Nimemaliza kusoma kitabu cha mchumi mbobezi, Jeffrey Sachs, kiitwacho The End of Poverty: Economic Possibilities for Our Time, au, kwa tafsiri isiyo rasmi, Mwisho wa Umasikini: Kinachoweza Kufanyika Kwenye Uchumi Katika Zama Zetu.
Hiki ni kitabu ambacho toka kitambo nilikimezea mate, nilikuwa na hamu ya kukisoma, labda ni kwa sababu ya kuushuhudia binafsi na kuuchukia umaskini. Nikiri kuwa ni kitabu kizuri kuanzia muundo na maudhui yake; mwandishi, kama mshauri-elekezi mzoefu katika suala zima la uchumi na sera zake, amekitendea haki na itifaki.
Kitabu kina taarifa nyingi muhimu na mbinu tofauti tofauti kuhusu maendeleo ya kiuchumi; kinakupa takwimu na mifano halisi ya kitafiti namna ya kuelewa uchumi sambamba na nyenzo za kupambana na hili jinamizi andamizi la umaskini. Hivyo basi, ningependa kuwashirikisha na kuwafikirisha kile ambacho nimejifunza katika kitabu hiki.
Naamini umaskini ni aibu na fedheha kubwa hasa kwa nchi tajiri kama Tanzania. Kwa taarifa yako, sisi, pamoja na ukwasi wa kila aina toka kusi hadi kasi, bado ni moja ya nchi ombaomba ambayo inategemea sehemu kubwa ya bajeti na misaada kutoka ng’ambo.
Hili ni ombwe kubwa na utegemezi unaotuvua nguo. Naam, umaskini ni mbaya sana kwani unapumbaza na kufubaza fikra, na kuhatarisha afya ya akili. Ni kama kupe anayenyonya hadhi na utu wa binadamu. Hata mwanafalsafa na nguli wa uchumi, Amartya Sen, katika kitabu chake, Development as Freedom, anasema kuwa umaskini siyo tu ile hali duni ya kukosa fedha na kujimudu, bali ni hali ya ndani kabisa ya kushindwa kutumia uhuru, vipawa na uwezo wako majaliwa.
Dimbwi la umasikini
Awali ya yote, Sachs anaeleza kwa masikitiko kuwa zaidi ya watu milioni mia saba (700,000,000) duniani wanaishi katika zimwi na dimbwi la umaskini. Hii ni zaidi ya idadi inayotisha, bali ni uhai wa watu ulio hatarini! Vilevile, kila siku watu wengi wanakufa kutokana na umaskini uliokubuhu.
Na, mbaya zaidi, ni kuwa nchi, au jumuiya ya kimataifa, haijafanya jitihada za kutosha kutokomeza huu umaskini ambao ni huzalishwa na kuendelezwa na mifumo ya kidunia; imewakatia tamaa maskini na kuwatelekeza pekee yao. Jambo hili linaleta tafsiri kuwa umaskini umehalalishwa na kutamadunishwa.
SOMA ZAIDI: ‘Animal Farm’ ya George Orwell Inavyotusaidia Kuelewa Dhana ya Uongozi wa Umma na Uwajibikaji
Vizazi na vizazi vinarithishana umaskini. Kumbe, umaskini kama vile vita siyo ajali bali hutengenezwa, hivyo kugeuka kuwa mtaji wa kisiasa ili kuendeleza matabaka na utawala hawala. Siasa na sera za kibepari zinahitaji mtaji wa umaskini wa wengi, au deliberate impoverishment of masses kwa kimombo, ili upumue na kushamiri.
Ndiyo kusema kuwa, taasisi, au nchi, zilizoendelea ambazo zinatumia sera na sheria za kibiashara ambazo ni za kinyonyaji ni maskini pia kwa namna fulani. Na mwandishi Sachs anadai mabadiliko ya kimfumo katika hizi taasisi. Maana, wanaoongoza taasisi za kifedha kama IMF na Benki ya Dunia zinawapendelea nchi tajiri.
Pia, sheria na kodi za biashara na mahusiano ya kimataifa si rafiki kwa nchi za dunia ya tatu. Itoshe kusema kuwa, wao wana ule umaskini wa kukosesha watu haki na usawa. Hawana utu na dhamira ya kweli. Umasikini wao, kwa lugha ya Kiingereza, huitwa anthropological poverty.
Mfano hai na halisi ni kinachoendelea nchini DRC ambayo ni nchi tajiri kwa madini ya Cobalt. Sasa, asilimia 70 ya hayo madini yanatumika kwa ajili ya kutengeneza magari ya umeme na vifaa vya kieletroniki, lakini yanatoka nchini DRC kwa njia za magendo, mauaji na makovu ya umaskini wa kupindukia.
Kama hilo halitoshi, vita vya DRC na huo umwagaji damu haupewi uzito unaostahili katika mahusiano na vyombo vya kimataifa, maana umaskini kwa asilia una tabia ya kile wanasema kwa Kiingereza making its victims invisible, au huwafanya waathirika wake wasionekane.
Umaskini maskani Tanzania
Hali ya umaskini ya Watanzania imetamalaki, inatisha na kukatisha tamaa. Ukipitapita hapa na pale na kujionea lindi la umaskini ni lazima roho ikuume, upate hasira na maswali mengi, kama sivyo basi una shida ya utashi.
Pamoja na hali hiyo wazi wazi, kinachosikitisha ni kwamba zile ‘hasira’ na hamasa, yaani harakati, au vuguvugu, za kitaifa za kupambana na umaskini zimepungua sana. Fikria, hata harakati hizo zimebinafsishwa, yaani kwa kiasi kikubwa kila mtu anapambana na hali yake.
SOMA ZAIDI: ‘Elimu Isipomkomboa Maskini, Basi Ndoto Yake ni Kuwa Mnyonyaji’
Mikakati na sera juu ya maskini ni hafifu bila meno, imetelekezwa. Kumbe, hali hizi za uduni na umaskini ilibidi zitutie hasira na kutuumiza vichwa ni jinsi gani tutamaliza hii aibu na taabu ya karne.
Pia, mwandishi anatuasa kuhusu lugha baguzi na mtazamo hasi juu ya maskini kama unatweza na kukoleza umaskini. Ni aghalabu kusikia asasi mbalimbali na wanasiasa wakichukua picha za maskini bila ridhaa yao, hali inayojulikana kama poverty porn, na wakisema kwa dharau: “Lazima kuwasaidia hawa maskini” au “Tunafanya haya yote kwa ajili maskini.”
Wanazungumza hivi kana kwamba si haki, bali ni fadhila au hisani fulani, kumbe wanafaidika kupitia mgongo wa maskini. Kwa hiyo, vita na maamuzi dhidi ya umaskini inahitaji lugha mbadala ya heshima na shirikishi, yanayojali mahitaji ya wahusika, ili maskini wenyewe wasijione wanyonge na wapokeaji tu wa misaada na makombo.
Ni bayana kwenye kitabu kuwa, umaskini una sura, jinsia na jiografia, yaani Afrika inaendelea kuzama na kudidimia kwenye umaskini licha ya utajiri wake lukuki. Tafiti zinaonesha kwamba umaskini wa kipato kwa wanawake ni changamoto kubwa ambayo huwatumbukiza katika ukatili wa kijinsia na manyanyaso mengi kwa sababu ya kuwa tegemezi.
Pia, hizo tafiti zinaweka wazi kuwa uchumi wetu Tanzania umeendelea kukua kitakwimu, lakini hauna faida/tafsiri halisi katika kupunguza umaskini, kuleta unafuu wa maisha na kuzalisha ajira-ujira. Na bajeti kuu ya nchi kwa asilimia kubwa ni zaidi kwa ajili ya matumizi na matanuzi na si kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Kutokomeza umaskini
Mijadala na ushauri nasaha kuhusu kutokomeza umaskini ni kemkem. Wengi wanasema tunaweza kumaliza umaskini kwa kuwakopesha mitaji maskini. Wengine, kama mchumi Dambisa Moyo kutoka Zambia anasema tuvae manda tujitegemee na kuachana na misaada kwa sababu inatulemaza, kama tunavyoona kasheshe ya USAID. Wengine wanasema tuwape maskini haki zao kwa kuimarisha taasisi za haki na kuzuia ukoloni wa ndani kwa kupora ardhi za jamii kama Wamasai.
Sachs anaeleza kuwa suala la umaskini ni nyeti. Anashauri kwanza tuuelewe umaskini kwa upana wake kama vile daktari anavyomwelewa mgonjwa wake. Umaskini ni kama vile wagonjwa wawili wenye dalili zinazofanana lakini wana magonjwa tofauti.
SOMA ZAIDI: Kwaheri Amir Sudi Andanenga, Tanzania Itakukumbuka Daima
Ama wanaweza hata kuwa na ugonjwa sawa lakini bado dawa zao zisifanane katu. Kwa hiyo, hakuna njia moja ya kumaliza gonjwa sugu la umaskini. Ni vizuri kuwa na muktadha mpana wa kila hali ya umaskini.
Mwandishi anatolea mfano wa nchi za China, Singapore na India, wamepiga hatua kubwa za kimaendeleo na kutokomeza umaskini kwa hasira, kwanza kutokana na uongozi mathubuti kuwekeza maeneo ya teknolojia, anga, afya, ufundi stadi, uhandisi, STEM.
Maana yake ni kuwekeza kwa nguvu endelevu kwenye Human Capital Development. Hiki kiwe kipaumbele na mpango wa kudumu. Kuwajengea wananchi uwezo na ustadi mbalimbali.
Basi pasi na shaka, njia nzuri ya kumaliza mtego wa umaskini lazima itoke ndani, iwahusishe wahusika. Ambao hawataki kuwa patronized. Njia mbadala haiwezi kuagizwa kutoka nje kwa misaada wala juu kwa jua la dua. Kwa sababu, bado kuna watu wanaamishwa tena kwa propaganda za kidini kuwa umaskini ni mpango wa miungu au laana/pepo fulani hivyo lazima kuombea udongo au ukoo, na kadhalika.
Ni kawaida sana kuwakuta Watanzania kwenye nyumba za ibada wakifunga na kuomba ili ‘pepo la umaskini’ liwatoke. Kwa namna fulani, wanachezewa hisia na imani zao bure kwa siasa za viinimacho.
Laiti kama wangetambua kuwa umaskini wao unatengenezwa kila uchao kwenye meza za maamuzi za watawala na majahili wao tena kwa gharama za kodi zao, wangeshamtoa huyu ‘pepo’ wa umaskini nduki ambaye anawakodolea macho kila leo kupitia hali ngumu ya maisha, ukosefu wa ajira na usawa. Umaskini kokote duniani hautaisha kwa kupiga ramli, kubashiri, maombolezo au maombezi fulani.
Lazima tunuie na tupambane na jinamizi hili la umaskini. Sach anashauri Serikali iwekeze katika sekta za kimkakati zinazogusa moja kwa moja maisha ya watu. Ndio maana, hata yale Malengo ya Milenia ya Maendeleo ambayo huyu mwandishi Sachs alihusika kutengeneza iliweka kutokomeza umaskini katika kizazi chetu.
SOMA ZAIDI: ‘Binadamu na Maendeleo’ Kinaonesha Kazi Tanzania Inapaswa Kufanya Kufanikisha Dira Alizohubiri Nyerere
Vivyo hivyo, Dira yetu ya maendeleo 2050 lazima iweke wazi mikakati ya dhati kumaliza kabisa janga na mnyororo wa umaskini. Kuwa na sera nzuri, mipango kabambe haitoshi, lazima kutekeleza na kuwajibishana ili kuwa na nidhamu ya fedha za umma, uchungu na rasmilimali za umma sanjari na utashi wa kisiasa kumaliza kabisa hii dosari na hasara ya umaskini.
Isaac Mdindile ni mwanaharakati wa haki za binadamu na mazingira. Kwa mrejesho anapatikana kupitia ezyone.one@gmail.com au X kama @IsaacGaitanJr. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.