“Wafu wetu kamwe hawawi wafu kwetu mpaka pale tunapokuwa tumewasahau.” Hii ni nukuu mashuhuri kutoka kwa mshairi wa Kiingereza, George Eliot, inayozungumzia thamani ya kuwakumbuka wale tunaowaita wapendwa wetu baada ya kupatwa na umauti, na kulazimika kutangulia mbele ya haki.
Kama ilivyo kwa sehemu nyingine yoyote ile ya dunia, Tanzania pia ilipoteza raia wake wengi kwenye mwaka huu unaoishia wa 2024 kwenye misiba iliyoacha majonzi na simanzi kubwa kwa familia, jamii, na taifa kwa ujumla.
Tukiwa tunamalizia mwaka, sisi hapa The Chanzo tunaungana na familia za wapendwa wetu hawa kukumbuka maisha ya wenzetu waliotangulia mbele ya haki, na kuchagiza kuendelea kusherehekea maisha na urithi waliotuachia sisi tuliobahatika kuendelea kubaki duniani.
Siasa na uongozi
Kwenye orodha hii wapo Watanzania waliolitumikia taifa kwa uadilifu na uwajibikaji wa hali ya juu ambao, licha ya kuwa na kasoro za hapa na pale za kibinadamu, tunalazimika kuenzi maisha yao. Hawa ni pamoja na Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki Februari 29, 2024.
Mzee Rukhsa, kama Watanzania walivyokuwa wanamfahamu Rais huyo wa awamu ya pili wa Tanzania, alifariki kutokana na saratani ya mapafu baada ya kuugua kwa siku chache. Mwinyi, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 99, anatambulika nchini Tanzania kama “Baba wa Mageuzi.”
Kipindi cha uongozi wake uliodumu kati ya mwaka 1985 mpaka 1995, Rais Mwinyi anatambulika kuipitishia Tanzania katika mageuzi ya msingi ya kiuchumi yaliyopelekea kuimarika kwa uchumi na maisha ya Watanzania na yale ya kisiasa yaliyopelekea kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.
Hapa pia tungependa kumtaja Edward Ngoyai Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, aliyefariki Februari 10, 2024. Mbunge wa Monduli kwa miongo kadhaa, Lowassa alifariki akiwa na umri wa miaka 70 kufuatia changamoto za moyo zilizokuwa zikimkabili.
SOMA ZAIDI: Yaliyoing’arisha, Kuipaisha Tanzania Mwaka 2024
Akiandikia The Chanzo kufuatia kifo cha Lowassa, aliyekuwa mgombea wa urais wa CHADEMA 2020, akiungwa mkono na vyama vingine vya upinzani chini ya muungano wa UKAWA, mchambuzi wa masuala ya kisiasa Nicodemus Minde alimwelezea mwanasiasa huyo kama “mtu mwenye utashi wa hali ya juu na utayari usiyo kifani.”
Watanzania watamkumbuka Lowassa kama mtu aliyelitumikia taifa kwa muda mrefu, ambaye, licha ya kukabiliwa na shutuma nyingi dhidi ya uadilifu wake, aliendelea na utumishi wake huo, akitumia muda mchache sana kujitetea, hali iliyowashangaza hata wakosoaji wake.
Tunamtaja hapa pia, kwa mara nyingine tena, Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni (Chama cha Mapinduzi – CCM), aliyefariki Novemba 27, 2024. Kifo cha Dk Ndugulile, aliyepata kuhudumu kama naibu waziri na waziri kamili, kiliwashitua wengi kutokana na wadhifa mkubwa tu aliyotoka kukabidhiwa siku chache zilizopita.
Wajumbe wa Umoja wa Mataifa (UN) walishawishika na hoja za Dk Ndugulile na kumteua kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, hatua iliyoipa Tanzania heshima kubwa ndani na nje ya bara la Afrika.
Mwanasiasa huyu atakumbukwa kwa mengi, ikiwemo uwezo wake wa kuwaunganisha Watanzania nje ya mipaka ya kisiasa na itikadi pamoja na ujasiri wake wa kusimamia maadili ya uongozi na yale ya kitaaluma.
Tukitoka nje kidogo ya siasa tunakutana na Lawrance Mafuru, moja kati ya watu makini waliotokea kwenye sekta binafsi kabla ya kupewa dhamana ndani ya utawala wa umma, aliyefariki Novemba 9, 2024.
Mafuru, aliyefariki akiwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, atakumbukwa kwa mengi na Watanzania, ikiwemo kwa ushauri wake kwa watu waliokaribu na wenye mamlaka kuwaambia ukweli wakubwa wao, akisema kusema uongo kwenye mazingira kama hayo ni dhambi na uhalifu mkubwa ambao msaidizi anaweza kufanya dhidi ya ‘bosi’ wake.
SOMA ZAIDI: Tukiwa Ukingoni mwa Mwaka, Tukumbushane Baadhi ya Matukio Muhimu Yaliyoikumba Tanzania 2024
Kauli hii ilimgusa sana Rais Samia Suluhu Hassan kiasi cha kuirudia kwenye msiba wa Mafuru, akiwataka wasaidizi wake wafuatishe ushauri huo. Tunategemea kwamba watendaji wa Serikali watayaishi maisha ya Mafuru kwa vitendo kwa kutekeleza ushauri aliotuachia na ambao umesisitizwa na Rais wa nchi.
Wengine wanaoingia kwenye orodha ya Watanzania mashuhuri waliofariki 2024 ni Mustafa Mkulo, aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha na mbunge wa Kilosa mkoani Morogoro kwa kipindi cha miaka 10 mpaka mwaka 2015, aliyefariki Mei 3, 2024.
Panya Ali Abdala alikuwa ni mwakilishi wa viti maalumu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, aliyeshikilia nafasi hiyo tangu mwaka 2010, kabla ya kufariki Julai 25, 2024.
Kuna John Tendwa aliyefariki Disemba 17, 2024. Huyu aliwahi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuanzia mwaka 2001 mpaka 2013.
Christina Kibiki, Katibu wa CCM wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, aliuwawa Novemba 13, 2024, baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana nyumbani kwake. Tunamkumbuka pia Ali Mohamed Kibao, mwanamikakati wa CHADEMA, aliyeuwawa kikatili Septemba 7, 2024. Polisi inaendelea kufuatilia undani wa kisa hiki.
Vyombo vya ulinzi
Tukiingia kidogo kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, tunakutana na jina la Jenerali David Mugozi Musuguri, aliyefariki Oktoba, 29, 2024, na kuwaachia Watanzania, pamoja na mambo mengine mengi, mtaa wa Mbezi kwa Musuguri, jijini Dar es Salaam.
Msuguri aliwahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Tanzania kuanzia mwaka 1980 hadi 1988. Pia, akiwa jeshini, mzalendo huyu aliwahi kuongoza majeshi ya Tanzania katika vita dhidi ya Idi Amin wa Uganda mnamo mwaka 1978. Ni wazi, ameishi maisha ya fakhari atakayokumbukwa nayo milele na Watanzania wenzake.
Charles Mbuge, aliyekuwa Meja Jenerali Mstaafu ambaye mwaka 2019 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa. Kati ya mwaka 2021 hadi 2022 aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Kagera. Mbuge alifariki Oktoba 12, 2024.
Utangazaji
Huko kwenye uwanda wa habari na burudani, tunaliona jina la Gardner Habash, maarufu kama Captain, moja kati ya watu ambao sauti zao ziliunguruma kwa miaka kadhaa kwenye vyombo vya habari, vikichangia kwenye kuzalisha maelfu ya watangazaji wapya wa redio na televisheni wanaochangia kulisukuma taifa mbele.
Captain alifariki Aprili 20, 2024, akiwa ni mtangazaji mwandamizi wa kipindi cha Jahazi cha Clouds FM. Captain pia, kama tulivyotangulia kusema hapo awali, aliwahi pia kutangaza redio nyingine kama Times FM na E-FM.
SOMA ZAIDI: Kwa Watanzania Walioipeperusha Vyema Bendera ya Taifa 2024, Kongole
Kwenye orodha hii pia yumo Khadija Shaibu maarufu kama Dida aliyefariki Oktoba 4, 2024. Dida alikuwa ni mtangazaji wa kipindi cha redio ya Wasafi FM, aliwahi pia kuwa mtangazaji wa Times FM.
Michezo & burudani
Tukirudi kwenye sanaa na burudani, tunakutana na Joseph Francis maarufu kama ManDojo aliyeuwawa Agosti 11, 2024. Enzi za uhai wake ManDojo alikuwa ni msanii wa muziki wa kizazi kipya. Taarifa za kifo chake zilieleza kuwa kilitokana na kushambuliwa na watu.
Khalfani Khalimandro, ni mtu mwingine tunayemkuta kwenye uwanda wa sanaa na burudani aliyefariki Mei 5, 2024. Khalfani alikuwa mtayarishaji wa video za muziki wa kizazi kipya.
Marco Joseph ni mdau mwingine wa burudani aliyefariki Agosti 22, 2024. Enzi za uhai wake, Joseph alikuwa ni mwimbaji wa kundi la muziki wa injili la Zabron Singers.
Yusuph Kaimu maarufu Pembe alikuwa ni mchekeshaji mkongwe hapa nchini aliyefariki Oktoba 20, 2024.
Boniface Kikumbi maarufu Kingi Kikii alikuwa ni mwanamuziki wa mziki wa dansi aliyefariki Novemba 15, 2024. Grace Mapunda maarufu Tesa alikuwa ni mwigizaji wa filamu aliyeitumikia tansia hiyo kwa miaka 20 aliyefariki Novemba 2, 2024.
Fredy Kiluswa, aliyekuwa muigizaji wa filamu, alifariki Novemba 16, 2024. Frank Patrick maarufu Molingo alikuwa ni mchekeshaji aliyejizolea umaarufu hapa nchini kupitia mtandao wa TikTok aliyefariki Disemba 10, 2024.
Bila shaka watu wengi zaidi ya ambao tumeweza kuwaorodhesha hapa waliagana nasi kwenye mwaka huu 2024, wakiwemo wale waliofikwa na umauti kupitia majanga mbalimbali yaliyolikabili taifa letu kwa mwaka 2024, ikwemo mafurika, moto, kuporomoka kwa majengo, na kadhalika.
Tunaungana na familia zote zilizopoteza wapendwa wao kwa sababu mbalimbali kwenye mwaka huu wa 2024, na tunaungana nao kwenye maombi yao ya kuwatakia dua ndugu zao hawa wapate mwisho mwema huko waliko.
Tunawasihi wasomaji wetu wafuate nyayo njema zilizoachwa na wapendwa wao hawa kwenye michakato yao ya kukuza miingiliano ya kijamii na kujitafutia maendeleo yetu binafsi na yale ya taifa letu kwa ujumla.