The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

FIFA Yatoa Kanuni Mpya za Uhamisho wa Wachezaji. Klabu Zetu Zinafuatilia?

Sasa kutakuwa na uwezekano wa wachezaji wengi kuvunja mikataba yao, huku nguvu ya kuamua masuala ya malipo ikihama kutoka mikononi mwa klabu na kwenda kwa wachezaji na mawakala wao.

subscribe to our newsletter!

Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) limetoa kanuni mpya za uhamisho wa wachezaji, likiweka vipengele vilivyokuwa sehemu ya hukumu ya kesi iliyofunguliwa na mchezaji wa zamani wa Ufaransa, Lassana Diarra, akipinga kanuni inayomlazimisha mchezaji kulipa fidia wakati anapovunja mkataba na klabu yake.

Kesi hiyo ilifunguliwa na mchezaji huyo katika Mahakama ya Haki ya Ulaya (ECJ) baada ya kushindwa katika shauri lililofunguliwa mbele ya Kitengo cha Usuluhishi cha FIFA (DRC) na klabu yake ya Lokomotiv ya Russia mwaka 2014.

Lassana, ambaye aliwahi kuzichezea klabu za Arsenal, Chelsea na Portsmouth za England, aliingia katika mzozo wa mshahara na klabu hiyo na klabu hiyo ikaona kuwa kitendo chake kilistahili kuvunjiwa mkataba na hivyo ikauvunja na kuwasilisha suala lake DRC.

Licha ya Lassana kupinga, DRC iliipa ushindi klabu hiyo na kumtoza faini ya Euro milioni 10.5. Wakati huo, klabu ya Charleroi ya Ubelgiji ikampa mkataba, huku ikitaka uthibitisho kutoka FIFA kuwa mchezaji huyo ataweza kuhamia klabuni hapo na Charleroi haitawajibika kulipa gharama zozote atakazodaiwa na Lokomotiv.

FIFA haikutoa uthibitisho huo, huku kanuni zake zikisema Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) hutoklewa na ligi ambayo mchezaji anaihama na hapo ndipo uhamisho huwezekana.

SOMA ZAIDI: Kukuza Netiboli Tanzania, Juhudi Zinahitaji Kurejesha Mapenzi, Unazi kwa Mchezo Huo Mkakati kwa Taifa

Kwa kuwa hakuna fedha zozote zilizolipwa Lokomortiv, hakukuwepo na uwezekano wowote kwa uhamisho wa Lassana kwenda Charleroi kufanyika. Ndipo mwaka 2015 kiungo huyo akaamua kulipeleka suala hilo mahakamani, akidai kupoteza mapato mengi katika sakata hilo.

Uamuzi wake ukawa mwanzo wa mchakato mrefu ambao utasababisha mabadiliko makubwa katika uhamisho wa wachezaji.

Shauri lake liliibua hoja mbili zinazohusiana na sheria za Umoja wa Ulaya. Kwanza, ni haki ya uhuru wa mfanyakazi kwenda popote na pili kulinda ushindani ndani ya soko la ndani.

Na maswali makuu yakawa: Je, FIFA ilimnyima Lassana haki yake ya uhuru wa kwewnda atakako wakati ilipokataa kumuidhinisha kujiunga na Charleroi? Je, wajibu uliowekwa kwa klabu inayomnunua mchezaji wa kulipia gharama za mchezaji kuondoka unaathiri uwezo wa kufanya biashara?

Azam FC na Yanga

Sakata kama hilo liliwakumba wachezaji wawili wa Azam FC na Yanga ndani ya misimu miwili iliyopita.

SOMA ZAIDI: Ziko Wapi Hamasa za CHAN 2025?

Yanga walianza kwa kumzuia mchezaji wao wa zamani wa kiungo, Feisal Salum, kuvunja mkataba wake, licha ya mchezaji huyo kurejesha Shilingi milioni 112 zilizowekwa kwenye mkataba kama fidia iwapo atavunja mkataba. Yanga ilidai sababu zake za kuvunja mkataba hazikuwa za kimichezo.

Ilibidi Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati kwa kuiomba Yanga impe Fei Toto kile anachotaka ikiwa nipe-nikupe iliyoanzia kwa klabu hiyo kumuomba mkuu wa nchi aruhusu kujengwa uwanja wa mpira makao makuu yake, Jangwani, ambako katika miaka ya karibuni kumekuwa na mafuriko kila nyakati za mvua kubwa.

Mchezaji huyo alihamia Azam FC mara baada ya msimu kuisha. Katika tukio lililoonekana la kulipiza kisasi, mshambuliaji wa Azam, Prince Dube naye alivunja mkataba, akitaka Kwenda sehemu nzuri zaidi. Azam nao wakaweka kiwango kikubwa cha fidia zilizolipwa na mchezaji huyo na msimu ulipoisha alitangazwa kuwa mchezaji wa Yanga.

Lakini sasa kanuni hiyo haipo tena na FIFA ilihangaika huku na huku kutafuta maoni ya wadau, ambao ni pamoja na Chama cha Wanasoka wa Kulipwa na kufikia uamuzi wa kutoa kanuni za muda zitakazoanza kutumika Januari kabla ya wadau wote kuzikubali.

Hata hivyo, hakukuwepo na uwakilisha wa wanasoka, lakini FIFA ikasema chama cha wanasoka duniani kilikataa kushiriki, kitu ambacho kilikanushwa na FiPro.

SOMA ZAIDI: Kwa Kamwe, Ali: Soka Sasa ni Biashara

Pamoja na FIFA kusema kuwa imezingatia mambo yote yaliyomo kwenye uamuzi wa ECJ, bado inahisi kuwa kanuni mpya zinaweza kupingwa, ikiwa ni pamoja na kuwekewa zuio la muda la kutumika.

Katika uamuzi wake wa kutoa kanuni hizo za muda, FIFA imesema imekubaliana na kipengele cha hukumu kuhusu ukokotoaji wa fidia inayotakiwa ilipwe iwapo kuna ukiukwaji wa mkataba uliofanywa na mchezaji au kocha.

Mahakama hiyo pia imeizuia FIFA kutumia ITC kumzuia mchezaji ambaye amevunja mkataba na klabu yake kwenda sehemu atakayochagua.

FIFA imeona iwapo itabainika kuwa uamuzi wa mchezaji kuvunja mkataba umetokana na kushawishiwa na klabu nyingine, hiyo klabu inayomtaka, pamoja na mchezaji, watawajibika kulipa fidia. Kwa maneno mengine, jukumu la uthibitisho litabakia kwa klabu iliyoathirika.

Kanuni hizi mpya pia zinaeleza kuwa klabu itakayobainika kumshawishi mchezaji kuvunja mkataba bila ya sababu za kimichezo, itafungiwa kusajili kwa vipindi viwili, yaani kipindi cha usajili na dirisha dogo.

SOMA ZAIDI: Wageni Hawakuzi Soka la Tanzania, Wanalitangaza

Pia, imekubaliana na suala la mchakato kuhusu utoaji wa Hati ya Kimataifa ya Uhamisho (ITC). FIFA imesema: “Upande wowote ambao umeathirika kutokana na kuvunjwa kwa mkataba na upande mwingine, utakuwa na haki ya kulipwa fidia.”

Kanuni zapingwa

Tayari chama cha wanasoka wa kulipwa kimeshapinga kanuni hizo za muda na huenda kukawa na mijadala mingi zaidi.

Baada ya Mahakama kutoa hukumu hiyo, ni dhahiri sasa kutakuwa na uwezekano wa wachezaji wengi kuvunja mikataba yao, huku nguvu ya kuamua masuala ya malipo ikihama kutoka mikononi mwa klabu na kwenda kwa wachezaji na mawakala wao.

Pia, kuna uwezekano wa kuwepo na sintofahamu kubwa katika kupanga ada ya uhamisho na suala hilo linaweka uwezekano wa kuanzisha chombo kipya cha kuamua kiwango cha fidia na masuala mengine.

Ndio tumeshaingia kwenye usajili wa dirisha dogo, lakini suala lililozisumbua Yanga na Azam halionekani kama ni muhimu wakati huu ambao FIFA imetoa kanuni za muda na Mahakama imefuta sheria zilizokuwa zinawabana wachezaji kuhama kutoka klabu anayoichezea kwenda klabu nyingine kwa kuvunja mkataba.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts