The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wimbi la Wachina Kununua Migodi ya Wachimbaji Wadogo Wadogo Lazua Hofu ya Upotevu wa Ajira, Mapato na Uchafuzi wa Mazingira

Wachimbaji kutoka China wamekuwa wakinunua migodi kutoka kwa wachimbaji wadogo kwa kisingizio cha kutoa msaada wa kiufundi

subscribe to our newsletter!

Mgodi wa Mwakitolyo Namba 5, wenye zaidi ya wachimbaji 10,000, upo katika hali ya sintofahamu hadi sasa. Ofisi yake imefungwa baada ya kuharibiwa kufuatia mvutano uliokuwa kati ya wachimbaji wadogo, viongozi wao, na wafanyabiashara wanaoonunua migodi eneo hilo kutoka China.

Mzozo huu unaonyesha wasiwasi unaoongezeka kuhusu wachimbaji wa Kichina kuchukua migodi midogo, hasa Mwakitolyo, mji wenye watu 38,000 katika eneo lenye utajiri mkubwa wa dhahabu la Shinyanga.

“Mvutano kuhusu kuuza migodi kwa wawekezaji wa Kichina umekuwa mkubwa hapa, na hili linaathiri zaidi wachimbaji wadogo ambao hawana namna nyingine,” alisema Leonard Waziri, mchimbaji mdogo na msimamizi wa mgodi wa Mwakitolyo 5.

Waziri alieleza jinsi wachimbaji wadogo walivyolazimika kuhamia katika migodi midogo baada ya migodi jirani kuuzwa kwa Wachina.

“Tangu migodi mingi ya eneo hili ilipochukuliwa na Wachina, wachimbaji wadogo walihamia mgodini hapa. Sasa, kuna siku hapa ofisini tulikutana na wawekezaji wa Kichina tukawa na mazungumzo fulani, wao [wachimbaji] walidhani tunafanya makubaliano ya kuuza mgodi huu pia, jambo ambalo halikuwa kweli. Walijawa taharuki, wakaamua kuwapiga wale Wachina na kuharibu ofisi hii unayoiona,” alieleza Waziri.

Hofu ya upotevu wa mapato na ajira

Licha ya sheria kupiga marufuku uhamishaji wa leseni za uchimbaji mdogo kwa wageni, wawekezaji wa Kichina mara nyingi huzipata kwa kisingizio cha kutoa msaada wa kiufundi.

Kifungu cha 3 cha Sheria ya Madini (2019) kinaruhusu wamiliki wa leseni kuingia mikataba ya msaada wa kiufundi na wageni, kipengele kinachotumiwa vibaya mara kwa mara.

“Huwa wanakuja kwa kisingizio cha msaada wa kiufundi,” Waziri alifafanua. “Wenyeji mara nyingi huingia mikataba isiyofaa kwa sababu hawana uelewa wa masharti ya mikataba.”

Mara baada ya wawekezaji hawa kuchukua migodi, huzungushia kuta ndefu pande zote na kuendesha uchimbaji mkubwa wa madini, hali inayoongeza taharuki huku wachimbaji wadogo wakilalamika kukosa maeneo ya kujitafutia riziki.

“Hali hapa ni mbaya,” alisema Adamu Kuzenza, mchimbaji mdogo mwingine. “Wawekezaji wanavyozidi kuchukua maeneo, sehemu za uchimbaji zinapungua, na hatuna pa kwenda. Idadi ya watu inazidi kuongezeka, lakini maeneo kwa ajili ya uchimbaji yapungua.”

Kampuni za kigeni zinazofanya kazi chini ya leseni za uchimbaji mdogo huepuka kulipa kodi muhimu na kufuata matakwa yanayowakumba wachimbaji wa kati au wakubwa. Hali hii ilifanya baadhi ya wabunge kuhoji juu ya hatma ya miji midogo midogo iliyokuwa ikitegemea uchumi wa uchimbaji mdogo.

“Wachina wanaendelea kununua migodi midogo kutoka kwa wananchi,” alisema Jumanne Kishimba, Mbunge wa Kahama Mjini, wakati wa akichangia hoja Bungeni, Februari 14, 2024.

“Mgodi uliokuwa ukiwaajiri watu 10,000 au 20,000 na kuzalisha takriban kilo 20 za madini kila mwezi ukiichangia serikali na halmashauri za mitaa sasa uko mikononi mwa Mchina mmoja.”

Kishimba alionya: “Wanaponunua migodi hii, hakuna masharti ya kimkataba yanayohakikisha [huyu mwekezaji] atakuwa anazalisha kiwango fulani. Miji kama Geita, Kahama, na Singida itakuwaje ikiwa hakutakuwa na uzalishaji?”

Maji yamechafuliwa

Athari za kimazingira kutokana na kuchukuliwa kwa migodi hii ni suala lingine linalozua hofu kwa wananchi. Tofauti na wawekezaji wengine wa kati au wakubwa wanaotakiwa kufuata viwango stahiki vya utunzaji wa mazingira, uchimbaji unaondeshwa na wawekezaji hawa husababisha uharibifu mkubwa wa mazingira. Hii inasababishwa na wao kutumia vibali vya wachimbaji wadogo ilhali wengi ni wachimbaji wa kati na wakubwa, hata kwa kuangalia mitaji na dhana zao.

Wakazi wa Nyamahuna, Geita, ambako wawekezaji wa Kichina wamechukua migodi, ni miongoni mwa waathirika wa uchafuzi wa vyanzo vya maji unaowafanywa na wawekezaji hawa.

“Bwawa letu limechafuliwa na wachimbaji wa Kichina,” alilalamika Ndiyabi Kazigile, mkazi wa Nyamahuna. “Mvua inaponyesha, kemikali kutoka kwenye shughuli zao huingia kwenye maji yetu tunayoyategemea kwa kila kitu. Tumejaribu kuwaomba viongozi wetu, lakini hakuna kilichobadilika. Tutaishije sasa?”

James Karidushi akinywa maji kwenye eneo ambalo kemikali kutoka migodini hufika

Mkazi mwingine, Kabalo Malimi, alielezea hali hiyo: “Maji yanakuja yakiwa yamechafuliwa kwani mifereji inayotirisha hizo kemikali zao inapita hadi kwenye visima vyetu. Wanasema Wachina wamelipia maji, lakini maji yetu bado yamechafuliwa. Kama Mwenyekiti wa Kitongoji wa zamani, nilijaribu kupambana hili suala, lakini hakuna kilichotokea.”

Wakati The Chanzo ilipotembelea eneo la Nyamahuna, ilishuhudia maji yenye rangi ya kijani na mifereji ya kemikali ikitiririka kuelekea kwenye bwawa la maji. Suala la milipuko kutoka kwenye shughuli za uchimbaji pia imesababisha uharibifu wa miundombinu mbambali ikiwemo nyumba za wakazi hawa.

“Kuna milipuko mikubwa, na nyumba zetu zinapasuka. Hata hivyo, tunapolalamika, hakuna anayesikiliza,” alisema James Karidushi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kijiji.

Udhibiti

The Chanzo iliwasiliana na Eng. Ramadhani Lwamo, Kaimu Mkurugenzi wa Leseni za Madini na Taarifa kutoka Tume ya Madini Tanzania, ili kuelewa jinsi ununuzi huu wa leseni unavyofanyika licha ya kwamba sheria ya madini inakataza wageni kumiliki leseni ya uchimbaji mdogo.

“Leseni ya uchimbaji mdogo haiwezi kuuzwa kwa mgeni mpaka ibadilishwe hadhi yake. [Hadi sasa], hakuna uhamishaji wa Leseni ya Uchimbaji wa Mdogo (PML) kutoka kwa mwenyeji kwenda kwa mgeni. Tume huchunguza maombi yote ya uhamishaji ili kuhakikisha yanakidhi vigezo,” alieleza Eng. Lwamo.

“Sheria ya Madini inaruhusu wageni kushirikiana na wenyeji (wenye leseni za uchimbaji mdogo) kupitia Mikataba ya Msaada wa Kiufundi iliyosajiliwa na Tume ya Madini. Kwa hivyo, [unachokiona] ni makubaliano kati ya mmiliki wa leseni na mtoa msaada wa kiufundi, na mikataba yote tuliyotoa inajulikana [kwa kuwa kuna] vyeti vya TSA vilivyosainiwa,” alisema.

Baadhi ya wadau wanasema suala hili la wawekezaji wa Kichina kuwepo katika migodi mbalimbali nchini kunatajwa kuwa na lengo lingine zaidi ya uchimbaji wa dhahabu.

Lucy Shao ambaye ni Mkurugenzi wa Utetezi na Mawasiliano wa Hakirasilimali, taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na masuala ya sekta ya madini hapa nchini, anaamini kuwa kuna mambo zaidi yanayojificha nyuma ya mpango huu.

“Tunajua kwamba China ni moja ya nchi zenye mahitaji makubwa ya shaba, hivyo wanatumia migodi hii ya [dhahabu] kuchimba madini mengine kama grafiti na shaba,” anafafanua Shao.

Matonyinga Makaro ni Mwandishi wa The Chanzo anayepatikana Mwanza, unaweza kuwasiliana na Makaro kupitia email yake matonyingamakaro@gmail.com . Kama una maswali, ushauri au habari zaidi wasiliana nasi kupitia editor@thechanzo.com  au 0753815105

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts