The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Yanga Haikufanya Uamuzi Sahihi kwa Wakati Sahihi Ilipoamua Kuachana na Miguel Gamondi

Timu ilikuwa na mechi muhimu za Ligi ya Mabingwa katika kipindi kisichopungua wiki moja kuanzia siku ambayo Gamondi alitimuliwa.

subscribe to our newsletter!

Kufanya maamuzi sahihi, kwa wakati sahihi, ni kitu muhimu sana katika maisha kwa sababu mambo yote yanakwenda kadiri yanavyotakiwa. Waweza kufanya uamuzi sahihi, lakini wakati usio sahihi, ukaibua tatizo kubwa.

Ndivyo uongozi wa klabu ya Yanga ulivyofanya mwaka huu wakati timu ikielekea kuanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Zikiwa zimebakia wiki mbili kabla ya kuanza michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu, Yanga ilipoteza kwa mbinge mechi yake ya Ligi Kuu ya Bara dhidi ya Azam FC. Ni mechi ambayo Yanga ilionyesha ubora wa juu, lakini ilimpoteza beki wake Ibrahim Bacca mapema.

Ikaruhusu bao wakati ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja. Lakini upungufu huo haukuifanya Azam itawale mchezo. Ilishambuliwa kwa muda wote kana kwamba Yanga ndio ilikuwa na wachezaji wengi zaidi. Haikuweza kusawazisha na hicho kikawa kipigo cha kwanza msimu huu.

Kama haitoshi ikakutana na Tabora United. Siku hiyo iliwakosa mabeki wanne wanaoanza kikosi cha kwanza. Hakuwepo Dickson Job, Yao Kouasi, Chadrack Boka na Bacca na hivyo kocha Miguel Gamondi akalazimika kumpanga Aziz Andambwile kushirikiana na Bakari Mwamnyeto katikati ya ngome.

SOMA ZAIDI: ‘Ilala ni Soka’ Ina Lengo Zuri Kukuza Soka Ngazi ya Vitongoji. Lakini Kuna Kasoro za Msingi

Lakini Andambwile akaumia dakika ya nane na hivyo kocha kulazimika kumrudisha nyuma Khalid Aucho ashirikiane na Mwamnyeto. Hilo halikuweza kutibu tatizo la kutokuwepo kwa Job na Bacca na matokeo yake ikafungwa mabao 3-1, kipigo cha kwanza kikubwa kwenye Ligi Kuu katika miaka ya karibuni.

Uongozi ukaanza kufuatilia mwenendo wa kocha na kuomba kikao naye siku hiyohiyo, kitu ambacho hakiwezi kutoa majawabu ya tatizo. Habari zinasema Gamondi akakataa kuhudhuria kikao hicho, jambo ambalo ni sahihi kabisa kwa kuwa alitakiwa apewe muda wa kutafakari na kuwasilisha ripoti ndipo ijadiliwe na kutoa maamuzi.

Siku chache baadaye uongozi ukatangaza kumtimua bila ya kueleza sababu hasa za kufikia makubaliano ya kutengana. Lakini habari zinasema kitendo chake cha kukataa kuhudhuria kikao baada ya mechi ndicho kilichochukuliwa kwa uzito.

Lakini habari nyingine ambazo pengine zilivujishwa, ama zilitokana na picha ziolizokuwa zinaenea mitandaoni, ni kwamba Gamnondi aliwaacha huru sana wachezaji kufanya starehe na kwamba hiyo ndiyo ilisababisha viwango vya baadhi yao kuporomoka.

Vipigo viwili mfululizo havikuchukuliwa kuwa ni matokeo ya mpira wa miguu, bali kulionekana kuna tatizo la kuporomoka viwango vya baadhi ya wachezaji kulikosababishwa na malezi ya Gamondi kuwaachia huru wachezaji kustarehe na kujumuika nao kwenye starehe.

SOMA ZAIDI: Tanzania Inahitaji Wachezaji Wenye Moyo wa Messi

Hali ya kujituma ambayo wachezaji waliionyesha katika mechi dhidi ya Azam licha ya kuwa pungufu haikuangaliwa, yakaangaliwa matokeo. Kukosekana kwa wachezaji wanne muhimu kwenye safu ya ulinzi na kuumia kwa Andambwile hakukuonekana tatizo, bali matokeo.

Ndipo uongozi ulipotangaza uamuzi ambao unaweza kuwa sahihi wa kumtimua Gamondi na kusaka kocha mwingine aiongoze Yanga katika mechi za mwanzo za hatua ya makundi kwa kuanza na Al Hilal siku saba baada ya Gamondi kutimuliwa.

Mahusiano mazuri

Gamondi alishajenga mahusiano mazuri na wachezaji ambao wakati mwingine walionekana wanamchukulia situ kama rafiki, bali mzazi wao na kuna uwezekano kuna mechi walijituma kwa ajili yake.

Ramovic alitakiwa kwanza aanze na kujenga hiyo saikolojia kwa wachezaji waliompoteza rafiki yao, waliokwishaelewa falsafa yake, waliokwishaelewa huwa anataka nini na wakati gani, waliokwishaelewa huchukulia vipi mapungufu yao.

Ramovic akatakiwa ajenge urafiki huo, ajenge kueleweka huko, ajenge falsafa yake na ieleweke kwa wachezaji, ajenge kueleweka nini anafanya pale mchezaji anapokuwa na mapungufu.

SOMA ZAIDI: FIFA Yatoa Kanuni Mpya za Uhamisho wa Wachezaji. Klabu Zetu Zinafuatilia?

Hayo yote yalitakiwa kufanyika ndani ya wiki moja kabla ya Yanga kukutana na Al Hilal, timu ambayo imemaliza katika nafasi ya kwanza ya kundi hilo ikiwa imepoteza mchezo mmoja tu na kutoka sare mmoja.

Haikuwa rahisi kwa Ramovic kufanya hayo yote ndani ya muda mfupi na kwenda uwanjani kupata matokeo dhidi ya Al Hilal na baadaye MC Alger, ambayo ndiyo imeizuia Yanga kuvuka kwenda hatua ya makundi.

Matokeo hasi

Yanga ikakubali vipigo vya mabao 2-0 kwa timu hizo mbili na hivyo kujenga msingi mbaya katika kundi lake. Kilichobakia katika mechi nne zilizosalia ni maajabu na maombi ili timu nyingine zifanye vibaya na kuweka huru tiketi za kufuzu hatua ya robo fainali. Ilishindwa kuchukua chake mapema kama ilivyokuwa kwa Al Hilal na MC Alger.

Ingawa Ramovic amekuja kueleweka kwa wachezaji na timu kurejesha makali yake, muda ulishakwenda na alikuwa akijenga nyumba juu ya msingi mbovu na hivyo matumaini ya kufanya vizuri yalikuwa yanaegemea kwenye miujiza na maombi, ambayo kila timu ilikuwa inayafanya na hivyo kumfanya Mungu aamue nani anastahili na si nani asaidiwe.

Pengine uamuzi wa kumtimua Gamondi ulikuwa sahihi kabisa kwa kuzingatia taarifa ambazo viongozi walizipata kuhusu tabia za kocha huyo ambazo ziliakisiwa kwenye matokeo ya mechi hizo mbili tu baada ya kocha huyo kutoka Argentina kuiongoza Yanga hadi robo fainali msimu uliopita na kutolewa kwa miujiza ya mpira wa miguu.

SOMA ZAIDI: Kukuza Netiboli Tanzania, Juhudi Zinahitaji Kurejesha Mapenzi, Unazi kwa Mchezo Huo Mkakati kwa Taifa

Lakini pengine wakati wa kumtimua Gamondi haukuwa sahihi. Timu ilikuwa na mechi muhimu za Ligi ya Mabingwa katika kipindi kisichopungua wiki moja kuanzia siku ambayo Gamondi alitimuliwa. 

Ingewezekana kabisa Ramovic angeshinda hizo mechi mbili zilizoiponza Yanga kuondokewa, lakini ushindi ungekuwa wa kufurukuta na si wa kisayansi, au usingekuwa wake kwa kuwa kwa kawaida kocha mpya hupewa mechi tano kabla ya kuanza kufanyiwa tathmini ya uwezo wake.

Masalia ya Gamondi

Kwa hiyo, tulichokiona katika mechi mbili za hatua ya makundi na nyingine tatu za Ligi Kuu kilikuwa ni masalia ya Gamondi yaliyokosa msimamizi sahihi kwenye benchi la ufundi ambaye angeweza kurekebisha makossa yaliyokuwa yakionekana uwanjani na timu kurudi kishujaa kama ambavyo “Yanga ya Gamondi” ilikuwa ikifanya kipindi cha pili.

Kuondolkewa kwa Yanga katika Ligi ya Mabingwa hakuwezi kuhusishwa na Ramovic kwa kuwa mechi zake zote za michuano hiyo zimekwenda vizuri, hata sare ya Jumamosi dhidi ya MC Alger ni matokeo mazuri kama Yanga ingekuwa imetengeneza mtaji mzuri katika mechi mbili za kwanza. 

Pia, kuondolewa huko hakuwezi kuhusishwa na Gamondi kwa kuwa hakuiongoza timu katika mechi hizo na hata kama alikuwa na udhaifu katika malezi, alijua afanye nini kupata ushindi, au kupata matokeo mazuri lakini fursa hiyo hakupewa.

SOMA ZAIDI: Ziko Wapi Hamasa za CHAN 2025?

Kuondolewa huko kunaweza kuhusishwa moja kwa moja na kufanya uamuzi sahihi kwa wakati usio sahihi. Haikuwa sahihi kumtimua kocha na wasaidizi wake katika kipindi ambacho timu inahitaji nguvu moja kupata matokeo mazuri katika michuano mikubwa.

Angalau ndani ya kipindi hicho, majukumu yangeenda kwa kocha ambaye angekuwa mmoja wa wasaidizi wake ili aendeleza falsafa ya kocha aliyetimuliwa na baadaye ndipo atambulishwe kocha mpya wakati timu ishakaa sawa na haina shinikizo la matokeo mazuri katika michuano mikubwa kama Ligi ya Mabingwa.

Ni muhimu kujua ni wakati gani wa kufanya maamuzi sahihi!

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts