The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Usalama wa Mtoto wa Kike Dhidi ya Ukatili wa Kinjinsia ni Jukumu la Nani?

Wazazi tuwe mstari wa mbele katika kuwaelimisha watoto wetu, kushirikiana na jamii, na kuhakikisha tunawalea mabinti zetu katika mazingira salama na huru.

subscribe to our newsletter!

Katika dunia inayobadilika kila siku, usalama wa wasichana unazidi kuwa suala la msingi kwa wazazi na jamii kwa ujumla. Miongoni mwa changamoto kubwa za vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyowakumba zinazowakumba mabinti zetu ni ukatili wa kijinsia (GBV), ambao hujumuisha vitendo vya unyanyasaji wa kimwili, kingono, kihisia, ndoa za utotoni na ukeketaji (FGM). 

Wiki hii tuliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji wa Wanawake na Wasichana (Februari 6), hivyo, ni muhimu kujadili njia bora za kuwalinda mabinti dhidi ya vitendo hivi vinavyovunja haki zao za msingi.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Utafiti wa Afya na Uzazi wa Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS-MIS) 2022/23, kiwango cha ukeketaji kwa wasichana wa umri wa miaka 15-49 nchini Tanzania kimeshuka hadi asilimia nane kutoka asilimia 10 mwaka 2015/16. 

Hii ni dalili kwamba juhudi za serikali na wadau zina matokeo, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya. Baadhi ya mikoa kama Manyara (43%), Mara (28%), na Singida (20%) inaendelea kuwa na viwango vya juu vya ukeketaji, hali inayoashiria haja ya kuongeza nguvu katika kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto wa kike katika maeneo haya.

Ukeketaji ni kitendo cha kikatili kinachowaathiri wasichana kimwili na kisaikolojia. Madhara yake ni pamoja na maumivu makali, matatizo ya uzazi, hatari ya maambukizi, msongo wa mawazo, na kupoteza hali ya kujiamini. Aidha, mara nyingi ukeketaji huenda sambamba na ndoa za utotoni, jambo linalozuia wasichana kupata elimu na fursa nyingine za maendeleo.

SOMA ZAIDI: Uelewa wa Kisayansi na Kimila Unavyoweza Kusaidia Kuelewa Uotaji Meno wa Watoto

Wazazi tuna nafasi kubwa katika kuhakikisha usalama na ustawi wa mabinti zetu, kwanza, wa kuwapatia elimu sahihi. Wasichana wanapaswa kufahamu haki zao za msingi, ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi bila hofu ya ukatili wa kijinsia. Wazazi tunapaswa kuwaelimisha juu ya madhara ya ukeketaji na ndoa za utotoni, huku tukiwaelekeza kuhusu umuhimu wa kusimama imara dhidi ya vitendo hivi.

Pili, tujenge mazingira salama ya watoto kuwa huru na sisi wazazi. Mabinti wanapokuwa na mahusiano ya karibu na wazazi wao, wanapata fursa ya kushirikishwa changamoto wanazokutana nazo. Wazazi tunahitaji kuwasikiliza watoto wetu bila hukumu, kuwawekea mazingira salama ya majadiliano, na kuwa tayari kuchukua hatua za kuwalinda pale inapohitajika.

Kama ule msemo unavyosema kuwa kidole kimoja hakivunji chawa ndivyo juhudi za mzazi mmoja haziwezi kuwa na matokeo makubwa bila ushirikiano wa jamii nzima. Kuwa na majukwaa ya majadiliano, vikundi vya kusaidianamsaada, na kushirikiana na mashirika yanayopingaambana na ukatili wa kijinsia kunaweza kusaidia kuongeza uelewa na kuchochea hatua madhubuti dhidi ya changamoto hii.

Ni vyema tufahamu kuwa vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia hutokana na fikra na imani za jamii. Hivyo kama jamii inatubidi kutafakari imani zetu na kujiuliza Je, imani hizi zinawalinda watoto wetu? Zinatengeneza mazingira bora ya ustawi wao? Zinawaandaa kuwa watu wazima wema wanaojiamini?

Pia, tukumbuke kuwa ulinzi na usalama wa mabinti zetu sio jukumu la wanawake peke yao. Wanaume na wavulana wanapaswa kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuelewa madhara ya vitendo hivi na kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii.

SOMA ZAIDI: Akina Baba Ndiyo Wahusika Wakuu wa Ukatili Dhidi ya Watoto. Dondoo Hizi Zinaweza Kusaidia Kurekebisha Hali Hiyo

Hatua muhimu

Serikali yetu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imechukua hatua kadhaa katika kupigania haki za watoto wa kike dhidi yakomesha ukeketaji. Hizi ni pamoja na kuanzisha kamati za ulinzi wa wanawake na watoto zaidi ya 18,000 katika maeneo mbalimbali nchini. 

Kuweka nyumba salama (Safe houseHomes) kwa ajili ya kuwahifadhi wasichana waliotoroka ukeketaji, kuanzisha vituo vya huduma jumuishi (One-Stop Centres) ili kutoa huduma za afya na msaada wa kisheria kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia pamoja na kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari, redio za kijamii, na mitandao ya kijamii ili kueneza ujumbe wa kuwalinda watoto wa kike dhidi ya ukeketaji.

Pia, Sheria ya Mtoto (Sura ya 13, Kifungu 158A) na Kanuni ya Adhabu (Sura ya 16, Kifungu cha 169A) zinaeleza kuwa mtu yeyote anayefanya ukeketaji anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka 5-15 au kutozwa faini ya kati ya shilingi milioni 1-2 au vyote kwa pamoja. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha ukeketaji unakomeshwa kabisa.

Kuwalinda wasichana dhidi ya ukatili wa kijinsia, hasa ukeketaji, ni jukumu letu sote. Wazazi tuwe mstari wa mbele katika kuwaelimisha watoto wetu, kushirikiana na jamii, na kuhakikisha tunawalea mabinti zetu katika mazingira salama na huru. Serikali, mashirika, na wadau wa maendeleo wanapaswa kuendelea kuimarisha juhudi za kuwalinda mabinti dhidi ya ukeketaji kwa kutumia elimu, sheria, na uhamasishaji.

Pamoja, tunaweza kujenga jamii inayothamini haki za watoto wa kike na kuhakikisha kila msichana anakua akiwa na ndoto na fursa za kufanikisha maisha yake bila hofu ya ukatili wa kijinsia.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts