The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kukuza Netiboli Tanzania, Juhudi Zinahitaji Kurejesha Mapenzi, Unazi kwa Mchezo Huo Mkakati kwa Taifa

Kunahitajika juhudi kubwa kurejesha mapenzi kwa mchezo huo, kurejesha unazi kama ulivyokuwa kwa timu za Bandari, JKT Mbweni na JWTZ ambazo zilikuwa zinavuta hisia za watu.

subscribe to our newsletter!

Serikali imeeleza kuwa itawekeza nguvu katika michezo sita kuhakikisha inaendeshwa kwa viwango na kuiwezesha kuwa ya ushindani na kushirikisha Watanzania wengi.

Kati ya michezo hiyo upo mpira wa pete, maarufu kwa jina la netiboli, lililotoholewa kutoka lugha ya Kiingereza la netball. Kihistoria, netiboli ndio mchezo wa pili kwa umaarufu nchini baada ya mpira wa miguu ambao pia umo kwenye orodha ya michezo sita ya kipaumbele.

Netiboli, ambao hivi sasa unachezwa pia na wanaume, ndio mchezo rahisi kuchezwa na wanawake na ndio mchezo wa kwanza ambao mtoto wa kike wa Kitanzania hukutana nao anapoanza kujenga mapenzi na michezo.

Katika shule za msingi, unaweza kutoona michezo yote ikichezwa isipokuwa mpira wa miguu na netiboli tu. Michezo hii haiwezi kukosekana katika shule za msingi, sekondari na vyuoni na zamani ndio mchezo uliosaidia wasichana wengi kupata ajira katika majeshi, kampuni za umma na taasisi nyingine.

Lakini ajira hizo zilianza kutoweka wakati Serikali ilipoanza sera za kubana matumizi, huku ikikaribisha sera ya kulegeza masharti ya kibiashara yaliyosababisha Serikali ijipunguzie majukumu ya kuendesha kampuni za kibiashara nakuziacha kwa watu binafsi ambao, kwa bahati mbaya, hawakuona tena umuhimu wa kuwa na michezo.

SOMA ZAIDI: Ziko Wapi Hamasa za CHAN 2025?

Lakini ulegezaji masharti ya kibiashara baadaye ukawa na manufaa kwa michezo kwa kuwa kampuni za kibiashara ziligeuka kuwa wadhamini wa michezo, wakiwekeza fedha kwenye klabu na vyama vya michezo.

Mchezo wa mpira wa miguu, mpira wa kikapu na ngumi za kulipwa ndio ilibahatika kupata udhamini huo kutoka kampuni kama za bia, huduma za simu na benki, lakini hivi sasa wigo umepanuka zaidi kiasi kwamba hata kampuni za michezo ya kubahatisha zinaingiza fedha kwenye michezo, tena fedha nyingi.

Hakuna udhamini

Si ajabu kuona Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likitangaza bajeti yake ya mwaka ya zaidi ya Shilingi bilioni 50, kitu ambacho ni rekodi katika ulimwengu wa michezo Tanzania.

Lakini mchezo wa netiboli haujabahatika kupata udhamini japo wa kutatua matatizo ya uendeshaji wa chama cha kitaifa.

Ilikuwa ni aibu kwa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kushindwa kushiriki mashindano ya kimataifa yaliyofanyika Afrika Kusini kutoklana na kukosa fedha na kushindwa kulipa ada ya Shirikisho la Netiboli la Afrika ya Dola za Kimarekani 250, sawa na takriban Shilingi 500,000 za Kitanzania, fedha ambazo zinaweza kuwa posho ya siku mbili ya mjumbe wa mkutano mkuu wa TFF.

Baada ya kushindwa kutuma timu Afrika Kusini, mwenyekiti wa CHANETA, Devotha Marwa, alilazimika kutumia fedha zake kwenda mashindanoni huko ambako kwa kawaida hufanyika mkutano mkuu wa shirikishi hilo.

SOMA ZAIDI: Kwa Kamwe, Ali: Soka Sasa ni Biashara

CHANETA pia ilishindwa kulipa ada ya Dola za Kimarekani 888, takriban Shilingi milioni mbili za Kitanzania, ambayo ni ada ya uanachama wa Shirikisho la Netiboli la Kimataifa (IFNA), fedha ambayo ni gharama ya viburudisho katika mechi moja ya mpira wa miguu.

Ilifika wakati mwenyekiti wa CHANETA alisema anajuta kugombea nafasi hiyo kwa sababu mambo hayaendi kama alivyotarajia na kuahidi kutotetea kiti chake. Hata hivyo, Marwa alitetea nafasi yake na kurudi madarakani, lakini mambo bado hayaendi vizuri na mchezo huo maarufu nchini.

Mwezi Mei, CHANETA iliendesha mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa yakishirikisha timu kutoka mataifa manne. Ni wakazi wachache waliojua kuwa kwenye uwanja huo kuna mashindano makubwa ya kiwanago hicho.

Hakuna hamasa

Hakuna hamasa kwa umma. Unaoweza kuwakuta wakiangalia ni wachezaji wa zamani wa netiboli, viongozi wao na watu wachache. Na kwa kuwa hufanyika pembezoni mwa uwanja huo mkubwa, huonekana kama mashindano yasiyo ya ushindani.

Ili kufanikisha uendeshaji wa mashindano hayo, Serikali ilisema inatoa Shilingi milioni 10, fedha ambazo zilikuwa ahueni kubwa kwa wenyeji. Lakini ni vigumu sana kwa kampuni binafsi, au ya umma, kuingiza fedha zake kudhamini mashindano ya aina hiyo kwa kuwa hakuna anayefuatilia zaidi ya wadau wakuu.

SOMA ZAIDI: Wageni Hawakuzi Soka la Tanzania, Wanalitangaza

Zile enzi za wananchi kuyafuata mashindano ya netiboli Uwanja wa Relwe Gerezani, au Uwanja wa Ndani wa Taifa, au kwenye viwanja vikubwa vya mikoani, zimetoweka. Wale mawaziri, wabunge, wanamichezo wengine na wananchi kwa ujumla hawaonekani tena kwenye viwanja vya netiboli hadi wawe wageni rasmi.

Netiboli imepoteza mvuto na hali hiyo inaufanya mchezo ushindwe kuwa na vyanzo vizuri vya fedha. Naibu Waziri wa Michezo, Athuman Mwinjuma, aliwahi kuitaka CHANETA imalize tofauti baina ya viongozi ili imani irejee na hivyo kuvuta wadhamini na wengine.

Amani imesharejea na kwa sasa kuna utulivu, lakini mambo hayaendi vizuri.

Pamoja na kuwa moja ya michezo ya kimkakati kwa Serikali, netiboli inahitaji jicho la ziada kuirejesha kwenye viwango vinavyostahili kulingana na ukubwa na umaarufu wake nchini.

Kunahitajika juhudi kubwa kurejesha mapenzi kwa mchezo huo, kurejesha unazi kama ulivyokuwa kwa timu za Bandari, JKT Mbweni na JWTZ ambazo zilikuwa zinavuta hisia za watu.

Vile viwango ambavyo mwenyekiti wa zamani, Anna Bayi, aliufikisha mchezo huo, havina budi kurejeshwa kwa hali na mali, ikiwezekana kumtumia mchezaji huyo wa zamani katika ushauri ili awagawie mbinu alizotumia.

Kurejesha mapenzi na unazi katika mchezo wa netiboli kutavutia kampuni kuwekeza fedha na hivyo kuuwezesha mchezo kupata fedha na ikiwezekana huko mbele netiboli ianze kuajiri.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts