The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mwisho wa Mwaka Vicoba Vinavunjwa Kwa Furaha: Simanzi, Madeni na Mitafaruku ni Upande Wa Pili wa Vicoba Usiozungumzwa

Wanawake wengi wamejikuta wakipitia kipindi kigumu cha sonona na hata kufikia maamuzi ya kujiua kwa sababu ya Vicoba

subscribe to our newsletter!

Mwisho wa mwaka huwa na shamrashamra na shughuli nyingi, na moja ya sababu ya shughuli hizi ni uvunjaji wa Vicoba. Katika maeneo mengi ya Tanzania vikundi mbalimbali vya Vicoba vimejitokeza kupongezana, ni msimu wa kufurahia matunda ya kazi yao.

Sehemu kubwa ya washiriki katika Vicoba huwa ni wanawake, na wengi wameonekanana  katika sare zao wakisherehekea pamoja, picha zikitumwa katika makundi sogozi mbalimbali. Huu ni upande wa kwanza wa Vicoba, upande unahusiana na uwezo wa kuwasaidia kinamama wengi kujikwamua kiuchumi na kujenga uwezo wa kuwa na akiba.

Hata hivyo, katikati ya sherehe hizi na picha picha, kuna upande wa pili wa Vicoba ambao hauzungumzwi sana. Kwa kawaida Vicoba hujumuisha kuhifadhi fedha kulingana na makubaliano ya wanachama na ikitokea mtu anahitaji kukopa, hukopeshwa na kutakiwa kurejesha fedha aliyoikopa kwa riba.

Riba! Imezua matatizo mengi. Imesababisha utitiri wa madeni ambayo imepelekea baadhi ya wanaocheza vikoba kushindwa kurejesha fedha.

Upande wa pili wa Vicoba

Nuru Hassan [43] ni mama wa watoto watatu anayejishughulisha na biashara ya kuuza maandazi. Alianza kucheza vicoba kwa zaidi ya miaka minne ila kwa sasa anajutia. Nuru, alikopa zaidi ya milioni mbili akiamini itakuwa rahisi kurudisha kwenye marejesho yake. Hata hivyo mtaji wake ulikata na mambo yakamwendea mrama.

‘’Mtaji ulivyokata nikaanza kudhalilika.’’ Nuru aliiambia The Chanzo wakati wa mahojiano yaliyofanyika kwa njia ya simu akiwa nyumbani kwake. “Ilikuwa inafikia wakati nakosa rejesho, kiukweli nilikuwa nikihangaika sana.’’

Mara baada ya mtaji kukata na kushindwa kurejesha rejesho Meneja, Mwalimu wa Vicoba na wanachama wenzake walimwendea nyumbani kwake, kila mtu alianza kuongea maeneo yake.

“Nilibaki mimi kama mimi, niko peke yangu,’’ alieleza. “Wana kikundi walikuwa hawana huruma hata kidogo, walianza kutoa vitu ndani wakachukua masofa yangu, televisheni na kuondoka.’’

Nuru alifikia mahali kwa kuwaza kunywa sumu sababu ya madeni, madhila haya aliyoyapitia, yamemsababishia ugonjwa wa moyo hali inayomuumiza sana mpaka leo.

‘’Sasa hivi vicoba nimeacha najiwekeza mwenyewe. Natoa wito, kwa mtu ambaye unachukua mkopo anatakiwa afanye biashara . Uwe na biashara maalum ndio ukachukue mkopo .Hivi hivi ,unasema eti ndio nianze yaani utadhalilika .Najuta kwa sababu nimefilisiwa.’’ alisisitiza Nuru.

Tafiti mbalimbali zinaonesha Watanzania wengi wanategemea njia zisizo rasmi katika kukopa, moja ya utafiti unaonesha hili ni ule wa Finscope wa mwaka 2023. Utafiti huo unaonesha kwamba asilimia 67 ya Watanzania wanapata mikopo yao kutoka kwa watu binafsi, ikifuatiwa na vikundi vya akiba kwa asilimia 17, na kisha mitandao ya simu kwa asilimia 6, mabenki yakiweza kukopesha asilimia 3 tu ya Watanzania.

Hii ikimaanisha Watanzania hawa wanaenda kukopa huku sababu ndio sehemu wanazozifikia na zenye kuwafikia hasa wafanyabiashara wadogo. Hata hivyo uzoefu unaonesha kuna wimbi kubwa la wanawake wanaojikuta kwenye hali mbaya kuliko ya mwanzo kutokana na Vicoba.

Mwajuma Hassan [23] mama wa mtoto mmoja alianza kucheza vicoba tangu mwaka 2019. Alikuwa akifanya biashara ya kuuza madera ya wanawake . Alitamani biashara yake ikue ,akapata wazo la kwenda kukopa fedha na kufanikiwa kukopa kiasi cha shilingi milioni moja na nusu.

Kwa bahati mbaya, baada ya kukopa biashara hazikumuendea vizuri. Hali iliyo pelekea kujikuta kwenye wakati mgumu kwa kushindwa kupeleka rejesho vicoba.

“Nilikwama rejesho sikuwa na sehemu ya kupata fedha. kwa hiyo ikanibidi nikakope pesa ya riba.’’ Alieleza Mwajuma wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Nilikuwa nipo kwenye hali ngumu sana, nikajikuta kila ninapo shindwa kupeleka rejesho wanakuja kunibebea kitu kinachoendana na pesa niliyokopa. ‘’

“Mwisho wa siku walikuja wana kikundi wenzangu nyumbani. Wakaja kunifanyia fujo pamoja na mwalimu.Hakuna aliyekuwa akinielewa wanachohitaji ni rejesho. Wakachukua vitu vinavyoendana na ile pesa ninayo daiwa .Nilifilisiwa kitanda, kabati la nguo, kabati la vyombo ,masofa , Televisheni ,Deki yaani vyombo vile vya thamani vyote walivichukua mpaka simu yangu ya kupangusa walinipokonya,‘’ aliongeza.

Mama mwenye mtoto mmoja Hamda Ramadhan [23] aliiambia The Chanzo ,alijiingiza kwenye uchezaji wa vicoba mwaka 2020. Alikukwa akijishughulisha na biashara ya uuzaji wa sabuni ya unga na sabuni ya maji. Kulingana na aina ya biashara yake alionelea ni vyema kukopa pesa kujitanua kibishara.

Wakati huo, biashara zake zilikuwa zikumuendea vizuri , kulazimika kukopa kiasi cha shilingi milioni moja na laki tano ambayo alipaswa kurejesha rejesho kila wiki. Haikuwa rahisi kwa yeye kurejesha kiasi hicho alikosa.

‘’Nilikwama rejesho baada ya kukwama wakaja kwangu kunifilisi’’ alieleza Hamda .’’Wakasema kwamba wanakata pesa zao zote zilizo bakia . Wakabeba friji ,kitanda na godoro lake na redio. Iliniumiza sana kiukweli kiasi kwamba nilikata tamaa ya kuendelea kuishi .’’

‘’Nilikuwa na vitu vyangu mwenyewe. Ni heri ningekuwa nacheza mchezo napokea hela narudisha vitu vyangu kuliko kukopa pesa za watu za riba . Nashauri wanawake wenzangu ikiwa watakuwa wana uhakika wa rejesho kutokana kazi wanazo zifanya wanaweza kucheza vicoba . Ikiwa hauna uhakika ni heria kuacha .’’

Ukiacha pilika pilika katika urejeshaji madeni kuna suala la dhuluma kama ambavyo Amina Lema (38) mama wa watoto wawili anavyoeleza wakati akiendelea na shughuli zake katika saluni yake iliyopo sabasaba Dodoma.

Amina anaeleza kuwa alikuwa kwenye Vicoba kwa muda wa miaka mitano hata hivyo siku ambayo kikoba kilipaswa kuvunjwa Amina hakupokea ujumbe wowote.

‘’Mimi walijifanya wamenisahau kunitumia ujumbe siku ya kwenda kuvunja kikoba,’’ alieleza Amina.’’ Sio mimi pekee tulikuwa kama watu wanne wanasema kwamba walitusahau . Mwisho wa siku kikoba kikavunjwa. Hata shilingi kumi mimi sijawahi kuchukua ya kikoba .Nakuja namuuliza mwenyekiti hana cha kujibu ,katibu hana cha kunijibu, mweka hazina hana cha kunijibu.’’

‘’Iliniathiri sana , kwa sababu, nilipanda hisa zangu miaka mitano mizima. Halafu leo naletewa sababu zisizo namsingi .Mimi ile pesa nilikuwa na malengo nayo, nilijinyima. Nasema pesa yangu naipanda hisa, mwisho wa siku nije kuvuna kile ninacho kihitaji kwa sababu nina malengo nacho milioni mbili ni pesa kubwa sana.’’ aliongeza

Afya ya akili

Hivi karibuni, tumeshuhudia matukio ya kuogofya kwa wanaocheza vicoba, taarifa nyingi zinaripotiwa ni za kujitoa uhai kwa wanaoshindwa kurejesha marejesho ya vicoba.  Matukio kama hayo tumeshuhudia mfano huko Iringa ambapo, Enea Mkimbo (55) alijinyonga baada ya kufuatwa na wanakikundi kwa ajili ya kulipa deni lake. Pia Ndatu, Arumeru, Johari Tarimo (32) alikunywa sumu na kueleza sababu kubwa ni deni la Vicoba la shilingi milioni moja na laki moja.

Akizungumza juu ya hali hii inayowapelekea watu kufikia kujidhuru mtaalamu wa magonjwa ya akili katika hospitali ya Mirembe Sadiki Mandali alieleza hali hii inafikia hapo kwa sababu ya sonona.

‘’Ukiangalia kwa asilimia kubwa wanawake wanapata shida ya sonona kubwa . Wanawake wanakuwa kwenye hatari kubwa kutokana na changamoto za maisha,’’ alieleza Dk.Mandali.

‘’Mpaka mtu amejiua, mara nyingi alishajaribu kujiua,‘’ alieleza. “Na sana, sana wanawake tafiti zinaonesha hawatumii njia zile za moja kwa moja ambazo ni hatarishi. Wanatumia kama sumu ambazo ni rahisi kulewa au akatumia vidonge. Kwa hiyo, ni tofauti na mwanaume ambaye atachukua njia ya kutaka kujiua kabisa.’’

Dk.Mandali anasisitiza mtu akifikia hali ya kupata sonana ni muhimu akapata wasaa wa kuongea na ndugu na jamaa ili kuweza kupata suluhu mbadala badala ya kuficha mambo.

Moja ya kitu ambacho The Chanzo iliweza kung’amua wakati wa utafiti wa Makala hii, ni kuwa shida kubwa huanzia katika uwelewa wa masuala ya fedha. Wengi wakitumia fedha za mikopo bila kuwa na vyanzo endelevu vya kipato au kuongeza matumizi yao kupita kiasi pindi tu wanapopata mikopo.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts