Watu mbalimbali leo, Disemba 31, 2024, wameeleza masikitiko yao kwamba wanatarajia kuufunga mwaka bila ya raia wenzao waliotoweka katika mazingira ya kutatanisha kurudi na kuungana na familia na wapendwa wao, huku jina la Deusdedith Soka, mwanaharakati na kada wa chama cha upinzani CHADEMA, likiorodheshwa na walio wengi.
Soka, kijana machachari aliyekuwa na maono makubwa kuhusu hatma ya taifa lake, alitoweka katika mazingira ambayo chama chake kimeyaelezea kama “utekaji” mnamo Agosti 18, 2024, maeneo ya Temeke, Dar es Salaam, akiwa na wenzake wawili, Jacob Mlay pamoja na Frank Mbise, na kutokupatikana mpaka leo.
Ni moja kati ya visa vingi vya “utekaji” vilivyoikumba Tanzania kwenye mwaka huu unaoishia wa 2024, hali iliyompelekea hadi Rais Samia Suluhu Hassan kujitokeza hadharani kulaani na kukemea vitendo hivyo, akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki kudhibiti hali hiyo.
Tukiwa tumebaki na masaa machache kabla ya kumaliza 2024, tunakuwekea hapa baadhi ya visa vikuu vya “utekaji” vilivyoishitua Tanzania kwa mwaka huo, vikizua mijadala mingi na mikubwa, vikiwajaza Watanzania hofu, na kuibua sauti za uwajibikaji na upatikanaji wa haki.
Ali Mohamed Kibao
Ali Mohamed Kibao, mjumbe wa sekretarieti ya CHADEMA, aliripotiwa kutekwa hapo Septemba 6, 2024, na mwili wake kupatikana Ununio, Dar es Salaam, Septemba 7, 2024, akiwa ameuwawa na kuharibiwa vibaya.
Ni tukio litakaloendelea kubaki kwenye kumbukumbu ya Watanzania wengi, hususan kwa namna Kibao alivyotekwa, akiwa kwenye basi akielekea nyumbani kwake Tanga, na watu waliojitambulisha kama polisi, ambao, hata hivyo, hawakumpeleka kituo chochote cha polisi.
SOMA ZAIDI: Usikubali 2024 Ipite Bila Kuzisoma Habari Hizi Tulizofanya Hapa The Chanzo
Kinachoacha maswali mengi miongoni mwa Watanzani ni ukweli kwamba licha ya Rais Samia Suluhu Hassan kulaani kitendo hicho hapo Septemba 8, 2024, na kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama vifanye uchunguzi, mpaka wakati wa kuchapisha habari hii hakukuwa na taarifa yoyote kuhusiana na hatua za uchunguzi huo.
Akizungumzia tukio hilo hapo Disemba 23, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliwaomba Watanzania kuwa “wavumilivu” kuhusiana na tukio hilo, akiwahakikishia kwamba mamlaka husika zinaendelea na uchunguzi kupata ukweli wote kuhusu suala husika.
Edgar “Sativa” Mwakabela
Edgar Mwakabela, maarufu kama Sativa, ni mwathirika mwingine wa vitendo vya utekaji vilivyoshitua Tanzania mwaka huu wa 2024, na ambaye, kama kwenye kisa cha Kibao, hatma ya uchunguzi wake kulipatia suala husika ufumbuzi wa kudumu ni ya kusuasua.
Sativa, 27, mkazi wa Mbezi, wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, alidaiwa kutekwa akiwa jijini humo mnamo Juni 23, 2024, kisha akapatikana Juni 27, 2024, katika Hifadhi ya Taifa Katavi akiwa na majeraha, likiwemo lile la risasi.
Sativa amelilaumu Jeshi la Polisi kuhusika na kutekwa na kuteswa kwake, akisema anawatambua watu waliotekeleza uhalifu huo, na endapo kama polisi wataonesha utayari wa kuhitaji afanye hivyo, basi atafanya.
Kwa upande wake, Jeshi la Polisi limekuwa likikanusha taarifa zote za kuhusika kwake na vitendo vya utekaji. Kuhusu uchunguzi, polisi pia wamekuwa wakieleza kwamba matukio yote ya utekaji yanachunguzwa na umma utapatiwa taarifa muda muafaka ukiwadia.
Soka na wenzake
Kama ambavyo tumedokeza hapo juu, Soka, na wenzake wawili, Mlay na Mbise, walitoweka katika mazingira ya kutatanisha na ambao mpaka wakati wa kuchapisha habari hii hatma yao ilikuwa bado haijajulikana.
SOMA ZAIDI: Kwa Watanzania Walioipeperusha Vyema Bendera ya Taifa 2024, Kongole
Wakiandika kwenye mtandao wa X, zamani Twitter, watu mbalimbali wameelezea simanzi zao za kulazimika kuuaga mwaka 2024 bila kujua hatma ya kijana huyo machachari, wanayemuhusisha na mapambano ya kupigania haki, na wenzake hao wawili, kutojulikana.
Hatua mbalimbali zimechukuliwa kuhakikisha vijana hao wanapatikana wakiwa hai au wamekufa, ikiwemo ile ya kwenda mahakamani kuliamrisha Jeshi la Polisi, linalodaiwa kuwakamata kwa nguvu, liwaachie. Mahakama, hata hivyo, ilisema kwamba hakuna ushahidi wa kutosha kwamba polisi wamehusika na kutoweka kwa vijana hao.
Nondo wa ACT Wazalendo
Abdul Nondo, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya chama cha upinzani cha ACT Wazalendo alidaiwa kutekwa mnamo Disemba 1, 2024, maeneo ya Stendi ya Mabasi ya Magufuli, jijini Dar es Salaam, majira ya 11 asubuhi wakati akitokea mkoani Kigoma.
Masaa takribani 18 baadaye, baada ya taarifa kuhusu namna alivyokamatwa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, Nondo, mwanasiasa kijana na machachari, alidaiwa kutelekezwa na watekaji wake maeneo ya Coco Beach, huku akiwa ameumizwa sana.
Mpaka wakati wa kuchapisha habari hii, Nondo alikuwa bado hajarudi kwenye shughuli zake za kila siku za siasa, kwani bado alikuwa anaendelea kujiuguza kutokana na maumivu makali aliyopatiwa na watekaji wake, waliomuonya kuhusu tabia yake ya kukosoa Serikali na viongozi wake.
Kiongozi BAWACHA
Mnamo Oktoba 19, 2024, Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake CHADEMA Taifa (BAWACHA), Aisha Machano, aliripotiwa kuwa mwathirika mwingine wa vitendo vya utekaji, akidaiwa kutekwa maeneo ya Kibiti, Pwani.
SOMA ZAIDI: Kwa Watanzania Waliofariki 2024, Tunawakumbuka na Kusherehekea Maisha Yenu
Aisha alidaiwa kutekwa, kupigwa, kuvuliwa nguo huku akirekodiwa na kisha ya kutupwa porini, akiokolewa na wasamaria wema waliompa msaada ambapo baada ya hapo alipoteza fahamu na aliposhtuka alikijuta yupo hospitali ya Mwananyamala, alisimulia kada huyo wa CHADEMA.
Aisha alisema kwamba watu hao waliomteka walikuwa wakimhusisha yeye na tukio la uchomaji wa vitenge ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan aliwapatia wanawake wa CHADEMA kama zawadi mwaka jana, 2024.
Aliyechoma picha
Shadrack Chaula, kijana mwenye umri wa miaka 24, mkazi wa kijiji cha Ntokela, wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, alidaiwa kutekwa Agosti 2, 2024, na mpaka sasa haijulikani yupo wapi.
Kutoweka kwa Chaula, aliyekuwa akiweka maoni yake kwenye mtandao wa TikTok, kulikuja siku chache baada ya Mahakama kumuachia huru baada ya Watanzania kumlipia faini ya Shilingi milioni tano aliyotakiwa kulipa baada ya kupatikana na makosa ya kimtandao.
Kesi yake ilikuwa maarufu hapa nchini kwa sababu awali Chaula alikamatwa kwa tuhuma za kuchoma picha ya Rais Samia Suluhu Hassan. Ni kesi iliyoibua hisia na shauku kubwa miongoni mwa Watanzania, na kuwasukuma kumchangia fedha hizo ili aepukane na adhabu ya kifungo jela.
Bila shaka, visa vingi zaidi ya hivi vinavyohusiana na utekaji viliripotiwa kwenye mwaka huu unaoishia wa 2024, na ni ngumu kuviweka vyote hapa.
Kwenye makala maalum ambayo tumeifanya hapa The Chanzo, iliyopewa kichwa cha habari Nani Aliyewateka, Kuwapoteza Watanzania Hawa? tumeangazia vilio vya ndugu na familia za Watanzania waliofikwa na kadhia hii, na ambayo tungekusihi sana kutenga muda na kuitazama.
Maoni ya Watanzania wengi ni kwamba watu wote waliotoweka katika mazingira ya kutatanisha wanapaswa kurudi kuungana na familia na wapendwa wao, ambao wameeleza kwamba wako tayari kuwapokea hata kama wakiwa wamekufa.
Watanzania pia wanataka kuona vitendo hivi vinakoma kwani vinawajaza hofu na kutishia usalama na haki yao ya kuishi kama raia.
Njia moja ambayo Watanzania wanaamini inaweza kufanikisha hilo ni kwa kuwepo kwa uwajibikaji dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo hivi, kwamba wasakwe, wakamatwe, na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili haki ichukue mkondo wake.
Je, 2025 itashuhudia mwisho wa vitendo hivi, na wahusika wake kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria? Muda, wabobezi husema, una majibu ya maswali yote!
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dodoma. Unaweza kumfikia kupitia jackline@thechanzo.com.
One Response
Kuna baadhi ya watu ambao hawajaonekana katika andiko Hilo ambao nao walipitia sekeseke hili la UTEKAJI, mfano Dioz Kipanya, Kiongozi wa CHADEMA ambaye hajapatikana Hadi sasa