The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ifike Wakati Maofisa Habari wa Klabu Waache Kupumbaza Mashabiki wa Soka

Watu hawa ndio wanapewa nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari bila ya tahadhari kuchukuliwa kuhusu athari ya kile wanachosema.

subscribe to our newsletter!

Kuna aina ya uvivu imeingia kwenye vyumba vya habari, hasa katika madawati ya michezo ambako hivi sasa wale watu rasmi, kama viongozi, makocha na wachezaji si muhimu katika utoaji habari, bali watu wanaoweza kuchekesha, au kusema magumu ambayo mtu anayewajibika katika taasisi hawezi kusema.

Mtu ambaye anasema anamuweka rehani mke wake iwapo timu fulani itashinda, si mtu anayewajibika kwa taasisi, jamii, na hasa familia yake.

Mtu anayesema timu yake ilipiga pasi milioni 90, hawezi kuwa anawajibika kwa taasisi yake, au chombo kingine chochote, kwa kuwa anazungumzia kitu ambacho hakiwezi kutokea kwenye mchezo wa mpira wa miguu.

Na sio hivyo tu, watu hawa hufikia kiwango cha kukejeli viongozi na hata wachezaji wao iwapo timu imekuwa na mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha.

Hawa ndio wanapewa nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari. Awali ilionekana kama ni vyombo vya mtandaoni pekee vinavyotafuta idadi kubwa ya kutazamwa, lakini hata redio zimeingia kwenye mkumbo huo, ambao binafsi nauona kama ni kutoyapa umuhimu maudhui rasmi na kutafuta hayo ambayo ni rahisi kuyapata.

SOMA ZAIDI: Uraia kwa Viungo Watatu wa Singida Big Stars Haukidhi Maslahi Yoyote ya Kisoka au Kitaifa. Ubatilishwe

Baadhi ya hao watu sasa wamekuwa maarufu. Kila mechi inapoisha, au jambo fulani kutokea, watu hawa wasiowajibika popote ndio hupewa nafasi kubwa ya kueleza jambo kwa fikra, au bila ya kuwa na sababu za kiufundi.

Watu kama mwenyekiti wa klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, waliwekwa katika hali ngumu na watu wa aina hii ambao hawawakilishi chombo chochote. Wakati Simba inafanya vibaya, walihusisha mwenendo huo na Mangungu bila ya kueleza alisababishaje yote hayo kutokea.

Ni bahati tu kwamba hakukuwepo na kikao cha wanachama wote wakati huo, la sivyo Mangungu angekuwa na wakati mgumu kikaoni kutokana na wanachama kulishwa maneno mabaya kumuhusu mbunge huyo wa zamani.

Watu hawa ndio wanapewa nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari bila ya tahadhari kuchukuliwa kuhusu athari ya kile wanachosema.

Na kwa sababu zilezile za kutaka kutazamwa na wengi, hivi sasa maofisa wa habari wa klabu ndio wamekuwa wasemaji wakuu wa kila kitu, ikiwa ni pamoja na kuzungumzia michezo ya timu yake kwa mapana na marefu.

SOMA ZAIDI: Yanga Haikufanya Uamuzi Sahihi kwa Wakati Sahihi Ilipoamua Kuachana na Miguel Gamondi

Hivi sasa huwezi kuwa ofisa habari wa klabu kama huna tabia ya kuchekeshachekesha au kuwa na maneno mengi. Na ukiwa ofisa habari lazima ufanye jitihada za kusemasema ili upate umaarufu utakaokufanya upate ajira nyingine pale utakapotimuliwa, au kama fikra za wengi zilivyo, ili upate ubalozi wa bidhaa.

Zile taarifa rasmi sasa si muhimu sana bali kutazamwa na wengi na hivyo hutumia muda mwingi kuchekesha kwa kuponda timu nyingine.

Kupata mahojiano marefu na kocha, au kiongozi, sasa si muhimu sana. Kocha atazungumza baada ya mechi tu, au kabla ya mechi, lakini si kupata muda wa kutosha kuzungumzia timu yake, muundo wa klabu zetu, soka la nchi kwa ujumla au mambo mengine ya kiufundi.

Yote hayo yatazungumzwa kimzahamzaha na maofisa habari wa klabu. Na kwa kweli wanachekesha, lakini wanapumbaza mchezo wa mpira wa miguu kwa kuwa jamii inaacha kufikiria mambo ya msingi na kujikita katika mambo ya mizaha.

Utashangaa kocha anazungumza baada ya mechi, lakini akitoka tu, umati wa waandishi unawakimbilia maofisa habari ambao katika hali ya kawaida wanatakiwa wasizungumze kuruhusu maneno ya kocha yawaingie mashabiki, lakini wao huzungumzia mchezo bila ya wasiwasi na kutumbukiza mizaha ambayo huchukua nafasi kubwa badala ya kile muhimu kilichozungumzwa na mwalimu.

SOMA ZAIDI: ‘Ilala ni Soka’ Ina Lengo Zuri Kukuza Soka Ngazi ya Vitongoji. Lakini Kuna Kasoro za Msingi

Matokeo yake, uelewa, au ufahamu wa mashabiki kuhusu falsafa ya kocha, unakuwa mdogo kwa kuwa akili zao zimejazwa mizaha na kejeli.

Mambo ya msingi kuhusu uendeshaji mpira katika ngazi ya klabu sasa si muhimu na unaweza usiyaone kwa kuwa hayapewi huo umuhimu na vyombo ambavyo moja ya majukumu yake makuu ni kuelimisha.

Wakati mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almasi Kasongo, alipotoa tahadhari kuwa wataadhibu maofisa habari wanaofanya mizaha, nilimwelewa ingawa sikujua atatumia mbinu gani kama chombo hicho hakina kanuni za udhibiti wa wasemaji.

Lakini kauli yake ilimaanisha kwamba mpira haujadiliwi kwa marefu na mapana yake, badala yake unajadiliwa kwa vichekesho na mizaha.

Kuna haja ya TPLB kuangalia ni jinsi gani itaweka mwongozo utakaolazimisha klabu kujikita katika kuzungumzia mambo yanayoendeleza mpira. Inaweza kuwa ngumu, lakini pakiwepo pa kuanzia, inawezekana mbona huko kwa wenzetu inawezekana?

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts