The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Uelewa wa Kisayansi na Kimila Unavyoweza Kusaidia Kuelewa Uotaji Meno wa Watoto

Kuota kwa meno ni hatua ya kawaida ya ukuaji wa mtoto, ingawa uzoefu hutofautiana kati ya watoto vivyohivyo kwa uelewa kati ya mzazi na mzazi.

subscribe to our newsletter!

Kuota meno ni hatua muhimu katika ukuaji wa mtoto. Baadhi ya watoto huanza kupata meno mapema tofauti na matarajio, wakiwa na miezi mitatu wakati wengine huanza kati ya miezi minne na saba ambao ni muda muafaka unaotarajiwa na wa kawaida kwa mujibu wa sayansi ya maendeleo ya ukuaji wa mtoto. 

Wengine huweza kuzaliwa na jino, au meno, hali inayojulikana kama meno ya kuzaliwa, au natal tooth, kwa kimombo, hali ambayo inatambulika kisayansi inayosababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo lishe, uzito wakati wa kuzaliwa.

Ni vyema kutambua kwamba, muda na dalili za kuota meno hutofautiana kutoka mtoto mmoja hadi mwingine, mara nyingi zikiathiriwa na vinasaba na mazingira. Mara nyingi mtoto anapoota meno mapema kwa muda usio tarajiwa, na hasa akizaliwanayo, wazazi wengi, kwa uelewa wa kitamaduni, huogopa.

Wazazi hawa hudhani huo ni mkosi, na huhakikisha wanayaondoa kwa njia za kienyeji, kama kumpeleka mtoto kwa waganga au vikongwe kuyasugua na majivu na dawa nyingine za miti shamba mpaka yapotee kabisa. 

Njia na imani hizi na nyingine nyingi huhatarisha afya ya mtoto kwa maana husababisha kuvuja damu na kupata vidonda kwenye fizi, hupelekea homa kali pia. Wale wenye uelewa wa sayansi ya meendeleo na hatua za ukuaji wa mtoto huchukua hatua sahihi za kumpaleka mtoto haspitali na kupata huduma stahiki.

SOMA ZAIDI: Akina Baba Ndiyo Wahusika Wakuu wa Ukatili Dhidi ya Watoto. Dondoo Hizi Zinaweza Kusaidia Kurekebisha Hali Hiyo

Katika jamii nyingi za Kitanzania, kuota kwa meno mara nyingine huhusishwa na hali inayoitwa ndui, au measles bandia kutokana na uhusiano wake na vipele vya ngozi. 

Wazazi wengi hutumia tiba za asili kama vile vipande vya miti ya mwarobaini, au mgomba kwa mtoto kutafuna, ikiaminika kuwa vinaweza kupunguza maumivu na kusaidia meno kuchomoza kwa urahisi. Njia nyingine ni kupaka dawa za mitishamba kwenye fizi au kumpa mtoto vipande vya matunda baridi kama embe au tikiti maji ili kupunguza maumivu.

Ingawa tiba za asili zinaweza kusaidia, ni muhimu kuwa makini na baadhi ya mitishamba ambayo huenda ikawa na madhara kwa afya ya mtoto. Kuepuka hivyo, ni vyema tutumie njia salama zilizothibishwa kisayansi kama vile kumpa mtoto pete ya silicone ya kutafuna iliyohifadhiwa kwenye friji, lakini si kwenye friza.

Njia nyingine ni pamoja na kumpa vyakula baridi, kama matunda laini, iwapo ameanza kula chakula kigumu; kupaka fizi za mtoto kwa kidole kilicho safi na kufanya masaji laini; na kutumia dawa za kupunguza maumivu kama paracetamol kwa idhini ya daktari.

Pia, tufahamu baadhi ya njia zinazotumiwa na wazazi zinazoweza kuwa hatari kwa afya ya mtoto, kama vile krimu na jeli za meno zenye kemikali kama benzocaine, lidocaine, au belladonna, ambazo zinaweza kuwa na madhara; vikuku na mikufu ya meno ambavyo vinaweza kusababisha hatari ya kumeza au kunyongwa; na aspirini, ambayo haipaswi kutumiwa kwa watoto kwani inaweza kusababisha ugonjwa hatari wa Reye’s.

SOMA ZAIDI: Leo Tuzungumze Mchango wa Kauli Chanya za Wazazi Katika Ukuaji wa Hisia, Akili wa Watoto

Kwa kawaida, watoto wengi hupata jino lao la kwanza kati ya miezi minne, sita na 12. Meno huanza kutengenezwa mtoto akiwa tumboni, lakini huchukua miezi kadhaa baada ya kuzaliwa ili yajitokeze. 

Baadhi ya watoto hupata meno kadhaa kwa wakati mmoja, huku wengine yakichomoza moja baada ya jingine. Ikiwa mtoto hajapata jino lake la kwanza hadi anapofikisha mwaka mmoja, ni vyema kushauriana na daktari wa watoto, au daktari wa meno, ili kuhakikisha hakuna changamoto zozote za kiafya.

Kwa kawaida, meno ya mtoto huota kwa mpangilio ufuatao: meno mawili ya katikati ya chini, au central incisors); meno mawili ya katikati ya juu; meno ya pembeni na nyuma, au canines na molars; na mwisho kabisa magego ya pili, ambayo hujitokeza karibu na umri wa miaka miwili. Ifikapo miaka mitatu, watoto wengi huwa na meno 20 ya utoto. 

Baadaye, kuanzia umri wa miaka sita, meno haya huanza kung’oka ili kupisha meno ya kudumu.

Watoto wengine hupitia kipindi cha kuota meno bila matatizo yoyote, lakini wengine hupata maumivu na usumbufu. Dalili za kawaida ni mtoto kuwa mkorofi au kulia mara kwa mara; kutokwa na mate mengi, jambo linaloweza kusababisha vipele usoni; fizi kuvimba na kuwa nyeti; mtoto kutafuna au kung’ata vitu mara kwa mara; homa ya chini ya kiwango (chini ya 38°C); matatizo ya usingizi; na mtoto kujikuna uso au kuvuta masikio.

SOMA ZAIDI: Fahamu Mbinu Zinazoweza Kuimarisha Mawasiliano Kati ya Mtoto na Mzazi

Kuota kwa meno ni hatua ya kawaida ya ukuaji wa mtoto, ingawa uzoefu hutofautiana kati ya watoto vivyohivyo kwa uelewa kati ya mzazi na mzazi. Kama tulivyoona hapo awali, kuwa na mchanganyiko wa maarifa ya kimila na uelewa wa kisayansi unaweza kutusaidia wazazi kukabiliana na kipindi hiki kwa usalama na ufanisi ili kulinda afya na ustawi wa watoto wetu.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts