na familia,” alisema Mohamed kupitia video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.
“Suala la pili ambalo tunakuomba kama Amiri Jeshi Mkuu ni kutoa kauli kali dhidi ya wale wanaohusika na matukio haya. Dhidi ya wahusika, siyo tukio tu, hapana, dhidi ya wahusika, ili na wao waishi kwa wasiwasi kama ambavyo tunaishi kwa wasiwasi sisi wanafamilia na Watanzania kwa ujumla,” Mohamed alieleza zaidi.
Akizungumza mnamo Novemba 15, 2024, kwenye mjadala uliofanyika katika mtandao X, Mohamed Ali Kibao elieleza kuwa familia yake imeendelea kuishi kwenye mazingira ya wasiwasi mkubwa, hata hivyo anasema baada ya wito alioutoa alipokea mrejesho.
“Baada ya wito ule kuna mazungumzo ambayo yalifanyika kuonesha ishara kwamba kuna hatua kidogo katika uchunguzi,” anaeleza Mohamed.
“Tutaendelea kupigania kuhakikisha haki inapatikana hata kama itachukua muda,” Mohamed aliongeza. Lakini imani yetu kwamba hili suala litapata ufumbuzi, imani yetu ni ndogo sana.”
“Tangu tukio litokee mpaka sasa hisia zetu ni kwamba hili ni jambo ambalo litakwenda lipotee kimyakimya kama mifano mingine ambayo imetokea hadharani na mpaka leo majibu hatujayapata.”
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com