Vitongoji vyote vya wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam kwa sasa vinashuhudia mashindano ya Super Cup yaliyopewa majina tofauti kulingana na wadhamini wa eneo husika.
Ni mashindano ambayo yamewapa wakazi wa wilaya hiyo gumzo tofauti na lile la kawaida la Simba na Yanga kuanzia asubuhi hadi jioni. Ni mashindano ambayo yamewapa wakazi wa Ilala burudani nyingine inayowafanya wabakie maeneo yao badala ya kuifuata kilomita kadhaa, tena wilaya nyingine za jiji hili.
Lakini kutokana na kushirikisha klabu ambazo hazijasajiliwa, mashindano haya hayana uasilia wa mitaa ya vitongoji hivyo, ingawa sehemu kubwa ya wachezaji wanaoshiriki ni wale wanaotoka maeneo husika, tofauti na mashindano mengine ya huku Uswahilini ambako timu nzima hujaa wachezaji wa kukodi.
Haya ni mashindano ambayo yanaratibiwa na Chama cha Soka cha Ilala (IDFA) na kwa kiasi fulani, yamechukua nafasi ya mashindano makuu ya chama hicho yanayoitwa Ligi ya Wilaya, ambayo ndiyo shughuli kuu ya kwanza ya chama cha wilaya. IDFA inayaelezea mashindano haya kama njia ya kukuza vipaji vya vijana walio ndani ya wilaya hiyo.
Lakini ukifika kushuhudia mechi za mashindano haya huku Uswahilini kwetu huwezi kuiona nia hiyo ya kukuza na kutambua vijana. Unaona vijana waliokomaa wanaokaribia kustaafu baada ya kukosa kwa muda mrefu bila ya kupata timu za madaraja ya juu.
Na wengi wao ni wale tunaokutana nao kwenye mechi za wachezaji wastaafu ndiyo maana nashangaa mashindano hayo kupachikwa jina la kukuza vipaji.
SOMA ZAIDI: Tanzania Inahitaji Wachezaji Wenye Moyo wa Messi
Nia
Nia ya IDFA ni njema kwamba angalau kuna shughuli za mpira katika kila kitongoji cha wilaya ya Ilala kama moto wa mashindano hayo unavyosema Ilala Ni Soka. Ni soka kweli linachezwa kila kona ya Ilala na wakazi wake wamesogezewa burudani ya soka barazani kwao; hawahitaji kwenda mbali kuburudika.
Lakini IDFA, na soka kwa ujumla, itanufaikaje na mchezo huo kuchezwa kila kona kwa mashindano ambayo hayana malengo halisi ya kimpira ya kuendeleza soka? Ndio, yanatangaza soka lakini nhayaendelezi soka.
Hao vijana walio kwenye vitongoji hivyo, hawapati nafasi ya kucheza kwenye timu zilizojaa wachezaji wenye umri mkubwa na kwa kuwa timu ni za kukusanyana, hazina mafunzo mazuri kutoka kwa kocha.
Mtu anayeitwa kocha ndio yule anayekutana na wachezaji uwanjani na kazi yake ni kupanga timu, kufanya mabadiliko ya wachezaji na kutoa mazungumzo marefu wakati wa mapumziko!
Haya hayana tofauti na mashindano mengine yanayoitwa ya ndondo, au “Kombe la Mbuzi.”
Pengine ilikuwa ni wakati muafaka kwa IDFA kufikiria kuweka kanuni zitakazowahakikishia vijana nafasi ya kucheza na pengine ndio mashindano ambayo chama hicho kinaweza kuwapatia fursa ya kufundisha kwa makocha wanaofuzu mafunzo ya awali.
Na hilo litaweza kufanyika kama mashindano hayo yatashirikisha timu zilizosajiliwa, na hivyo kuwa na uwezo wa kuzifuatilia na hata kuwa na programu nazo kwa ajili ya maendeleo ya mchezo huo.
SOMA ZAIDI: FIFA Yatoa Kanuni Mpya za Uhamisho wa Wachezaji. Klabu Zetu Zinafuatilia?
Nimezungumzia Super Cup ya Ilala kwa sababu inawakilisha vyama vingine vyote vya wilaya vinavyotoa kibali cha mashindano kama hayo wakati mashindano yao halisi ya kikatiba.
Ni muhimu kwa vyama kufikiria jinsi ya kuingiza programu zake za maendeleo katika mashindano yanayoandaliwa na wadau waliomo ndani ya wilaya zao kwa kulazimisha kuwemo kanuni zinazoweza kukuza mpira.
Wakati wa kuendesha mashindano kwa mtindo wa bora liende hauna budi kusahauliwa na badala yake kuwe na mashindano yanayoweza kuongeza thamani katika mchezo huu maarufu nchini.
Na akili hiyo yakuongeza thamani ni lazima ianze kwa kulazimisha wadau wajue umuhimu wa maendeleo badala ya kuwa na mashindano ya “ili mradi” au yanayoenda kwa motto wa “hivi ndivyo watu wanavyotaka.”
Shule za soka
Hivi sasa wadau wa soka wameanzisha shule za soka kila sehemu. Watoto wadogo wenye umri wa kuanzia miaka minane hadi 20 wanafundishwa mpira mara tatu kwa wiki, au hata wiki nzima. Nina uhakika hata wilaya ya Ilala ina shule hizi karibu katika kila kitongoji.
Baadhi zina walimu waliosomea kozi za awali za ukocha na baadhi zinafundishwa na watu waliowahi kucheza mpira wakaishia ngazi za chini.
SOMA ZAIDI: Kukuza Netiboli Tanzania, Juhudi Zinahitaji Kurejesha Mapenzi, Unazi kwa Mchezo Huo Mkakati kwa Taifa
Hawa wachezaji walio na umri chini ya miaka 20 ndio wanaweza kuongeza thamani kwenye haya mashindano na nina uhakika yanaweza kuvutia watu wengi iwapo vijana wadogo wanaofundishwa katika shule hizi na wanaotoka kwenye vitongoji hivi ndio watapewa nafasi zaidi.
Hapa ndipo utashuhudia timu zenye wachezaji waliokaa pamoja muda mrefu na wanaoitana majina halisi uwanjani, si wale wanaoitana Fadha (father) kutokana na kukutana uwanjani.
Hapa ndipo walimu waliomaliza mafunzo ya awali watapata nafasi ya kuongoza timu mashindanoni ili wanaporudi kutafuta elimu kubwa zaidi wawe wamepata kitu halisi uwanjani baada ya kufundishwa nadharia.
Yapo mengi ya kufanya kuyapa thamani mashindano haya iwapo IDFA na vyama vingine vitakuna vichwa zaidi kutaka kunufaika na utitiri wa mashindano katika wilaya zao.
Hata hivyo, IDFA imefanya kazi kubwa hadi sasa ya kushirikiana na wadau kuhakikisha soka linachezwa katika kila kitongoji. Kilichobakia ni kuyapa thamani zaidi ili yaakisi kauli mbiu ya mashindano hayo, ile ya Ilala Ni Soka.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
One Response
Ndugu muandishi,
Umeandika vyema sana, nadhani hili IDFA wanajitahidi sana. Changamoto iliyopo ni vilabu vyenyewe, na ndio maana IDFA wanaanza Sasa na hatua hii Ili kufikia lengo na maana halisi ya uanzishwaji wa IDFA SUPER CUP, tuwatie moyo na ni vyema tufike katika ofisi zao ili kupata mantiki nzima na changamoto wanazokutana nazo kama Chama cha Mpira wa Miguu.