The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tanzania Inahitaji Wachezaji Wenye Moyo wa Messi

Wanamichezo wa aina hii wanaoona thamani yao na kukumbuka kuwa kumbe wanaweza kutumia thamani yao kurudisha furaha na tabasamu kwa mamilioni ya watu duniani.

subscribe to our newsletter!

Rais wa Marekani anayeondoka madarakani, Joe Biden, amemtunuku mshambuliaji na nahodha wa Onter Miami, Lionel Messi, tuzo ya juu ya kirais, akiwa mmoja wa viongozi bora 19 waliotunukiwa.

Tuzo hiyo kubwa kwa taifa la Marekani huenda kwa watu binafsi ambao wameonyesha mfano kwa kuwa na mchango mkubwa kuwezesha jamii kiuchumi, maadili, au usalama katika taifa la Marekani, amani duniani, au mambo mengine ya kijamii yanayoonekana au mchango kwa jamii au sekta binafsi.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Argentina anatoa mchango wake katika masuala ya kiafya, programu za elimu kwa watoto kwa kutumia mfuko wake wa Leo Messi na ni balozi wa Shirika la Mfuko wa Kimataifa wa Dharura wa Umoja wa Mataifa (Unicef).

Katika siku za hivi karibuni, wachezaji kadhaa walioulizwa kuhusu uhusiano wao na Messi walitoa ushuhuda wa jinsi mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona anavyoweka mbele masuala ya kusaidia jamii.

Wachezaji hao walieleza jinsi walivyoomba kubadilishana jezi na mchezaji huyo baada ya mechi na jinsi alivyoshughulikia maombi yao. Mmoja alieleza jinsi Messi alivyochukulia kwa uzito suala hilo.

SOMA ZAIDI: FIFA Yatoa Kanuni Mpya za Uhamisho wa Wachezaji. Klabu Zetu Zinafuatilia?

Hata kabla hajaenda kumkumbusha baada ya mechi kuisha, Messi alitangulia kwenye varanda ya kuelekea vyumbani na kumsubiri, huku akiwa ameshikilia jezi mbili. Mchezaji huyo alivyofika alikuta Messi ameshikilia jezi yake ikiwa na saini na wachezaji wote wa Barcelona na nyingine ya kawaida.

Messi akamwambia anampa jezi moja kwa ajili ya kumbukumbu yake na nyingine kwa ajili ya kwenda kuipiga mnada, ili fedha zitakazopatikana ziende kusaidia wahitaji katika eneo alilotoka.

Mwingine ni Ronaldinho ambaye pia alimuomba jezi Messi na akapewa jezi kama hiyo na kuambiwa akaipige mnada kwa ajili ya kusaidia watu wa eneo lao. Ronaldinho hakutaka kupoteza kumbukumbu hiyo na akamwambia kuwa asingeipiga mnada, ndipo Messi akamtumia nyingine na akawasiliana na watu wanaopiga mnada vifaa vya watu maarufu.

Siku ya pili Ronaldinho alipigiwa simu na madalali kadhaa wakitaka jezi hiyo kwa bei mbaya, ndipo alipogundua kuwa Messi si mtu wa kawaida katika kusaidia jamii.

Kusaidia jamii

Wanamichezo wa aina hii wanaoona thamani yao na kukumbuka kuwa kumbe wanaweza kutumia thamani yao kurudisha furaha na tabasamu kwa mamilioni ya watu duniani.

SOMA ZAIDI: Kukuza Netiboli Tanzania, Juhudi Zinahitaji Kurejesha Mapenzi, Unazi kwa Mchezo Huo Mkakati kwa Taifa

Hivi sasa hapa nchini, baadhi ya wanasoka wameanza harakati hizo za kufungua mifuko ya kusaidia jamii, ingawa michango yao kwa jamii haijawa na muonekano huo mkubwa kiasi cha mamlaka kutambua jitihada zao.

Tumeona wachezaji nyota kama Mbwana Samatta, Bakari Mwamnyeto na Dickson Job wakiandaa mechi za hisani kwa ajili ya kutunisha mifuko yao ya kusaidia jamii kila wakati msimu unapoisha.

Lakini mifuko yao ya kusaidia jamii husikika pale wanapoandaa mechi za kuchangisha fedha ili mifuko hiyo iweze kufanya kazi zake. Baada ya mechi hizo ambazo hufanyika baada ya msimu kuisha, husikii tena shughuli za mifuko hiyo wala fedha zinakokwenda.

Inawezekana kabisa kwamba mifuko hiyo inafanya kazi kubwa ya kusaidia jamii, lakini haiambatani na habari zinazopewa uzito mkubwa na vyombo vya habari zinazoweza kuonyesha jinsi wachezaji hao wanavyoigusa jamii.

Kama mifuko hiyo inaigusa jamii kwa kiwango hata kidogo, ni muhimu kwa wachezaji hao, au wanaoiendesha mifuko hiyo, kufikiria upya mikakati yao ili kazi zake zitambuliwe.

Ni dhahiri kuwa mifuko hiyo haiwezi kutatua matatizo yote ya wahitaji, lakini kadiri shughuli zao za kusaidia wahitaji zinavyotangazwa, ndivyo jamii inavyojua kuna wahitaji na kuona wajibu wa kuisaidia kwa njia yoyote, ikiwemo hiyo ya kuhudhuria mechi hizo za hisani, tena kwa viingilio vya juu au kutuma fedha kwenda katika akaunti ambazo zimetangazwa na mifuko hiyo.

SOMA ZAIDI: Ziko Wapi Hamasa za CHAN 2025?

Watu maarufu wanafuatiliwa sana na jamii na hivyo wanapofanya mambo mazuri kwa jamii na jamii ikajua, ujumbe unaokwenda kwao huwaingia sana akilini wananchi na hivyo kuunga mkono juhudi zao.

Na inapofikia taasisi kama Ikulu ikatambua mchango huo na kuwatunuku wenye mifuko hiyo kama Rais Biden alivyotambua mchango wa Messi, basi ujumbe huenda mbali zaidi na jamii hutambua kuwa kumbe shughuli zao za kutunisha mifuko yao, hazilengi katika kujipatia chochote bali kusaidia wahitaji.

Tunahitaji akina Lionel Messi wengi zaidi wanaotambua thamani yao ya sasa, kuangalia walikotoka na nini wanachoweza kufanya kusaidia jamii inayoishi katika mazingira yanayofanana na waliyokulia.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts